KESI ISIYO NA MASHAHIDI NA USHAHIDI


 

Ukweli ni kwamba katika uendeshaji na usikilizaji wa kesi lazima kuwepo mashahidi wa pande zote mbili, mashahidi wa mshitaki na mashahidi wa mshitakiwa, ushahidi wanaouwasilisha mahakamani au mahali pa hukumu ndio unasaidia kumpa kila mmoja haki yake.

Bila mashahidi au bila ushahidi sio rahisi kupewa haki na kuendesha kesi. Huwezi kuwaambia mahakamani kwamba shahidi yangu ni Mungu wakakuelewa.

Lakini Biblia inaripoti kesi ambayo haikuwa na mashahidi au ushahidi, rejea kitabu cha kwanza cha Wafalme (1 Wafalme 3:16-28) lakini Mfalme alitenda haki.

Hii ni kesi ambayo Mfalme Sulemani alikuwa akimsikiliza mshitaki na mshitakiwa bila kuwepo kwa mashahidi na Mfalme alitenda haki. Maelezo ya aliyekuwa anashitaki yalitosha kabisa kufuta kesi ile lakini Mfalme aliisikiliza na akatenda haki, yule mshitaki alisema "mwanamke huyu alichukua mtoto wangu nilipokuwa nimelala usingizi halafu akaniwekea kifuani mtoto aliyekufa"

Maelezo yale yanazua maswali mengi ambayo yangeliweza kupelekea kesi kufutwa, kwa mfano angeulizwa "ulijuaje alikuwekea mtoto aliyekufa wakati unasema tukio hilo lilifanyika ukiwa usingini umelala? kimsingi ukiwa usingizini huwezi kujua yanayoendelea kwenye mazingira yako.

Lakini Mfalme Sulemani kwa hekima yake aliisikiliza hiyo kesi isiyo na ushahidi na mashahidi na akatenda haki.

MFALME SULEMANI ALIWEZAJE KUTENDA HAKI KWENYE KESI ISIYO NA MASHAHIDI AU USHAHIDI?

Alikuwa na hekima ya Mungu.

Alisikiliza pande zote na akalinganisha maneno ya wahusika (mshitaki na mshitakiwa) na maelezo yao kwa makini sana kisha akatumia hekima kutoa hukumu.

HITIMISHO

Ni kweli usiopingika kwamba kesi isiyo na mashahidi au ushahidi ni vigumu kuishughulikia, inachukua muda kutoa hukumu nakadhalika.

Lakini Mfalme Sulemani alikabiliana na kesi kama hiyo na akatenda haki ndani ya muda mfupi sana.

Tukio hilo linatupa ufahamu kuwa kutenda haki inawezekana hata kama mazingira ya kesi yamejaa utata mwingi sana.

Tunachohitaji ni hekima ya Mungu na kusudio la dhati la kutenda haki.

Chapisha Maoni

0 Maoni