WATU AMBAO UNAWAHITAJI KATIKA MAISHA YAKO NA MAMBO YA MSINGI YA KUOMBEA




(Isaya 43:4)
Ukisoma andiko hilo utaona Mungu akiwaambia wana wa Israeli kuwa ametoa Misri kuwa ukombozi kwa ajili yao na ametoa Kushi na Seba kwa ajili yao na pia atatoa watu na kabila za watu kwa ajili ya maisha yao. Kwa hiyo biblia inataka tujue kuwa katika maisha yetu ya kila siku tunahitaji watu wa aina tofauti tofauti ili tuweze kufanikiwa, katika maisha unahitaji watu watakaokupa taarifa juu ya mambo mbalimbali, unahitaji watu wa kukupa changamoto, unahitaji watu wa kukukosoa, unahitaji watu wa kukutia moyo, unahitaji watu wa kukulea (Walezi na Mchungaji), unahitaji watu wa kukufundisha, unahitaji marafiki, unahitaji watu wa kukunganisha na watu wengine au kukuunganisha ili upate kitu kutoka eneo Fulani, unahitaji watu wa kukuombea, unahitaji watu wa kukupongeza, unahitaji watu wa kukuchukulia mzigo(watu wa kukusaidia), unahitaji watu wa kukuhamasisha, unahitaji watu wa kukuongoza ili ufike mahali fulani n.k hao ni baadhi ya watu unaowahitaji katika maisha yako ili uweze kufanikisha mambo mbalimbali.
Kumbuka kila mtu ameumbwa kwa ajili ya kusudi Fulani la Mungu haijalishi mtu huyo anamcha Mungu au hamchi Mungu na ndio maana si vizur kumdharau mtu kwa sababu ziwazo zote kwa kuwa tunaishi kwa kutegemeana (Mitahli 16:4) na kwa kuwa kila jambo lina majira yake na wakati wa kila kusudi chini ya mbingu, Mungu huwa anatoa watu watakaosimama na wewe katika mazingira tofautitofauti. Kwa kuwa shetani kazi yake ni kuhakikisha mambo mema hayatokei kwenye maisha yako huwa anafanya jitihada zote ili kuhakikisha watu wanaokufaa katika kipindi Fulani hawatokei na ndio maana ni muhimu ujue mambo ya kuombea, nami nahitaji nikufundishe yale ambayo Mungu alinifundisha mimi juu ya namana ya kuomba.

1.      Ombea malango yako yawe wazi
(Isaya 60:9-11-14)
Ukisoma andiko hilo utaona biblia ikikuonesha kuwa malango yako yanapokuwa wazi kuna aina Fulani ya watu watakaokuja kwako ili kuleta utajiri wao upate kuutumia, maana yake ni kwamba malango yako yanapokuwa wazi watu hao wanajisikia vizuri kukuletea mali zao upate kuzitumia.
Kumbuka kazi ya mlango ni kuruhusu kitu kingie na kutoka kwa hiyo kama malango yamefungwa hakuna kitu chochote utakachopokea.

2.      Waombee kibali watu ambao Mungu amewatoa kwa ajili yako
(Mwanzo 39:21-23)
Ukisoma andiko hilo utaona Mungu akimpa kibali Yusufu, kutokana na kibali alichopewa akapata fursa ya kupewa wafungwa awasimamie na katika kusimamia na katika kusimamia wafungwa ndipo Yusufu alipokutana na wafungwa aliowatafsiria  ndoto zao na yakatukia kama vile alivyowatafsiria (Mwanzo 40:1-23) kupitia mmoja kati ya wale wawili aliowatafsiria ndoto Yusufu alijulikana kwa Farao.
Kibali cha Mungu kitawafanya watu ambao Mungu amewatoa kwa ajili yako hata kama wako mbali watakuja kwa ajili ya kufanikisha jambo Fulani katika maisha yako, ndio maana nakwambia wanadamu tunategemeana kila mmoja anamuhitaji mwingine ili jambo Fulani litokee kwenye maisha yake.

