MKRISTO NA UCHUMI



                                                           NA:MWL MWAKASEGE

🔄MAMBO MANNE UNAYOPASWA KUYAJUA

Kuna mafundisho ambayo si sahihi yaliyowafanya wakristo wengi hasa wale waliookoka kutokujua cha kuamini juu ya uhusiano wa ukristo wao na utajiri. Na tuangalie maeneo manne yafuatayo ambayo wakati mwingine yamezaa mafundisho yasiyo sahihi:

1
.TAJIRI NA UFALME WA MUNGU:

Nadhani utakuwa umewahi kusikia watu wakisema; “Matajiri hawataurithi ufalme wa Mungu” Na wanasema ndivyo Bwana Yesu alivyosema baada ya tajiri aliyetaka uzima wa milele kukataa kuuza mali yake.

Hata mimi mwanzoni ilikuwa karibu sana nikubaliane na usemi huu. Lakini baada ya kuyachunguza maandiko niliona ya kuwa Yesu Kristo hakusema hivyo bali anasingiziwa tu.

Yesu Kristo alisema hivi;“Kwa shida gani wenye mali WATAUINGIA ufalme wa
Mungu”(Luka 18:24)
Kwa mstari huu tunajua ya kuwa Yesu Kristo hakusema ya kuwa wenye mali hawatauingia ufalme wa Mungu; bali alisema “kwa shida gani wenye mali watauingia ufalme wa Mungu!”

Na akaendelea kusema, “ Kwa maana ni vyepesi ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.” (Luka 18:25). Na wale waliosikia wakashtuka na kushangaa, kwa maana waliona itakuwa vigumu sana kwa tajiri kuokoka, na naona walifikia mawazo kama waliyonayo wengi siku hizi ya kuwa tajiri hawezi kuingia katika ufalme wa Mungu. Ndiyo maana wakauliza “Ni nani basi awezaye kuokoka?” (Luka 18:26).
Yesu Kristo akawajibu akasema;“Yasiyowezekana kwa wanadamu yawezekana kwa Mungu” (Luka 18:26).
Kwa maneno mengine alikuwa anasema tajiri anaweza KUWEZESHWA NA MUNGU kuingia katika ufalme wa Mungu akiiamini injili inayookoa. Hata hivyo maskini naye anaokolewa kwa neema ya Mungu.
Na kwa kuamini kuwa tajiri hawezi kuurithi ufalme wa Mungu, wakristo wengi kwa kudhamiria kabisa wameamua kuwa maskini ili wasije wakaukosa ufalme wa Mungu. Lakini hii si sawa na ni kukwepa wajibu wetu tulionao kama mawakili wa mali zote za Mungu.

Na ni vizuri ufahamu ya kuwa umaskini wa kukosa chakula, mavazi na nyumba ya kukaa siyo tiketi ya kuingia katika ufalme wa Mungu. Na wala umaskini siyo utakatifu – ingawa kuna maskini walio watakatifu! Na pia utajiri siyo utakatifu ingawa kuna matajiri walio watakatifu.
Kuna Mkristo mmoja wa dhehebu fulani alikuwa akinieleza hali iliyowasonga katika dhehebu lao; alisema;
“Katika kanisa letu Mchungaji akionekana amevaa vizuri, wakristo wake wanasema amepoa kiroho. Kwao mtu wa kiroho ni mtu aliye maskini, asiyevaa nguo nzuri wala viatu vizuri.”
Niliposikia maneno hayo nilisikitika sana, na nikakumbuka maneno ya Mungu aliyosema kwa kutumia kinywa cha nabii Hosea, yasemayo, “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa ….” (Hosea 4:6) na pia Yesu Kristo aliwahi kusema ya kuwa watu wanapotea kwa kuwa hawajui maandiko wala uwezo wa Mungu.
Kwa hiyo fungua moyo wako uisikie kweli ambayo ndiyo neno la Mungu. Na utaifahamu kweli na hiyo kweli itakuweka huru (Yohana 8:32)

2
.MUNGU NA MALI
Kuna uhusiano gani kati ya Mungu na Mali? Kuna uhusiano gani kati ya Mkristo na Mali? Kuna uhusiano gani kati ya wokovu na mali?
Je, ni dhambi kwa mkristo kuwa na mali nyingi? Hebu na tuangalie maneno ya Yesu Kristo juu ya Mungu na Mali.

“Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili, Kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na Mali” (Mathayo 6:24)
Neno la kiingereza lililotafsiriwa na kuandikwa ‘mali’ ni ‘mammon’ Na neno hili ‘mommon’ ni jina la roho ya ibilisi inayotawala mali. Kwa maneno mengine naweza kusema kuwa ‘mammon’ ni jina la pepo.

Kwa hiyo, neno ‘mali’ lilivyotumika hapa linamaanisha ‘pepo linaloitwa Mali’ Ndiyo maana Yesu Kristo alisema; “Hakuna mtu awezaye kutumikia MABWANA wawili ….” Yesu Kristo asingeliita mali kuwa ni mojawapo ya MABWANA kama hakuwa anasema juu ya roho inayoitwa mali. Roho hii ya shetani iitwayo Mali imewafanya watu wengi, hata wakristo waache kumtumikia Mungu aliye hai, na badala yake waitumikie roho inayowasukuma na kuwatamanisha juu ya mali, ili waitumie kwa uchoyo na ubinafsi.

Wakristo wengine wanadhani wanaweza kumtumikia Mungu na vile vile wamtumikie Mali. Yesu Kristo alisema; “HAKUNA mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana ATAMCHUKIA HUYU, NA KUMPENDA HUYU: AMA ATASHIKAMANA NA HUYU, NA KUMDHARAU HUYU. Hamwezi kumtumikia Mungu na Mali.”
Kwa kusema hivi hakuwa anamaanisha kuwa na vitu vinavyoitwa mali ni vibaya. Kitu anachosema ni kibaya ni KUITUMIKIA MALI! Biblia inasema katika Zaburi 24:1 kuwa, “Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana; Dunia na wate wakaao ndani yake.”
Mtu hakuumbwa ili kuitumikia mali. Mtu aliumbwa kwa ajili ya utukufu wa Mungu na amtumikie Yeye peke yake. Mali ya dunia iliwekwa kwa ajili ya kumtumikia mtu, na siyo mtu kuitumikia mali! Mtu aliwekwa juu ya mali yote na aliagizwa kuitawala (Mwanzo 1:28 – 30).

Kuwa na mali siyo vibaya, wala siyo dhambi. Mali inakuwa kikwazo katika maisha ya ukristo inapoanza kumfanya mtu amsahau Mungu na mapenzi yake. Ndiyo maana Yesu Kristo alisema; “Kwa shida gani wenye mali watauingia ufalme wa Mungu” (Luka 18:24) siyo kwamba hawezi kuuingia ufalme wa Mungu, bali kwa shida wenye mali watauingia ufalme wa Mungu. Kwa maneno mengine ni kwamba wakimtanguliza na kumtumikia Mungu, mali haitakuwa kwazo katika maisha yao ya ukristo.
Sasa tuishije katika ushauri wa namna hii?

“Kwa sababu hiyo nawaambieni, msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao? NI YUPI KWENU AMBAYE AKIJISUMBUA AWEZA KUJIONGEZA KIMO CHAKE HATA MKONO MMOJA? Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti; nami nawaambia ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, JE! HATAZIDI SANA KUWAVIKA NINYI, ENYI WA IMANI HABA? Msisumbuke basi, mkisema, Tule nini? au Tunywe nini? au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote” (Mathayo 6:25 – 32)

