(1 Wakorintho 3:1-)
UTANGULIZI
Mtume Paulo aligundua Wakorintho ni watu wa kimwili (watu wa tabia ya mwilini - wanaenenda kimwili) kutokana na tabia zao, alipojua tabia zao akagundua wanaenenda kimwili.
Mtume Paulo aliwaandikia waraka watu waliookoka akasema katika kanisa la Korintho kuna watu wa tabia ya mwili, kwa hiyo ni sawa na kusema kwamba kuokoka hakukufanyi kuwa mtu wa tabia ya rohoni ila kuokoka ni kuingia kwenye njia ya kuwa mtu wa tabia ya rohoni ndio maana Wakorintho walikuwa wameokoka ila bado walionekana na tabia ya mwilini (walienenda kimwili)
Kwa hiyo tunaweza kuwatambua watu wa kiroho (watu wa tabia ya rohoni) na watu wa kimwili (watu wa tabia ya mwilini) kupitia TABIA ZAO.
TABIA 7 ZA WATU WA TABIA YA ROHONI
1. Hawana makundi makundi (hawana migawanyiko)
(1 Wakorintho 3:3-6)
Katika kanisa la Korintho lilikuwa na migawanyiko (watu waligawanyika katika makundi makundi) wengine walisema wao ni wa Paulo wengine wakasema wao ni wa Apolo. Mtume Paulo alikemea migawanyiko hiyo.
Mtume Paulo aliwaita hao Wakorintho watu wa tabia ya mwilini kutokana na makundi yaliyokuwepo katika kanisa.
Watu wa tabia ya rohoni hujitenga au huepuka makundi (migawanyiko).
2. Hawafanyi vita kwa jinsi ya kimwili bali kwa jinsi ya rohoni.
(2 Wakorintho 10:3-5) kufanya vita kwa jinsi ya kimwili ni kupigana na watu na shetani kwa kutumia silaha za kimwili (panga, bunduki, mishale nakadhalika).
Kupigana vita kwa jinsi ya rohoni ni kupigana na watu au shetani kwa kutumia silaha za kiroho (silaha za Mungu) ambazo baadhi zimetajwa katika kitabu Waefeso 6:12-18).
Kwa mfano huwezi kupigana na pepo wachafu au kuwatoa Pepo wachafu kwa mapanga ila ukitumia silaha za kiroho unaweza kupigana na pepo na kuwashinda.
Watu wa tabia ya rohoni wanapigana vita kwa kutumia silaha za Mungu na sio silaha za kimwili kama vile mikuki, mapanga nakadhalika.
3. Wanaenenda kwa Roho.
(Wagalatia 5:16)
Kuenenda kwa Roho ni kuenenda kwa kumfuata Roho Mtakatifu au kwa kuongoza na Roho Mtakatifu.
Watu wa tabia ya rohoni hawafuatishi namna ya dunia hii (hawafuatishi mitindo ya kidunia, hekima ya kidunia) bali wanafuata uongozi wa Roho Mtakatifu katika mambo yote ya maisha haya.
Kwa mfano Mtume Paulo alizuiwa na Roho Mtakatifu asihubiri injili mahali Fulani na akatii (Matendo ya Mitume 16:6), wakati fulani Mtume Paulo akiwa na Timotheo walitaka kwenda mahali panaitwa Bithinia lakini Roho Mtakatifu akawakataza wasiende na walitii.
Watu wa tabia ya rohoni hawaenendi kwa jinsi ya mwili (kwa matakwa yao, Kwa utashi wao, kwa ujuzi wao) bali wanaenenda kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu.
4. Hudhihirisha tunda la Roho kupitia TABIA.
(Wagalatia 5:22-23) Biblia inasema "Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.
Watu wa tabia ya rohoni hudhihirisha upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi kupitia tabia, ni sawa na kusema kwamba "tunda la Roho ni tabia ya watu wa rohoni (watu wa tabia ya rohoni)
5. Ni watu wa utaratibu au wanaenenda kwa utaratibu.
Kuenenda kwa utaratibu ni kuenenda kwa kufuata mpangilio wa mambo, kufuata ratiba, kufuata kanuni, kuenenda sawasawa na unavyopaswa kuenenda, kuishi sawasawa na unavyopaswa kuishi na kufanya jambo kama jinsi linavyopaswa kufanywa kwa mujibu wa neno la Mungu.
Kwa mfano Mungu alipomuumba Adamu na kumuweka kwenye Bustani ya Edeni, Mungu alimpa utaratibu wa kuishi pale bustanini (Mwanzo 2:15-17). Adamu na mkewe walipoacha kuzingatia utaratibu ambao Mungu aliwapa, walisababisha matatizo makubwa sana kwao binafsi na kwa dunia kwa ujumla.
