JINSI KIJANA ANAVYOWEZA KUSHINDA TATIZO LA MAWAZO MABAYA

 


(Mwanzo 8:21)

UTANGULIZI

Vijana wanakabiliwa na matatizo mbalimbali, tatizo mojawapo ni MAWAZO MABAYA ambayo yako kwenye mioyo yao.

Biblia inathibitisha hilo kwenye kitabu cha Mwanzo 8:21, Mungu anasema mawazo mabaya huanza kwenye siku za ujana.

Nataka tuangazie mambo ya msingi sana kwenye mada hii, mambo hayo ni;-

1. Mawazo

2. Moyo 

Kwanza nataka ufahamu kuwa mawazo ni maneno yaliyomo moyoni mwa mtu, wazo ni neno lililomo moyoni mwa mtu, neno lolote ambalo halijatoka kinywani mwako linaitwa wazo.

Kuna mawazo ya aina mbili tu, kuna mawazo mema na mawazo mabaya. Mawazo mabaya ni pamoja na kujiua, kuua, kulipa kisasi, wizi, utoaji mimba, utapeli, kusaliti nakadhalika. 

Moyo ndio kibebeo au begi la mawazo (maneno) mbalimbali ambayo ni mazuri au mabaya, kwa hiyo huwezi kukabiliana na tatizo la mawazo mabaya bila kushughulika moyo wako au moyo wa kijana.

BAADHI YA VYANZO VYA MAWAZO MABAYA

1. Wivu (Mwanzo 4:3-8)

Baada sadaka ya Habili kupata kibali kwa Mungu na sadaka ya Kaini kukosa kibali kwa Mungu, Kaini alimwonea wivu ndugu yake, wivu huo ulileta wazo la kumuua ndugu yake.

Naamini umeshawahi kusikia mtu kamuua mwenziye kwa sababu ya wivu wa kimapenzi, wivu huzalisha mawazo mbalimbali ikiwemo kujiua, kuua nakadhalika.

2. Kukata tamaa au kuvunjika moyo.

Kuna watu wamejikuta wanasumbuliwa na mawazo mabaya baada ya kukata tamaa au kuvunjika moyo, wengine wamejiua, wamejiingiza kwenye uhalifu nakadhalika.

3. Tamaa ya mwili na tamaa ya mali na fedha.

Tamaa ya mwili husababisha watu kufanya matendo ya ubakaji nakadhalika. Tamaa ya mali husababisha watu kuua wenzao, kuiba na kufanya matendo mabaya.

4. Marafiki wabaya.

Vijana wengine wanateswa na mawazo mabaya kwa sababu ya aina ya marafiki walionao, marafiki wenye mawazo mabaya watakuambukiza mawazo mabaya.

Rejea vitabu hivi (Mithali 1:19)(Luka 15:11-13)(1 Timotheo 6:10).

5. Kutokusamehe.

Watu wengi husuani vijana wanateswa na mawazo mabaya kutokana na kutokusamehe waliowatendea mambo mabaya.

Usiposamehe utajikuta umekuwa mtu mwenye mawazo mabaya sana.

BAADHI YA MBINU ZA KUSHINDA MAWAZO MABAYA

1. Mwamini Bwana YESU ili aingie moyoni mwako (Ufunuo wa Yohana 3:20), Yesu akitawala moyoni mwako, mawazo mabaya hayawezi kukusumbua.

2. Weka neno la Mungu kwa wingi kwenye moyo wako ili mawazo mabaya yasiwe na nguvu ndani yako  (Zaburi 119:10-11)

3. Epuka marafiki wabaya (Mithali 13:20).

4. Samehe waliokutendea mabaya, hii ni njia mojawapo ya kuondoa mawazo mabaya kwenye moyo wako.


Chapisha Maoni

0 Maoni