Kuna wakristo wengine wameyaelewa vibaya maneno haya ya Bwana Yesu Kristo hata kufikia kutokufanya kazi kwa kisingizio cha kwamba Yesu Kristo alisema tusiyasumbukie maisha. Kwao kufanya kazi ina maana kusumbukia maisha. Lakini napenda kukuambia ya kuwa Yesu Kristo hakuwa ana maana ya kutuambia tusifanye kazi aliposema tusiyasumbukie maisha.
Nadhani unaamini ya kuwa ni Roho wa Kristo aliyemwongoza Mtume Paulo kuwaandikia Wathesalonike juu ya mashauri mbali mbali ya kikristo. Katika 1Wathesalonike 3:10b anasema, “Ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula.” Ni muhimu kufanya kazi. Kufanya kazi siyo kusumbuka na maisha. Kusumbuka na maisha siyo kufanya kazi.
Jambo ambalo Bwana Yesu Kristo alitaka tufahamu wakati alipokuwa akisema tusisumbukie maisha, ni kwamba katika kila jambo tumshirikishe Mungu na kumtanguliza Yeye. Wakristo wengine wanadhani wanaweza kula, kunywa na kuvaa bila msaada wa Mungu. Yesu Kristo alisema katika Yohana 15:5b kuwa; “…… maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya NENO LO LOTE” (Hili ni pamoja na kula, kunywa na kuvaa) Ndiyo maana katika Wafilipi 4:13 imeandikwa kuwa “Nayaweza mambo yote katika YEYE anitiaye nguvu” Yesu Kristo ndiye atutuaye nguvu.

Yesu Kristo alitoa mwongozo mzuri sana wa jinsi ya kuishi hapa ulimwenguni aliposema;
“Bali utafuteni KWANZA ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa”(Mathayo 6:33)
Ukiyaangalia maisha ya watu wengi waliookoka utadhani Yesu Kristo alisema, “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote MTAONDOLEWA.” Inahuzunisha kuona ya kuwa watu wengi wakiokoka maisha yao yanageuka kuwa duni, wanashindwa kula vizuri, wala kuvaa vizuri.

Ngoja nirudie kusema kuwa SI MAPENZI YA MUNGU TUWE MASKINI. SI MAPENZI YA MUNGU TUKOSE CHAKULA WALA MAVAZI. Ni Mungu yupi ambaye atawapenda ndege akawavika na kuwalisha, na akawaacha watoto wake aliowaumba kwa mfano wake wakose chakula na mavazi?

Mungu wetu tunayemwabudu na kumtumikia katika Kristo Yesu, anapenda tuishi maisha mazuri, tule, tunywe na kuvaa vizuri. Tunachotakiwa kufanya ni kuutafuta KWANZA ufalme wake, na haki yake, na hayo yote (chakula na mavazi) TUTAZIDISHIWA na siyo TUTAONDOLEWA.

Ukiona mtu anasema ameokoka na halafu anajikuta anakosa chakula na mavazi huku anafanya kazi, basi ujue anafanya kazi na kukusanya vitu hivyo pasipo Bwana; kwa kuwa asiyekusanya pamoja na Bwana hutapanya.

3
. FEDHA NA KUPENDA FEDHA
Nimewahi kumsikia mhubiri mmoja akisema; “Fedha ni shina la maovu, kwa hiyo wakristo wajihadhari nazo.” Na wakristo wengi wamekuwa wakisikika wakisema hivyo, kwa hiyo wanaogopa kuwa na fedha za kutosha.

Lakini ninaposikia watu wakisema hivi, huwa najiuliza wanaupata wapi usemi huu? Biblia haisemi;“Fedha ni shina la maovu.”
Badala yake Biblia inasema hivi;“ Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha;ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi”(1Timotheo 6:10)

Kupenda fedha ni kuwa na tamaa ya fedha; ni kuzitamani fedha. Na kupenda fedha huku ndiko shina moja la mabaya ya kila namna.
Kuwa na fedha nyingi au kidogo siyo dhambi, kwa kuwa fedha ni mali ya Mungu (Hagai 2:8) Lakini kupenda fedha nyingi au kidogo ni shina moja la maovu.
Tamaa ya fedha ndiyo inayoleta wizi, ujambazi, mauaji, dhuluma, kutokutosheka, uchoyo, wivu, uasherati; nakadhalika. Lakini unaweza kuwa na fedha bila ya kufungwa na roho ya kupenda fedha.

Je! Unafahamu ni kwa nini shetani hapendi wakristo safi wawe na fedha? Maana ni kazi ya shetani kuwapiga vita wakristo wanaotaka kujipatia fedha kwa njia ya halali. Akishindwa kuwazuia kupata fedha; atahakikisha zile fedha walizonazo wanazimaliza haraka hata kwa matumizi ambayo hawakupanga.
Je! Unafahamu ni kwa nini?