Biblia imezungumza mambo mengi sana kuhusu utaratibu , baadhi ya maandiko ambayo unaweza kuyapitia ni (2 Wathesalonike 3:7)(2 Wakorintho 10:1)(1 Wathesalonike 5:14)(2 Wathesalonike 3:6-11)
Mambo yasipofanyika kwa utaratibu ni sawa na machafuko, Mungu si Mungu wa machafuko (1 Wakorintho 14:33) (Yakobo 3:16)
6. Hawana tabia ya kupenda fedha.
Biblia imezungumza mambo mengi sana kuhusu kupenda fedha, kwa mfano Biblia inatuambia kupenda fedha ni tabia ambayo hatupaswi kuwa nayo (Waebrania 13:5) tena Biblia inasema shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha (1 Timotheo 6:10), Biblia inasema sifa mojawapo ya mtu anayetaka kuwa Askofu "asiwe mtu anayependa fedha" (1 Timotheo 3:2-3) pia Biblia inasema siku za mwisho watu watakuwa wakipenda fedha (2 Timotheo 3:2)
Kuna tofauti kubwa kati ya kuhitaji fedha na kupenda fedha, ukweli ni kwamba kila mtu anahitaji fedha kwa ajili ya mambo mbalimbali kama vile kununua chakula, kupeleka watoto shule, kujenga nyumba, kulipia bili za aina mbalimbali nakadhalika.
Kupenda fedha ni nini?
Kupenda fedha ni shauku au hamu ya kutaka kuwa na fedha au kupata fedha wakati wote kwa kutumia njia yoyote ile (halali au haramu). Ukiniuliza nini kiliharibu utumishi na maisha ya Mtume Yuda Iskariote nitakujibu ni TABIA YA KUPENDA FEDHA.
Kupenda fedha ni tabia ambayo watu wa tabia ya rohoni wanaiepuka sana kwa kuwa tabia hii ni mojawapo ya tabia mbaya sana inaharibu watu, inachafua utumishi wa mtu, inaingiza roho za kuzimu ndani ya mtu nakadhalika, tabia ya kupenda fedha ilisababisha Gehazi ambaye alikuwa mtumishi wa Nabii Elisha akapatwa na ukoma na wazao wake (2 Wafalme 5:27)
Baadhi ya mifano ya watu wa tabia ya rohoni walioepuka tabia ya kupenda fedha, nitafundisha kupitia visa vya watumishi wa Mungu ambao ni Nabii Elisha, Mtume Petro na Mtume Yohana.
(a) Baada ya Naamani kupona ukoma alirudi kwa Nabii Elisha akiwa na vitu mbalimbali ikiwemo fedha lakini Nabii Elisha alikataa kuchukua vitu hivyo (2 Wafalme 5:16-17). Gehazi alichukua fedha na mavazi kutoka kwa Naamani hatimaye akapatwa na ukoma wa Naamani.
(b) Simoni alikuwa mchawi, baada ya kuokoka aliona watu wanapokea Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya Mtume Petro na Mtume Yohana akatamani apate uwezo huo wa kuwawekea watu mikono Ili wapokee Roho Mtakatifu, aliamua kuwapa fedha wakina Petro na Yohana ili wampe uwezo ambao utamsaidia akiwawekea watu mikono watapokea Roho Mtakatifu lakini MITUME WALIKATAA FEDHA ZAKE.
7. Maombi na maombezi.
Tofauti ya maombi na maombi ni kwamba "maombi - unajiombea mwenyewe ila maombezi ni kuombea wengine"
Watu wa tabia ya rohoni sio wabinafsi (hawajiombei wenyewe tu) bali wanawaombea na wengine (Waefeso 6:18-19)
Kuomba na kuombea wengine sio suala la muda kwa watu wa tabia ya rohoni bali kuomba na kuombea wengine ni TABIA YA WATU WA ROHONI (WATU WA TABIA YA ROHONI).
HITIMISHO
Zipo tabia nyingi sana za watu wa rohoni (watu wa tabia ya rohoni) ila nimefundisha hizo saba ili kukupa au kuongeza ufahamu kuhusu tabia za watu wa rohoni.
Unapaswa kuwa mtu wa tabia ya rohoni kwa sababu zifuatazo;-
1. Watu wa tabia ya mwilini ni milango ya ibilisi, ibilisi hupitishia vitu vyake kupitia watu hao ili kutimiza makusudi yake.
2. Watu wa tabia ya rohoni ndio watu wanaofanya ibada halisi (Yohana 4:24).
3. Unapaswa kuwa mtu wa tabia ya rohoni kwa kuwa ulizaliwa mara ya pili kwa Roho Mtakatifu kupitia mbegu ya neno la Mungu (1 Petro 2:23)(Tito 2:4-5)
0 Maoni