KUHUSU MAADUI USIOWATAMBUA


 

UTANGULIZI

Kila mtu ana maadui zake anaowatambua na asiowatambua kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo jinsi wanavyotenda kazi zao.

Watu wengi wanachojua ni kwamba ADUI NI

1. Mtu au watu wanaokutendea mabaya.

2. Mtu au watu wanaokupangia mabaya kama vile Hamani alivyowapangia mabaya wayahudi (Esta 3:8-9).

3. Mtu au watu wanaokushambulia.

4. Mtu au watu wanaokuharibia mambo yako au vitu vyako.

5. Mtu au watu wanaokuwekea vikwazo ili usifike unakotakiwa kufika, usipate unachotakiwa kupata nakadhalika.

Ni kweli kabisa hicho ambacho watu wengi wanajua kuhusu adui ni nani kiko sahihi kabisa lakini Biblia imeeleza mambo mengine mengi sana kuhusu nani ni adui.

ADUI NI NANI?

1. Adui ni mtu au watu wanaokutendea mema lakini wakiwa na nia mbaya.

(2 Samweli 11:5-17) Mfalme Daudi alichukua mke wa askari mmoja aliyekuwa kwenye jeshi lake akalala naye, huyo mwanamke akabeba mimba. Mfalme akabuni njia mbalimbali za kuficha uovu wake, alimwalika ikulu yule askari akampa vyakula pia alimwalika tena aje kula na kunywa pamoja na Mfalme lakini yule askari hakujua kwamba hayo mema yote yanafanywa na adui yake, ule wema ulikuwa kifuniko tu ili asije kugundua.

Njia zote za kuficha uovu alizotumia Mfalme Daudi hazikufanikiwa hatimaye akaamua kumuua yule askari katika namna ambayo hakuna ambaye angeweza kufahamu kuwa Mfalme Daudi ndiye aliyeua.

Kwa mfano sisi wanadamu tuna njia nyingi tunazotumia kuua panya, njia mojawapo ni kuwatendea mema panya, tunaweza kuweka chakula na ndani ya chakula tukaweka sumu, panya akija ataona chakula (wema) lakini bila kujua kwenye chakula hicho (wema huo) Kuna sumu.

2. Adui ni mtu au watu wanaokupa mawazo mazuri lakini mawazo ambayo yako kinyume na mapenzi ya Mungu.

(Mathayo 16:23) Mtume Petro alimpa Yesu mawazo mazuri lakini ambayo yako kinyume na mapenzi ya Mungu, Yesu alimekemea Mtume Petro akamwambia "nenda nyuma yangu shetani u kikwazo kwangu maana hauyawazi yaliyo ya Mungu bali ya wanadamu"

3. Adui ni mtu au watu wanaomsaidia adui yako au wanaoshirikiana na adui yako.

(Waamuzi 16:4-21) Delila alikuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na Samsoni lakini alikuwa akiwapa wafilisti taarifa zote kuhusu Samsoni hatimaye Samsoni aliishia pabaya.

(Mathayo 26:14-16) Mtume Yuda Iskariote alikuwa pamoja na Yesu lakini alikuwa akishirikiana na watu waliokuwa na mipango mibaya dhidi ya Yesu.

4. Adui ni mtu au watu wanaowatumia watu wengine kukutendea mabaya ikiwemo kukungamiza.

(2 Samweli 11:14-17) Mfalme Daudi alimuua askari wake aitwaye Uria, Daudi alimuua Uria kupitia jeshi la maadui zao.

5. Adui ni mtu au watu wanaokutengenezea mazingira ya kukuangamiza, kukukwamisha, kukudhoofisha, na kukuharibia mambo mbalimbali.

(Mithali 26:27) Kuna watu huchimba mashimo ili wengine waangukie humo yaani wanatengeneza mazingira ya kuangamiza au kuharibu watu wengine.

6. Adui ni mtu au watu walio kinyume na wewe kwa ubaya (kwa nia mbaya).

Angalizo: si kila aliye kinyume na wewe ni adui, ila mtu aliye kinyume na wewe kwa ubaya au kwa nia mbaya ni adui.

(Mathayo 13:25) wewe ukipanda mbegu halafu mwingine akapanda magugu, huyo aliyepanda magugu ni adui yako.

7. Adui ni mtu au watu wanaokupa zawadi, kitu au vitu vya kukudhoofisha au kukuangamiza bila wewe kujua.

(2 Samweli 11:14-17) Mfalme Daudi aliandika waraka wa kumuua Uria halafu akampa Uria aupeleke huo waraka jeshini.

Uria hakujua amebeba mauti mikononi mwake.

MAADUI USIOWATAMBUA

Ni maadui ambao wanatenda kazi kwa kujificha, kwa kutumia watu wengine, kwa kushirikiana na watu wengine ambao ni maadui zako unaowatambua.

Amini nakuambia si kila adui yako Unamfahamu, wengine ni maadui zako lakini wanacheka na wewe, wanaweza kukupa zawadi na kukutendea mema mbalimbali.

UNAWEZAJE KUWATAMBUA MAADUI HAO

1. Mtafute Mungu. 

Mungu anawajua na anawaona maadui zako wote unaowatambua na usiowatambua, Mungu ndiye anajua mbinu wanazotumia maadui zako kukudhoofisha, kukukwamisha au kukuangamiza, ukimtafuta atakufunulia au atakujulisha, nani rafiki wa kweli nani adui yako.

Mungu atakusaidia mbinu za kukabiliana na maadui hao.

Yesu alibaini Yuda ndiye atakayemsaliti kwa kuwa alikuwa na muda mwingi wa kusemezana na Baba yake (Baba yetu aliye mbinguni).

2. Soma neno la Mungu au liweke neno la Mungu kwa wingi ndani yako litakusaidia kuwatambua maadui hao.

HITIMISHO

Huwezi kukabiliana na adui usiyemtambua, ukishatambua ni nani adui yako itakuwa rahisi kujua unakabiliana naye namna gani ndio maana ni muhimu sana kuwatambua adui zako.


Chapisha Maoni

0 Maoni