KUSIKIA



 Mwl.Faraja Gasto

Mgawanyiko wa somo
1).Yaelewe masikio
2).Nyakati tatu katika kusikia
3).Madhara ya kutokata kusikia

Utangulizi
Mungu alipomuumba mwanadamu, Mungu alimuwekea mwanadamu milango mbalimbali na milango hiyo hujulikana kama milango mitano ya fahamu yaani Pua, Ulimi, Masikio, Ngozi na Macho.
Lakini milango hiyo hutumika pia kama milango ya kiroho, yaani vitu vya kiroho vinaweza kupita kwa kutumia masikio, Pua, Ulimi, Ngozi na Macho.
FAHAMU: Masikio ni viungo vidogo sana lakini masikio ni milango mikubwa sana ya kiroho, ngoja nikuonyeshe mfano mmoja kutoka kwenye kitabu cha (Matendo ya mitume 2:37) ukisoma andiko hilo utaona wakati Mtume Petro alipokuwa akiendelea kuhubiri, WATU WALIPOSIKIA WAKACHOMWA MIOYO YAO, maana yake ni kwamba Uweza wa Roho Mtakatifu aliyekuwa ndani ya Petro uligusa mioyo ya watu wale kwa sababu WALISIKIA.
Nikupe mfano wa pili kutoka kwenye kutoka kwenye kitabu cha (Warumi 10:17) “imani chanzo chake ni KUSIKIA na KUSIKIA huja kwa neno la Kristo”. Maana yake ni kwamba kupitia masikio huwa kuna vitu vinaingia ndani ya mtu na kumfanya aamini jambo.

Baadhi ya vitu vinavyoingia ndani ya mtu kwa njia ya masikio
Kuna vitu huwa vinaingia ndani ya mtu baada ya kusikia kitu Fulani
1).Roho Mtakatifu au roho chafu
(Yohana 6:63) Yesu aliwaambia wanafunzi wake kuwa “maneno niliyowaambia nirohotena ni uzima, maana yake ni kwamba alitaka wajue kuwa kuna roho imeingia ndani yao baada ya kusikia yale maneno aliyowaambia. Kwa hiyo roho Fulani inaweza kuingia ndani ya mtu kwa njia ya masikio.

2).Mbegu za kiroho
(Mathayo 13:19)
Yesu anasema kuwa Neno la Ufalme niMbeguambayo hupadwa ndani ya mtu, kwa hiyo kwa njia ya masikio kuna mbegu huwa zinapadwa ndani ya moyo wa mtu, hata shetani anaweza kupanda mbegu ndani ya moyo wa mtu.

(1 Wakorintho 15:33)
“mazungumzo mabaya huharibu tabia njema” maana yake ni kwamba mazungumzo ambayo si mazuri ni sawa na mbegu ambazo si nzuri, watu wanapozungumza mambo mabaya wanakuwa wanapandikiziana mbegu mbaya zitakazoharibu tabia za njema.

SEHEMU YA KWANZA
YAELEWE MASIKIO
Katika utangulizi nilikuambia masikio ni mlango wa kiroho unaopitisha vitu mbalimbali vya kiroho, katika sehemu hii ya pili tunahitaji kuona mambo machache kuhusu masikio.
(1 Wakorintho 12:14-26)
Katika andiko hilo utaona neno linasema kila kiungo katika mwili ni cha muhimu kwa kuwa vimewekwa kwa sababu mbalimbali mojawapo ni ili “vitunzane” na ikitokea kiungo kimoja kimeumia basi viungo vyote huumia nacho.
KUTUNZA- Ni kuhakikisha kitu kiko katika hali ya usalama.
Ni vema ujue kama mikono inaweza kupata shida kwa mfano kuvunjika n.k hata masikio nayo yanaweza kupata shida mbalimbali ikiwemo kutokusikia kabisa au kutokusikia vizuri.