Kwa sababu anafahamu mkristo safi akiwa na fedha za kutosha, atazitumia hizo kumpiga nazo vita kwa kuihubiri injili! Na shetani anafahamu kuwa Yesu alisema mwisho hautakuja mpaka injili ihubiriwe katika mataifa yote. Kwa hiyo anajua akiweza kuwakosesha wakristo fedha za kutosha ili injili ihubiriwe, yeye anapata muda wa kupumua na kupumzika.

Wengi wameshindwa kujenga makanisa kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Watumishi wa kanisa wanalipwa mishahara kidogo, kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Mikutano ya injili na semina za neno la Mungu hazifanyiki mara kwa mara kwa kukosa fedha. Wainjilisti wanatafuta fedha za kununulia vipaza sauti wanakosa. Na matokeo yake ni kazi ya Mungu kupoa.

Je! Unadhani ni nani ambaye anaweza kutoa fedha yake ili ikahubiri injili kama siyo wakristo wenyewe? Na wakristo watatoaje fedha kama hawana fedha? Na watakuwaje na fedha, kama wanadhani kuwa na fedha nyingi ni dhambi?

Na shetani ameutumia mwanya huu kuzitumia fedha ambazo wanazo watu wasiopenda haki kueneza dhambi na uovu. Je, ni haki kwa nchi nyingine kutumia ma-billioni ya fedha kutengeza silaha ambazo baadaye wanaziharibu tena, huku mamillioni ya watu wanakufa kwa njaa na maafa mengine?

Kwa hiyo usikubali unaposikia mtu akisema kuwa na fedha ni vibaya; lakini uwe mtu wa kutokupenda fedha. Kwa kuwa ukizitamani fedha utajikuta unaanza kuzitafuta hata kwa njia ambazo ni kinyume cha maadili yetu ya Kikristo; na pia kinyume cha utu wa mwanadamu.

4
. MASKINI NA TAJIRI
Nafahamu ya kuwa si mpango wa Mungu kwa mtu aliye tajiri kumtawala maskini kwa sababu ya umaskini wake. Na pia nafahamu si mpango wa Mungu kwa nchi zilizo tajiri kuzitawala nchi maskini kwa sababu ya umaskini wake.

Lakini ni vizuri tufahamu uhusiano uliopo kati ya matabaka haya mawili:-

Biblia inasema;“Tajiri humtawala maskini, Naye akopaye ni mtumwa wake akopeshaye.”(Mithali 22:7)
Maneno haya ni kweli kabisa, na mtu ye yote ambaye ni msomaji wa historia na magazeti, anafahamu majadiliano ya muda mrefu yaliyopo kati ya nchi tajiri na nchi maskini duniani.

Ukoloni mbaya uliopo sasa hivi kati ya nchi na nchi, ni ukoloni wa kiuchumi. Katika ukoloni huu wa kiuchumi nchi tajiri zinatumia utajiri wake katika kuzikandamiza nchi maskini. Na kwa njia hii mamillioni ya watu wamo katika hali mbaya sana kimaisha.
Na njia kuu ambayo nchi hizi tajiri zinatumia kuzitawala nchi maskini ni kwa njia ya kuzipa mikopo. Na nchi maskini zote zimejikuta zimeingia katika utummwa mbaya kwa sababu ya mikopo ambayo haijajulikana kama inaweza kulipwa yote.

Inakisiwa ya kuwa jumla ya madeni yote ya nchi zinazoendelea ni mabilioni ya dola za Kimarekani na yanazidi kuongezeka.
Ni kweli kabisa kwamba utajiri huu wa nchi hizo si wote uliopatikana kwa njia ya halali. Na wafuatiliaji mambo ya uchumi duniani, wanafahamu jinsi nchi hizi zilizoendelea zinavyobuni mbinu mbalimbali kuzinyonya nchi zinazoendelea.

