Faraja Gasto
1.UTANGULIZI
2.MADHARA YA
LAWAMA
3.MAMBO YA
KUFANYA IKIWA TATIZO LIMESHATOKEA
4.JAMBO LA
KUFANYA IKIWA UNALAUMIWA
UTANGULIZI
Katika kuishi kwetu duniani huwa tunajikuta tukikumbana
na matatizo mbalimbali, matatizo hayo yapo katika makundi makuu mawili;-
a).Yale tuliyosababisha au tunayosababisha
wenyewe
b).Yale tuliyosababishiwa au
tunayosababishiwa na wengine kama vile ndugu, jamaa, marafiki, wazazi, waume au
wake zetu n.k
Matatizo hayo yanapokuwa yametokea huwa tunajikuta
tukiwa tumebeba LAWAMA, pale tunapojua au tunapohisi tatizo au matatizo hayo
yamesababishwa na watu wengine huwa tunajikuta tukiwatupia lawama watu hao
tunaojua au tunaohisi ndio chanzo cha tatizo au matatizo yaliyotupata au
yanayotupata.
Mara nyingi tunapokuwa tumejisababishia
wenyewe matatizo Fulani huwa inakuwa ngumu sana kukubali kwamba sisi ndio
chanzo cha tatizo au matatizo, watu wengi huwa wanaanza kutafuta mchawi wao
hata kama mchawi wa maisha yao ni wao wenyewe, na hii ni asili ya dhambi
inayosababisha hali hiyo.
(Mwanzo 3:9-19)
Adamu alipokubali ushawishi wa mke wake kwa
kukubali kula tunda ambalo Mungu aliwazuia wasile walijikuta wako uchi na
kutokana na aibu wakaaamua kujificha ili Mungu asiwaone, lakini baada ya Mungu
kuwafuata na kuwauliza kwa nini wamekula tunda, Adamu akaanza kumtupia lawama
mke wake, mwanamke naye alipoulizwa akaanza kumtupia lawama nyoka.
Tunaona hapo kila mtu anakwepa kuwa yeye
hakusababisha tatizo hilo hapo bustanini, kilichotokea ni kwamba Mungu
aliwatengenezea mavazi akawavika kasha akawafukuza kutoka bustanini hapo ndipo
ukawa mwanzo wa matatizo na mateso katika maisha ya Adamu na mkewe na pia
wanadamu wote waliofuatia.
Tabia ya kutokukubali kosa na kuwatupia lawama
wengine ilianzia hapo bustanini, Adamu alidhani kwa kumtupia lawama mke wake
ingesaidia kutatua tatizo kumbe ndio alikuwa anaamsha vitu vingine, mwanamke
alidhani kumtupia lawama nyoka ingesaidia kutatu tatizo kumbe haikusaidia kitu
chochote.
Kwa hiyo tunachojifunza ni kwamba “Lawama
hazijawahi kuwa dawa ya kutatua tatizo au kuleta ufumbuzi wa tatizo” na muhimu
kukumbuka au kufahamu kuwa “Mungu ndiye bingwa wa kutatua matatizo”.
MADHARA YA
LAWAMA
1.Lawama
inalifanya tatizo lizidi kuwepo.
Watu wengi utawasikia wakisema mimi niko hivi
kwa kuwa wazazi hawakunisomesha, tuko hivi kwa kuwa baba alitutelekeza, wengine
utasikia wakisema tuko hivi kwa kuwa serikali yetu haitujali n.k hizo ni baadhi
ya lugha za lawama ambazo zinasikika vinywani mwa watu.
Watu wengi hawafahamu kuwa lawama ni njia
mojawapo ya kulijengea boma tatizo, pale watu wanapolaumiana wanakuwa
wanalijengea ngome tatizo na ndio maana ukichunguza kwa makini utagundua mahali
popote penye lawama huwa kunakoseakana ufumbuzi wa tatizo kwa kuwa kazi
mojawapo ya lawama ni kuondoa umoja, umoja unapokosekana ghafla matengano
yanaingia na matengano yanapoingia kunakosekana watu wa kushughulikia tatizo
lililotokea.
(Mwanzo 3:9-19)
Tunaona Adamu na mkewe walipoanza kulaumiana
kilichotokea ni kwamba kila mmoja alikuwa anasema yeye sio chanzo cha tatizo
bali ni mwenzake, maana yake ni kwamba kila mtu anajiondoa kwenye hatia ya
kusababisha hiyo shida.
