Faraja Gasto
Kama hakuna maadui
basi hakuna vita, kama kuna vita basi wapo maadui unatakiwa kukabiliana nao.
Ukweli ni kwamba kuna vita ambazo watu wanazitengeneza wenyewe bila wao
kufahamu, kuna watu wanajitengenezea maadui bila wao kufahamu. Kuna vita ambazo
huwa zinatokea kwa sababu umejitengenezea maadui kwa hiyo unatakiwa kuwa makini
sana ili usije ukajikuta unafanya kazi ya kuongeza maadui bila wewe kufahamu.
Mambo
baadhi yanayowafanya watu kujitengenezea maadui bila wao kufahamu
1.
Kukosa
maarifa juu ya mambo mbalimbali (Hosea 4:6a)(Mithali 20:5)
Mungu anasema watu
wake wanaangamizwa kwa kukosa maarifa, kwa hiyo mwanadamu ambaye hana maarifa
anakuwa anaruhusu roho ya ujinga ambayo inatoka kwenye ufalme wa giza imkalie
na kuharibu maisha yake na ya watu wanaomtegemea ndio maana utaona Mungu
anasema “kwa kuwa umeyakataa maarifa, ATAWASAHAU WATOTO WAKO” kwa hiyo
unapokataa maarifa unakuwa kwenye kazi ya kujitengenezea maadui bila wewe
kufahamu.
2.
Kutojua
namna ya kulinda moyo (Mithali 4:23)
Biblia inasema “linda
sana moyo wako KULIKO CHOCHOTE unacholinda kwa sababu kwenye moyo ndiko
kunatoka chemichemi za uzima” kwa hiyo kama moyo unatakiwa kulindwa kuliko kitu
chochote maana yake ni kwamba kila kitu kinautegemea huo moyo wako, maendeleo
au mafanikio yako yanautegemea sana moyo wako, mahusiano yako na Mungu yanaweza
kujengwa au kuvurugwa na moyo wako, moyo wako unaweza ukakufanya umsahau Mungu
au umkumbuke Mungu, moyo wako unaweza kukudanganya maana moyo una tabia ya
kumdanganya mtu ndio maana unaambiwa linda sana moyo wako kuliko yote
uyalindayo kwa sababu moyo wako ukiwa sawa ni rahisi sana kufanikiwa, ni rahisi
sana kwenda mbinguni, ni rahisi sana kumpendeza Mungu n.k.
Usipojua namna ya
kuulinda moyo wako utajikuta umejitengenezea maadui bila wewe kufahamu. Nataka nikujulishe
mambo machache kuhusu moyo wa mwanadamu.
·
Moyo unaweza KUUMIA au KUVUNJIA (Isaya 61:1)
·
Moyo unaweza kudanganya (Yeremia 17:9)
·
Moyo ndio unamfanya mtu AAMINI au
ASIAMINI (Warumi 10:10)
·
Moyo unaweza kuwa MZITO (Mathayo 13:15)
·
Moyo unaweza KULEMEWA NA MAMBO
MBALIMBALI
·
Moyo unaweza KUBEBA VITU MBALIMBALI
kama vile siri, neno n.k (Zaburi 119:11)
·
Moyo unaweza KUTEMBEA (Mathayo 6:21)
·
Moyo una MACHO (Waefeso 1:18)
Biblia inapozungumza
habari ya moyo haizungumzii moyo huo ambao uko ndani ya mwili wako upande wa
mkono wa kushoto bali Biblia inazungumzia moyo wako wa mtu wa ndani (inner man)
au UTU, kwa sababu mwanadamu ni roho, ana nafsi na ana mwili. Ukiona mtu ana
tabia mbovu au tabia za kikatili shida iko kweny UTU, shida ni huo utu wa ndani
(inner man) ndio maana Biblia inakuagiza kuulinda huo moyo wako wa mtu wa ndani
– UTU.
Njia
kadhaa za kuulinda moyo
(a). Weka neno la Mungu moyoni mwako kwa
kulisoma na kulisikiliza (Zaburi 119:11) (Wakolosai
3:19)
(b). Usiwe mwepesi
kumwambia au usipende kumwambia kila mtu mambo yako
Ninaposema usipende au usiwe mwepesi kumwambia
kila mtu mambo yako namaanisha usiwe mwepesi kumwambia kila mtu mafanikio yako,
mipango yako siri zako n.k kwa sababu kuna watu ukiwaambia mambo yako unakuwa
umemwaga siri zako kwenye uwanja wa vita, wana mioyo ina matundu haina uwezo wa
kutunza kwa hiyo ukiwaambia kitu lazima watakisema kwa watu wengine ambao
wengine wanaweza wakawa si wema kwako. Ukweli ni kwamba wapo watu wana uwezo wa
kutunza siri ila yapo mambo ambayo yanaweza yakawafanya wakavujisha siri zako
kwa mfano ukifariki kuna uwezekano mtu mwenye siri zako akazivujisha, kuvurugika
kwa mahusiano kati yako na mtu mwenye siri zako pia mtu mwenye siri zako
anaweza kuzivujisha endapo kutatokea ushawishi uliojengwa juu ya ahadi ya fedha
au nafasi n.k kwa hiyo kabla haujampa mtu siri zako jifunze kumsikiliza Mungu
itakusaidia kujua nini cha kuongea, wapi uongee, uongee na nani n.k.