Ingawa si mapenzi ya Mungu tuwe maskini, lakini pia si mapenzi ya Mungu tuwe matajiri ili kuwatawala wengine kwa sababu ya umaskini wao. Ole ni kwa matajiri wanaoutumia utajiri wao kuonea na kuwafanya wenzao kuwa watumwa.
Mungu anapotupa nguvu za kupata utajiri ndani ya Kristo ni kwa kusudi muhimu la kuimarisha agano lake la kumhudumia mtu mzima – kiroho na kimwili.

Ni kweli maskini ana shida, maana hata biblia inasema maneno yake hayasikilizwi (Mhubiri 9:16). Na hii imejionyesha wazi sana katika maoni na malalamiko ya nchi maskini ambayo yanapuuzwa na kutosikilizwa na nchi tajiri.

Lakini hali hii si kwa nchi tu, bali hata katikati yetu humu humu makanisani. Sehemu nyingi kuna wakristo ambao ni matajiri, na mara kwa mara huwa wanatumia utajiri wao katika kuwatawala viongozi wa kanisa; na hata wakati mwingine kudiriki hata kutaka kubadilisha maamuzi ya vikao vya kanisa.

Na kwa upande mwingine viongozi wa sharika wanajikuta wameingiwa na hofu na kushindwa kuwakemea matajiri hao wakati wanapokwenda kinyume na maadili ya kikristo. Kama siyo ukoloni wa namna yake ulioingia katika kanisa ni nini basi?

Naamini ya kuwa wachungaji na viongozi, wengi wao wangekuwa na hali nzuri kiuchumi, baadhi ya matajiri wanaotaka kutawala viongozi wengine wangeshindwa katika mbinu zao. Au wewe unasemaje?

Shetani amekuwa akijitahidi sana kuwakandamiza wakristo wasiwe matajiri kwa kutumia njia mbali mbali kwa kutegemea mazingira yalivyo. Mahali pengine ametumia mifumo na vyombo vya fedha kama mabenki; pengine ametumia serikali, pengine ametumia mafundisho mabaya kwa wakristo, nakadhalika.

Na shabaha yake ya kufanya hivyo ni:-
Maneno ya wakristo yasisikilizwe wanapohubiri, kwa kuwa imeaandikwa;“….Walakini hekima ya maskini hudharauliwa wala maneno yake hayasikilizwi” (Mhubiri 9:19b). Kwa lugha nyingine maana yake “hayatiliwi maanani.”
Wakristo waendelee kuwa watumwa ingawa wanadai ya kuwa wamewekwa huru. Kumbuka imeandikwa hivi; “Tajiri humtawala maskini. Naye akopaye ni mtumwa wake akopeshaye” (Mithali 22;7)

Na maneno haya ni kweli kabisa. Hebu nieleze ni nani atakayesikiliza na kuyaamini maneno ya mchungaji au mwinjilisti au mtumishi yoyote wa Mungu anayesema mtegemee Yesu katika kila kitu wakati yeye mwenyewe ana nguo yenye viraka! Jambo la kwanza ambalo msikilizaji atajiuliza ni kwamba kama huyu Yesu ameshindwa kumpa mtumishi wake nguo nzuri, atawezaje kunisaidia mimi mkristo wa kawaida?

Kwa hiyo lazima tuwe waangalifu ili tunayosema yawe sawa na tunavyoishi. Na tuishi sawa sawa na ahadi za Mungu tunazozisimamia.

Siku moja nilimsikia mchungaji mmoja mwanafunzi wa chuo kimoja cha biblia akisema hivi; “Kuna mtu mmoja alikuja kutufundisha kuwa sisi kama wachungaji tusisikitike tunapoona hatuna nguo nzuri, wala chakula kizuri, wala sabuni nzuri za kuogea kwa sababu IKO SIKU MOJA VITU HIVI TUTAVITAWALA NA BWANA MBINGUNI”.

Mara moja nikamkatisha na nikasema; “ Hayo mafundisho si sawa. Unadhani Mungu aliweka hivi vitu duniani (chakula, mavazi, sabuni) kwa ajili ya shetani na watu wake?

Unadhani mbinguni tukifika tutahitaji tena chakula, mavazi na sabuni? Hivi vitu Mungu aliviweka kwa ajili yetu tuvitumie wakati huu.”

Chapisha Maoni

0 Maoni