Baadhi ya shida ambazo zinayapata masikio na matokeo ya shida hizo kwenye maisha ya watu(kumbuka nayazungumzia masikio kwa upande wa masuala ya kiroho)
1).Uzito kwenye masikio
(Isaya 6:8-10)
Masikio yanaweza kutiwa uzito na yakitiwa uzito ghafla mtu atajikuta amekuwa mzito wa kufahamu mambo mbalimbali, ukienda mashuleni utagundua kuwa kuna wanafunzi ambao huwa ni wazito wa kufahamu mambo hata kama mwalimu atatoa mifano zaidi ya mitano n.k na watu wengi hawafahamu kuwa masikio yakipata shida ya kiroho pia matokeo yatatokea katika ulimwengu wa mwili.
Uzito ukikaa kwenye masikio ghafla mtu atajikuta akianza kupuuzia(hajali) mambo mbalimbali hata kama ni ya muhimu maishani mwake.
(Waebarania 2:1-3) Biblia inauliza “tutapataje kupona TUSIPOJALI WOKOVU mkuu namana hii”
Suala la kujali jambo au kutojali jambo ni matokeo ya hali iliyopo kwenye masikio ya mtu husika.

2).Uvivu kwenye masikio
(Waebrania 5:11-14)
Tunaona watumishi wa Mungu walikuwa na mambo mengi ya kufundisha kanisa lakini hawakuyafundisha kwa kuwa watu walikuwa “wavivu wa kusikia” uvivu ulipokaa kwenye masikioghafla wakajikuta kuna vitu hawafundishwi kwa kuwa wasingeweza kuvielewa kwa kuwa uvivu ule uliookaa kwenye masikio yao uliwafanya wakawa watoto wachanga kiroho kwa hiyo walikuwa wanahitaji chakula laini na si chakula kigumu.
Uvivu ulisababisha kanisa likawa linahitaji watu kutoka nje ili kuja kuwafundisha mafundisho laini kwa kuwa miongoni mwao hakuwepo mwenye uwezo wa kuwafundisha wengine kwa kuwa wote walikuwa watoto wachanga.
Uvivu ukiaa kwenye masikio ghafla utaona mtu akisinzia kanisana au wakati wa ibada n.k kwa kuwa tabia mojawapo ya uvivu ni kumtia mtu katika usingizi mzito (Mithali 19:15) utakuta mtu amelala wakati wa ibada utadhani amekuja kwenye nyumba ya wageni (guest house).
3).Kuziba kwa masikio
(Isaya 50:5)
“Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi tena, wala sikurudi nyuma”
Ukisoma andiko hilo utaona kuwa masikio yanaweza kuziba katika namna ya kiroho, kwa hiyo ili asikie lazima masikio yazibuliwe.
Mungu alipozibua sikio la Isaya ghafla ukaidi ukaondoka moyoni mwake na pia hakutenda tena yale aliyokuwa akiyatenda hapo awali, kwa hiyo Biblia inataka tujue kuwa masikio ya mtu yakiziba atajikuta akiwa mkaidi na akifanya mambo mabaya.
Umeshawahi kujiuliza kwa nini wakati mwingine utakuta mzazi anamuadhibu mtoto huku akimwambia “mbona una masikio amgumu wewe” anachomaanisha sio masikio haya unayoyaona hapo kichwani bali ni masikio kwa namna ya kiroho lakini sina uhakika kama wazazi hao huwa wanafahamu ni nini wanachokizungumza.
HITIMISHO: Baada ya kuyaona hayo yote nina uhakika umepata ufahamu kuhusu masikio na unaweza kujiombea au kuwaombea wengine.



SEHEMU YA PILI
NYAKATI TATU KATIKA KUSIKIA
1)Kabla ya kusikia
2)Kusikiliza
3)Baada ya kusikia

KABLA YA KUSIKIA
Kwa kuwa shetani anajua kuwa imani chanzo chake ni kusikia na kusikia huja kwa neno la Kristo, shetani huwa anapambana kabla mtu hajasikia neno ili wakati wa neno utakapofika mtu asisikie vema.
(2 Wakorintho 10:4-5)
Biblia inasema kuwa shetani huwa anainua vitu ambavyo viko kinyume  na elimu ya Mungu, njia mojawapo ambayo shetani anaitumia kuharibu usikivu wa mtu kabla hajasikia neno, ni kumpandikizia mtu mawazo mabaya au kumletea mtu mtu kumbukumbu za mambo mbalimbali katika moyo wake akiwa na lengo la kumfanya asije akapokea kitu kutoka kwenye neno ambalo atakwenda kulisikia.
Na hapa ndipo utaelewa maana ya “maandalio ya moyo ni ya mwanadamu lakini jibub la ulimi linatoka kwa Bwana” (Mithali 16:1) maana yake ni kwamba wewe ndiye mwenye jukumu la kuuandaa moyo wako ili neno litakapofundishwa au kuhubiriwa uweze kulipokea na hatimaye uone matokeo ya neno kwenye maisha yako, njia mojawapo ya kuuandaa moyo wako ni pamoja na kuuombea moyo wako ili shetani asije akapandikiza mambo yatayofanya neno la Mungu lisipate nafasi kwenye moyo wako.

