ROHO YA USALITI


 ✍Faraja Gasto

Lengo la chapisho hili ni kukufunulia baadhi ya tabia na ishara za mtu mwenye roho ya usaliti.

UTANGULIZI

Jambo mojawapo ambalo limeacha majeraha, machozi na matatizo mbalimbali kwenye maisha ya watu, familia na taasisi mbalimbali ni USALITI.

Miongoni mwa watu walioathirika na usaliti ni Mfalme Daudi, alisalitiwa na watu wengi sana ikiwemo mtoto wake aitwaye Absalomu (2 Samweli 15:1-37)

Yesu aliuawa baada ya kusalitiwa na mwanafunzi wake aitwaye Yuda Iskariote.

IKO HIVI: Kila mtu anapaswa kufahamu kuwa "usaliti ni roho" (Luka 22:3), hii roho ikimwingia mtu atasaliti tu.

BAADHI YA TABIA AU BAADHI YA ISHARA ZA MTU MWENYE ROHO YA USALITI

●Kujitenga na wenzake.

(Luka 22:4) 

Yuda Iskariote alipoingiwa na roho ya usaliti (Luka 22:) alianza kujitenga na timu yake akajiweka karibu na wapinzani wa timu yake.

●Kuwa karibu au kuwa na mahusiano na watu wasiokuamini au wasiokukubali.

(Luka 22:3-4)

Yuda Iskariote alipoingiwa na roho ya usaliti alianzisha mahusiano na wapinzani wa Yesu hatimaye akamsaliti Yesu.

●Kufanya ulichomkataza.

(Mwanzo 2:15-17)(Mwanzo 3:11)

Mungu alimkataza Adamu asile matunda fulani lakini Adamu hakutii.

●Kufanya kinyume na sheria, kanuni au utaratibu.

(2 Samweli 15:1-4)

Absalomu alikiuka utaratibu uliotumika wa kusikiliza kero, malalamiko na kesi za wananchi kwenye utawala wa baba yake.

Yeye akajipa kazi ya kuwasikiliza watu, jambo hilo lilikuwa kinyume na utaratibu, kanuni na sheria.

●Kuvujisha siri.

(Zaburi 41:9)

Mfalme Daudi alisalitiwa na mtu aliyekuwa na siri zake.

Ukiona mtu anavujisha siri zako, za taasisi nakadhalika ujue hiyo ni tabia na ishara za mtu mwenye roho ya usaliti.

HITIMISHO

Ni muhimu kupambanua roho hiyo ya usaliti ili isije kukuletea madhara.

Kupambanua roho ya usaliti kunakusaidia kuikabili kwa njia tofauti ikiwemo kuwaombea watu hao au mtu huyo mwenye roho ya usaliti, kujitenga nao, kujizuia kuwaambia siri zako nakadhalika.

NB: 

●Kama wewe ni msaliti fahamu kuwa usaliti ni dhambi na haitakuacha salama, dhambi ya usaliti haikumuacha salama Yuda Iskariote, haikumuacha salama Absalomu mwana wa Daudi (2 Samweli 18:15-18)

●Kama umesalitiwa, samehe aliye/waliokusaliti ili umpe Mungu nafasi ya kukupigania.

Chapisha Maoni

0 Maoni