Kinachotokea pale watu wanapolaumiana ni
kwamba mara nyingi watu wengi wanakuwa wakijitetea kuwa wao hawakusababisha
shida au tatizo kwa hiyo suala la kutatua tatizo au shida hiyo haliwahusu kwa
kuwa wao hawakuisababisha, kwa kufanya hivyo wanakuwa wanalijengea ngome tatizo
na matokeo yake tatizo hilo linazidi kuwepo na kuwasumbua.
2.Lawama ni
njia mojawapo ya kuchelewesha maendeleo au mabadiliko.
Zipo njia nyingi sana zinazochelewesha
maendeleo au mabadiliko katika maisha ya mtu binafsi, familia, kanisa, taasisi,
taifa n.k njia mojawapo ni LAWAMA au kulaumiana.
Kwa mfano katika familia nyingi ukikuta baba
na mama ni watu wa kulaumiana kila wakati ukichunguza kwa makini familia hiyo
huwa haina mabadiliko au maendeleo, utakuta maisha ya familia hiyo ni yaleyale
miaka nenda rudi.
Ukiona katika nchi yoyote au taifa lolote
kuna siasa za kulaumiana kila wakati ukichunguza kwa makini utagundua maendeleo
au mabadiliko huwa yanachelewa sana kwenye hilo taifa au hiyo nchi kwa sababu
lawama ni njia ya kuchelewesha maendeleo.
(Hesabu 12:1-16)
Ukisoma andiko hilo utaona Miriamu na Haruni
wakaanza kumtupia lawama Musa kwa nini ameoa mwanamke ambaye sio wa jamii yao,
Musa alioa mwanamke wa kiafrika na hali hiyo ikasababisha hao wenzake wakaanza
kumlaumu, Mungu alipoona hivyo ilibidi amshughulikie Miriamu aliyeanzisha hiyo
mada ya lawama mwishowe Miriamu akawa na ukoma.
Ukoma wa Miriamu ulisababisha wana wa Israeli
wasiendelee na safari ya kuelekea nchi ya ahadi(Kanaani) kwa kuwa Mungu alisema
Miriamu atengwe nje ya kambi yao muda wa siku saba na baada ya siku saba ndipo
atajumuika na msafara huo, ni uhimu ufahamu kuwa walikuwa wanazidi kuchelewa
kufika kanaani kwa sababu ili safari iendelee walitakiwa wake pale mpaka muda
wa Miriamu kutengwa uishe ndipo waendelee na safari.
Suala la kulaumiana liliwatesa sana wana wa
Israeli, hili ni suala mojawapo lililowachelewesha kufika kanaani kwa kuwa mara
zote lawama zilikuwa zinawafanya wasiendelee na safari yao ya kuifikia nchi ya
ahadi.
Suala kama hili la kulaumiana ni mojawapo ya
sababu ya kutoendelea kwa mataifa mengi ya bara la Afrika kwa kuwa hata siasa
zinazofanyika Afrika ni za lawama, vyama tawala vinatupia lawama vyama vinzani
kuwa vinasababisha matatizo kwenye nchi, wakati huohuo na vyama pinzani
vinatupia lawama kwa vyama tawala kuwa vinasababisha matatizo katika nchi
mwishowe kunakosekana sauti moja na nguvu ya pamoja ya kuleta maendeleo au
mabadiliko katika nchi.
3.Lawama zinawafanya
watu watumie muda wao vibaya kwa kufanya
mambo yasiyo ya msingi
Mara nyingi watu wengi wanatumia muda mwingi
kutupiana lawama pale tatizo linapokuwa limetokea, muda ambao watu wanautumia kutupiana
lawama laity wangeutumia muda huo kutafuta ufumbuzi wa tatizo ni hakika
ufumbuzi ungekuwa umepatikana hata kama si wa kulimaliza kabisa tatizo ila kwa
kiasi Fulani wangekuwa wamelipunguza.
(Habakuki 1:12-17, 2:1)
Katika kipindi hiki ambapo mtumishi wa Mungu
Habakuki aliishi palikuwa na matatizo mengi sana; mahakamani watu walinyimwa
haki zao, wenye pesa ndio walikuwa miungu watu na matatizo mengine mengi sana,
kutokana na hali hiyo mtumishi wa Mungu Habakuki alijikuta anamtupia lawama
Mungu kwa nini haingilii kati hali hiyo, ukisoma wakati Habakuki anamtupia
Mungu lawama, Mungu alinyamaza kimya wala hakujibu chochote.
Habakuki alitumia muda mwingi sana kulaumu,
na hii ni tabia ya watu wengi pale tatizo linapotokea wanajikuta wanatumia muda
mwingi sana kulaumu badala ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo.