Kwa nini ujiombee kabla haujasikia
a)Itakusaidia usikie vema
Biblia inasema “na kwa masikio yao hawasikii vema”  (Mathayo 13:15) kusikia vema maana yake ni kusikia kama jinsi ambavyo Mungu anataka usikie, unaweza ukajikuta umesikia lakini ukawa haujasikia vema kwa hiyo unapojiombea inakusaidia usikie kama Mungu anavyotaka usikie. Kwa mfano Mungu alipomwambia Yeremia “umeona vema” maana yake ni kwamba Yeremia aliona kama jinsi ambavyo Mungu alitaka Yeremia aone, kwa hiyo kusikia vema ni kusikia kama ambavyo Mungu anakusudia usikie.

b)Itakusaidia uushinde upinzani wa shetani wakati unalisikiliza neno na hatimaye utaona maajabu yanayotoka kwenye neno la Mungu
(Matendo ya mitume 13:6-12)
Tunaona liwali aliwaita Paulo na Barnaba ili alisikie neno la Mungu lakini kumbe alikuwepo mchawi aliyetaka kumtia moyo wa kuiacha ile imani, kwa hiyo Paulo akamfundisha huyo liwali lakini liwali akawa hapokei hilo neno moyoni ndipo Roho Mtakatifu akamfunulia Paulo kinachoendelea kwenye yale mazingira, Paulo alashughulika na macho ya Yule mchawi kwa kuwa nguvu za giza zilitokea kwenye macho yake kwa hiyo macho yake yakapofushwa ghafla liwali akajikuta amefunguka na akayastaajabia mafundisho ya Bwwana.
Kwa hiyo ni vema ujue kuna mambo huwa yanainuka kinyume na neno la Mungu kwa hiyo unapojiombea kabla ya kusikia inakusaidia wewe kuzishinda hila za shetani wakati utakapolisikiliza neno la Mungu.
c)Itakusaidia upate tafsiri sahihi ya neno la Mungu
Kazi mojawapo ambayo shetani huwa anaifanya ni kubadilisha maana ya neno ili upate tafsiri ambayo yeye anataka uipate na si tafsiri ambayo Mungu anataka uipate.
(Mathayo 4:1-10)
Utaona shetani akimjia Yesu huku akiwa na maandiko lakini shetani aliyatumia maandiko ili aweze kumnasa Yesu lakini Yesu akayapangua yale maandiko shetani aliyokuja nayo, shetani alikuwa anatoa ufafanuzi ambao si sahihi ili ampate Yesu lakni kwa kuwa Yesu alijua hizo hila za shetani ilibidi Yesu atoe ufafanuzi sahihi wa neno la Mungu ili amshinde shetani.


KUSIKILIZA
Kusikiliza na kusikia ni vitu viwili tofauti, Kusikiliza ni kutega masikio yaani ni kuyaelekeza masikio yako ili usikie jambo Fulani(kusikiliza ni jambo la hiari).
Kusikia ni jambo ambalo si la hiari maadamu una masikio basi ni lazima utasikia tu haijalishi utakachosikia utakipenda au hautakipenda.
Kumbuka imani inakuja kwa kusikia na hauwezi kusikiliza kama hujasikia.
(Zaburi 81:11-14)
Mungu hupenda watu wake wamsikilize yeye peke yake, yaani wamtegee masikio yeye peke yake ili wasikie ambacho anakisema.