(Waamuzi
16:4-21)
Delila alihakikisha
anampeleleza Samsoni ili apate kujua siri iliyoko moyoni mwake kuhusu asili ya
nguvu zake, ilifika hatua Samsoni akaitoa ile siri ya moyoni akamwambia Delila
pasipo kujua Delila yuko pale kwa kusudi maalumu (special mission), alipotoa
siri ya moyo wake mwishowe alijikuta kwenye matatizo makubwa sana hatimaye
alikufa.
(c) Jifunze kusamehe wale
waliokukosea au wanaokukosea
Mara nyingi
kutosamehe kunaua maisha ya kiroho ya watu wengi sana, pia kuosamehe kunaharibu
hata maisha ya kimwili kama vile afya ya mtu n.k, kuna watu wana magonjwa kwa
sababu ya kutosamehe wengine, Biblia inasema usiposamehe hata Mungu hawezi
kukusamehe (Mathayo 6:15)
Unaposamehe
unaufukuza uchungu uondoke moyoni mwako kwa sababu uchungu ulioko kwenye mioyo
ya watu ndio unawafanya wafanye maamuzi mabaya sana ya kiroho na kimwili.
(d). Jifunze kuyazuia
masikio yako kusikiliza mambo yaliyo tofauti na neno la Mungu
Biblia inasema “imani
huja kwa kusikia” (Warumi 10:17), imani
yoyote haijalishi ni imani sahihi au imani potofu chanzo chake ni kusikia sasa
kumbuka Biblia inasema “kwa moyo mtu huamini” (Warumi 10:10) unaposikia jambo
linakwenda moja kwa moja kwenye moyo wako likifika huko linaanza kutengeneza
imani, mitazamo, fikira n.k itategemea umesikia nini, ukisikia vibaya utavuta
roho kutoka kwenye ufalme wa giza zije zikuwezeshe kufanya mambo ambayo yako
kinyume na mapenzi ya Mungu kwa hiyo unakuwa unajitengenezea maadui bila wewe
kujua.
Wakati fulani
nikasikia watu wanajadiliana “je ni halali mkristo kusikiliza nyimbo za
kidunia” watu wengi hawafahamu kuwa silaha kubwa anayotumia shetani ni
kutengeneza sauti za aina mbalimbali kwa njia ya mafundisho na muziki ili
afanikiwe kuharibu miyo ya watu kwa hiyo ni vema uwe makini sana katika
kusikia.
3.
Kutumia
vibaya ulimi (Mithali 18:20-21)(Mithali 15:4)
Ukisoma Biblia utaona
kuna aina mbalimbali za ukorofi, aina mojawapo ya ukorofi unaotajwa na Biblia
ni “ukorofi wa ulimi” (Mithali 15:4). Kutojua
namna ya kutumia kinywa kumewafanya watu wengi kujitengenezea maadui badala ya
marafiki, wapo wanawake ambao wamewafanya waume zao kuwa maadui zao bila wao
kujua, Biblia inasema “mwanamkwe mwenye hekima hujenga nyumba yake bali
mpumbavu huwa anabomoa kwa mikono yake mwenyewe” (Mithali 14:1) wanawake wengi wameharibu nyumba zao kwa sababu ya
ukorofi wa ndimi zao mwishowe wanajikuta waume zao wamekuwa maadui zao.
Biblia inasema “uzima
na mauti huwa katika uwezo wa ulimi” (Mithali
18:20-21) kwa hiyo ukiutumia vibaya ulimi wako utajikuta umejitengenezea
mauti na matati mengine bila wewe kufahamu kwa sababu kuna nguvu katika kinywa
cha mwanadamu.
4.
Kutokuwa
na amani na watu (Waebrania 12:14)
Biblia inaposema
“tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote” maana yake ni kwamba suala la
kuwa na amani na watu wote linahitaji BIDII au JITIHADA kila inapoitwa leo.
Ukishindwa kuishi na amani na watu wote unakuwa unajitengenezea maadui bila
wewe kujua, kwa sababu watu wanapokuchukia ni rahisi sana kukusingizia, ni
rahisi sana kukushuhudia uongo, ni rahisi sana kukuangamiza hata kama wanaona
kuna shimo mbele yako hawatakuambia kwa sababu hauna amani nao.
Biblia inaposema
“tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote” maana yake ni kwamba unatakiwa
kuwa na mahusiano mazuri na watu wote, anaposema watu wote hamaanishi walio wa
imani moja na wewe, bali hata wale ambao wana imani tofauti nay a kwako ni
muhimu uwe na amani nao ndio maana Biblia inataka ufahamu kuwa suala la kuwa na
amani na watu wote linahitaji bidii au juhudi.
5.
Kuchekea
dhambi katika maisha ya mtu binafsi au kwenye familia
(Zaburi
101:7)
“
Hatakaa ndani ya nyumba yangu mtu atendaye hila. Asemaye uongo hatathibitika mbele
ya macho yangu”.
Hayo
ni maneno ya Mfalme Daudi alipogundua dhambi na kuchekea dhambi kunatengeneza
maadui alijiwekea huo utaratibu kwamba hatakubaliana na dhambi ya aina yoyote
katika malango yake.
Kuna
familia ambazo utaona watoto wakifanya dhambi za hapa na pale halafu wazazi wanaona
kukemea ni kutowapenda au kutowatendea haki watoto, sina uhakika kama wazazi
walio wengi wanafahamu kama kuchekea dhambi ni kutengeneza maadui
watakaowararua siku moja.
0 Maoni