4.Lawama
zinasababisha chuki, ugomvi, matengano n.k
(Mwanzo 45:21-24)
Kama huwa unasoma Biblia hasa kama umewahi
kusoma kitabu chote cha Mwanzo naamini unazijua habari za kijana aitwaye Yusufu,
Yusufu ni kijana aliyeuzwa na ndugu zake katika nchi ya Misri na kwa kuwa Mungu
alikuwa pamoja naye Yusufu alifanikiwa sana katika nchi ya ugeni hata akawa
kiongozi mkubwa sana wa serikali, Yusufu ndiye ambaye alikuwa na mamlaka ya
mwisho ya maghala ya vyakula katika nchi ya Misri na kwa kuwa nchi ya Misri kwa
kipindi hicho ndio ilikuwa nchi yenye chakula cha kutosha nchi nyingi zilikuja
Misri kununua chakula.
Kutokana na njaa ya kipndi hicho hata ndugu
wa Yusufu walikuja Misri kununua chakula na hatimaye Yusufu aliwafahamu ndugu
zake na akaamua kujitambulisha kwao kuwa yeye ndiye Yusufu waliyemuuza nchini
Misri, wakati Yusufu alipoagana na ndugu zake wakiwa wanarudi kwao aliwaambia
“msigombane njiani” Yusufu aliwaambia hivyo kwa kuwa alikuwa na uhakika katika
safari yao wangeanza kutupiana lawama kwa kuwa miongoni mwao walikuwemo watu
waliomuuza kwa hiyo lazima wangetupiwa lawama na lawama hizo zingezalisha
ugomvi miongoni mwao ndio maana akawaambia msigombane njiani.
Lawama zinazalisha chuki, ugomvi na matatizo
mengine mengi sana kwa hiyo si vema kutupiana na lawama.
MAMBO YA KUFANYA IKIWA TATIZO LIMESHATOKEA
Hizi ni hatua za kufuata ili kupata suluhisho
la tatizo lililotokea
1.Acha
Kulaumu
Nimekuonyesha madhara ya lawama katika
kipengele kilichopita, kwa hiyo tatizo linapokuwa limekwisha tokea, jambo la
kwanza la kufanya ni kuacha kulaumu au kulalamika.
Ni muhimu kukubali kuwa tatizo limekwisha
kutokea na ili liondoke lazima upatikane ufumbuzi.
(2 Wafalme 7:3-5)
Ukisoma hilo andiko utaona habari za wakoma
wane waliokuwa wametengwa na jamii na wakati huohuo palikuwa na njaa kali sana
katika taifa lao kwa hiyo wanakabiliwa na matatizo mawili; tatizo la kwanza ni
ukoma na tatizo la pili ni njaa kwa hiyo ilifika hatua wakasemezana, wakasema
tukiingia mjini tutauawa kwa kuwa tumetengwa kwa sababu ya ukoma, tukikaa hapa
tutakufa na hata tukisema twende kwa maadui zetu tutauawa.
Hao wakoma hatuoni mahali popote
wanapowatupia lawama watu wengine
kutokana na matatizo waliyonayo badala yake wanawaza namna ya kutatua matatizo
yanayo wakabili, kwa hiyo pale ambapo tatizo linakuwa limekwisha kutokea ni muhimu
kuacha kulaumu kwa kuwa ukikaa unalaumu hautapata ufumbuzi wa tatizo hilo.
2. Tafuta
Ufumbuzi Wa Tatizo
Kwanza kabisa ni muhimu kufahamu Mungu huwa
anafanya nini pale tatizo linapokuwa limekwisha kutokea.