BAADA YA KUSIKIA
Baada ya kusikia ni vema ujifunze kufanya mambo yafuatayo
a)Tafakari (Mithali 16:20)
Kutafakari ni hatua inayohusisha kulinganisha mambo kwa lengo la kujua au kuona kitu Fulani. Kwa mfano unapotafakari neno ukilinganisha neno na maisha yako ndipo utagundua dosari iliyopo kwenye maisha yako katika eneo Fulani kwa kuwa neno litakuonyesha.
Umuhimu wa kutafakari
i)Utapata kuona au kufunuliwa mambo mbalimbali
(Hagai 1:2-7) wana wa Israeli walipopanda mbegu nyingi na wakavuna kidogo hawakukaa chini kutafakari ni kwa nini ndipo Mungu akawaambia wazitafakari njia zao kwa sababu katika kutafakari wangepata kuona dosari iko wapi.
(Mathayo 16:13-17)
Yesu alipowauliza wanafunzi wake kuwa watu wanamjua yeye kuwa ni nani, tunaona wanafunzi wake walianza kutoa majibu mbalimbali kisha akawageukia wao na kuwauliza wanamjua yeye kuwa ni nani, ukisoma andiko hilo utaona Petro alitafakari kwa muda kisha akajikuta ametoa jibu ambalo Yesu aliliita Ufunuo ambao Petro alipewa na Baba aliye mbinguni.
Kwa hiyo katika kutafakari kuna siri ya ajabu sana, jifunze kutafakari neno.
ii)Utajua linalokupasa kutenda kulingana na wakati, mazingira n.k
(Hagai 1:2-7) Biblia inasema wana wa Israeli walijikuta wamechanganya mambo kwa sababu ya kutotafakari, wakati waliotakiwa kujenga nyumba ya Bwana wao walijenga nyumba zao kwa hiyo wakachanganya nyakati na mwishowe walijikuta wakitumia nguvu nyingi huku matokeo yakiwa kidogo ndio maana Bwana aliwaambia ZITAFAKARINI NJIA ZENU.
Laiti wangekaa chini na kutafakari ndipo wangejua kinachowapasa kutenda kwa wakati ule.
(Yoshua 1:8) Mungu alimwambia Yoshua kuwa ATAFAKARI yaliyoandikwa kwenye kitabu cha torati ndipo atakapojua KUTENDA sawasawa na anavyotakiwa kutenda.
Mambo ya kuzingatia wakati wa kutafakari
i)Tenga muda wa kutafakari (Mwanzo 24:62-63)
Tunajifunza kwa Isaka kuwa alitenga muda wa kutafakari wakati wa jioni lakini Biblia haituambii alikuwa akitafakari nini ila tunaambiwa alitenga muda wa kutafakari, kwa hiyo ni vema ujifunze kuwa na muda maalumu wa kutafakari.
ii)Kaa mahali penye utulivu (Mwanzo 24:62-63)
Isaka alikwenda KONDENI ili akatafakari mambo yake, kwa hiyo tunajifunza kuwa unapotafakari ni muhimu ukae katika eneo lenye utulivu kwa sababu nafsi yako na moyo wako utakuwa hauingiliwi na vurugu zinazoweza kukutoa kwenye utulivu.
b)Amini na utendee kazi neno la Mungu
Baada ya kuwa umesikia ni muhimu ukaamini na kisha ukatendea kazi ulichosikia
(Waebrania 4:1-2) Wana wa Israeli neno halikuwafaa kwa kuwa hawakulichanganya neno la Mungu na imani zao, maana yake ni kwamba walilisikia ila hawakulitendea kazi.
(Yakobo 2:17-19) kumbuka imani isiyo na matendo imekufa, maana yake ni kwamba imani isiyo na matendo haiwezi kukusaidia chochote.
KUMBUKA: “Ukisikia bila kutendea kazi ambacho umekisikia kutoka kwenye neno la Mungu unakuwa sawa na mtu ambaye haukusikia”.


SEHEMU YA TATU
MADHARA YA KUTOTAKA KUSIKIA
1.Unakosa Baraka za Mungu
(Kumbukumbu la torati 28:15)

2.Unafungulia mlango kwa maadui kuja maishani mwako kufanya uharibifu
(Kutoka 23:20-22)


Mungu akubariki sana, naamini utatendea kazi neno hili
Ikiwa una maswali au jambo lolote usiache kuniandikia kupitia
au simu 0767955334.

Chapisha Maoni

2 Maoni