Kwa mfano, wote tunafahamu kwamba dhambi ni
chanzo mojawapo cha matatizo hata Mungu hapendi kuona watu wakitenda dhambi na
mara zote huwa anatoa adhabu kwa watenda dhambi, lakini Mungu huwa haanzi kwa
kutoa adhabu, Mungu huwa anaanza kwa kutoa onyo kwa mwenye dhambi ili aachane
na dhambi zake na hata kama mtu huyo hakuacha na hatimaye matatizo yakampata,
Mungu huwa huwa anatafuta mtu ambaye atasimama mbele zake ili apewe maelekezo
ya kutatua tatizo lilokwisha kutokea (Ezekieli
22:30-31)
Kuna njia mbili za kutafuta ufumbuzi wa
tatizo, ila ni muhimu kufahamu hili “kutafuta ufumbuzi wa tatizo sio kutatua
tatizo bali kutafuta ufumbuzi ni njia ya kufikia utatuzi wa tatizo”
Njia mojawapo ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo
ni kujua kwanza chanzo cha tatizo kwa sababu huwezi kutatua tatizo mbalo haujui
chanzo chake, unaweza ukafahamu chanzo cha tatizo kwa kufanya mambo mambo
mawili (a) kwa kumuuliza Mungu (b) kwa kutathmini au kutafakari
(2 Samweli 21:1)
Ukisoma habari hiyo utaona kulikuwa na njaa
katika utawala wa Mfalme Daudi kwa muda wa miaka mitatu, nina uhakika ndani ya
miaka miwili Mfalme Daudi na wataalamu waliokuwepo kwenye ufalme wake
walihangaika sana kutafuta ufumbuzi wa tatizo la njaa lakini hawakupata
ufumbuzi wa tatizo hilo ndipo Daudi alipoamua kwenda kuutafuta uso wa Bwana na
Bwana akamwambia chanzo cha tatizo, Mfalme Daudi aliposhughulikia chanzo cha
tatizo ndipo tatizo likaisha.
CHA KUJIFUNZA HAPO: Kuna matatizo mengine yanaweza
kutatuliwa kwa njia za kitaalamu na kuna matatizo huwezi kuyatatua kwa kutumia
utaalamu bali yanahitaji maelekezo kutoka kwa Mungu mwenyewe kwa hiyo ni muhimu
kufanya kama alivyofanya Mfalme Daudi alipoona njia za kitaalamu zimegoma
aliamua kumtafuta Mungu.
(Yona 1:1-15)
Yona aliwaponza watu aliokuwa nao kwenye meli
kwa kuwa alikataa kwenda kule alikotumwa na Mungu, Mungu akaichafua Bahari Yona
na wenzake wakawa kwenye wakati mgumu kwa hiyo kila mtu akaanza kumuomba Mungu
wake, mwishowe hawa watu wakapata wazo la kupiga kura ili wajue kwa nini
wamekumbana na hilo tatizo, walianza kutafakari mambo kadhaa.
(a).Wakati dhoruba inaanza Yona alikwenda
kulala pande za ndani za meli
(b). Wakati wao wanaomba Yona alikuwa amelala
Walipotafakari haya wakagundua kuwa Yona
ndiye chanzo cha tatizo ndipo wakaanza kumhoji yeye ni nani, katoka wapi na kwa
nini hayo mabaya yamewapata, mwishowe Yona aliwapa wazo wamtupe Baharini,
walipomtupa baharini tatizo likaisha.
JAMBO LA KUFANYA IKIWA UNALAUMIWA
Kuna wakati mtu hujikuta akilaumiwa
haijalishi lawama hizo ni za kweli au si za kweli, ukilaumiwa halafu na wewe
ukarudisha lawama utakuwa unachochea moto mwingine pasipo kujua.
Ikiwa unalaumiwa kwa jambo Fulani ni vema
ukafanya jambo hili;-
Tafakari je! Lawama hizo ni za kweli au si za
kweli
Kuna wakati unaweza ukalaumiwa kwa sababu ya
hila za watu ila kuna wakati unaweza ukalaumiwa kwa sababu wewe ndiye
uliyesababisha tatizo Fulani, kwa hiyo unapotafakari ukagundua lawama hizo sio
za kweli ni muhimu UNYAMAZE Mungu atakutetea lakini kama lawama hizo ni za
kweli basi ni muhimu kuomba Mungu akaurehemu kwa sababu umekuwa chanzo cha
tatizo Fulani.
(Hesabu
16:1-46)
Ilifika hatua kundi Fulani likainuka kinyume
na Musa wanamlaumu Musa amekaa madarakani muda mrefu, wakamwambia muda wa kukaa
madarakani umeisha hebu tuache na sisi tuongoze, Musa aliposikia hayo
akawaambia Bwana ataonyesha ni nani aliyemchagua kuongoza wana wa Israeli,
baada ya hapo Mungu aliliangamiza lile kundi lakini baada ya hao watu kuuawakundi
linguine likainuka kinyume na Musa na Haruni wakawaambia “ninyi ndio mmewaua
watu wa Mungu” jambo hilo lilimkasirisha Mungu akaamua kuwaangamiza wale watu.
Tunachojifunza hapo ni kwamba Musa
alipolaumiwa hakujitetea bali alimuachia Mungu aliyempa hiyo Nafasi amtetee.
HITIMISHO
Mungu akubariki, ni ombi langu kwa Mungu
uyatendee kazi haya uliyojifunza.
1 Maoni
Ameen
JibuFuta