3.      Waombee Mungu aondoe hali ya wasiwasi na awape ujasiri
(Waamuzi 6,1,7,11-23,36-40)
Ukisoma hapo utaona wana wa Israeli walipokuwa kwenye utumwa chini ya wamidiani, wana wa Israeli walimlilia Mungu na walipomlilia Mungu, Mungu aliwapa mtu ambaye ni Gideoni ili awakomboe kutoka kwenye mikono ya wamidiani lakini Mungu aliposema na Gideoni juu ya hilo suala tunaona Gideoni anakuwa na wasiwasi kuwa yeye hataweza hiyo kazi kwa kuwa yeye ni mdogo, familia yao ni maskini n.k yaani roho ya uduni(spirit of inferiority) ikatawala fahamu zake na akawa na wasiwasi juu ya kile ambacho ameambiwa na Mungu, ilibidi Mungu atengeneze mazingira ya kumuondolea kwanza wasiwasi ili ujasir ujae ndani yake ilikusudi achukue hatua ya kuwakomboa wana wa Israeli dhidi ya utumwa.
Ni vema ujue kuwa unapomlilia Mungu huwa anasikia na anatoa watu kwa ajili yako kwa ajili ya kusudi Fulani lakini shetani anaweza kuachilia wasiwasi ndani yao ili wasichukue hatua kwa kuwa anajua wakichukua hatua lazima utatoka kweneye hali fualani ambayo si nzuri.
(Kutoka 3:1-14,4:10)
Musa na yeye alipoambiwa kwenda kuwatoa wana wa Israeli utumwani ghfla anajikuta akiwa na wasiwasi mkubwa sana mpaka anamwambia Mungu “mimi ni nani hata niende kwa Farao? Kumbuka ni wakati huohuo wana wa Israeli wanaendelea kupata mateso wakiwa utumwani na ni wakati huohuo aliyetumwa kuwatoa utumwani bado anabishana na Mungu, ilibidi kwanza Mungu atengeneze mazingira ya kumuondolea Musa wasiwasi ili ujasiri ujae ndani yake ilikusudi achukue hatua ya kwenda kuwakomboa wana wa Israeli.

4.      Waombee ulinzi, Baraka na mafanikio watu ambao Mungu amewatoa kwa ajili yako wao pamoja na familia zao
(Waamuzi 6:29-30)
Mungu alimwambia Gideoni kuwa anatakiwa aivunje madhabahu ya mungu Baali na ndipo aifanye kazi ya kuwakomboa wana wa Israeli, Gideoni alipoivunja ile madhabahu ghafla watu wa mji ule wakainuka wakasema Gideoni lazima auawe, kumbuka huyo ndiye ambaye Mungu amewapa ili awatoe kwenye utumwa wa wamidiani lakini haohao wanasema auawe, jaribu kufikiria kama Gideoni angeuawa je! nani ambaye angewatoa kwenye utumwa? Jibu rahisi ni kwamba wangeendelea kubaki watumwa kwa kuwa Gideoni angekufa wangejenga tena madhabahu ya Miungu na kutokana na hilo Mungu asingewapigania ndio maana nakwambia ni muhimu kuwaomea ulinzi watu ambao Mungu amewatoa kwa ajili yako ili wasije kudhurika ukabaki kwenye hali usiyoipenda, hivi umeshwahi kufikiria kwa nini Mungu alimng’ang’ania Gideoni ili awatoe utumwani wana wa Israeli? Kwa nini Mungu alimng’ang’ania Musa awatoe utumwani wana wa Israeli? Kwa nini Mungu alimng’ang’ania Yona aende Ninawi? Je! Mungu alikosa watu wengine wa kuwatuma mpaka ang’ang’ane na hao? Jibu rahisi ni kwamba Mungu hakukosa watu wengine wa kuwatuma lakini aliwatuma hao kwa kuwa alikuwa na kusudi Fulani na hao.
(1 Wafalme 17: 8-16)
Mungu alimwambia Eliya kuwa amemwagiza mwanamke mjane wa huko sarepta amlishe na nina uhakika Eliya alikwenda Sarepta akijua kutakuwa na chakula cha kutosha lakini alipofika Sarepta aakakutana na mwanamke anaokota kuni halafu Mungu anamwambia huyo ndiye aliyepewa kazi ya kumlisha, kumbuka mjane amebakiza kachakula kadogo ambako amepanga kujipikia yeye na mwanae wale kasha wafe kwa njaa lakini Mungu kabla hajala hicho chakula Mungu akamtumia mtu ambaye ni Eliya ili ale hicho chakula na atamke neno la kinabii juu ya vyombo anavyotunzia chakula, na tunaona kwenye biblia kuwa baada ya Eliya kula akatamka neno la kinabii chakula hakikumuishia Yule mama mpaka Mungu alipoleta mvua juu ya nchi, jaribu kufikiri kama Yule mama angekataa ombi la Eliya unahisi nini kingetokea?. 

5.      Ombea fikra za watu ambao Mungu amewatoa kwa ajili yako ili wasitazame madhaifu yao ya kimwili kwa kuwa yatawafanya wasichukue hatua
(Kutoka 4:10-15)
Mungu alipomwmbia Musa akawatoe wana wa Israeli kutoka kwenye utumwa tunaona Musa anamwambia Mungu kuwa “mimi siwezi kusema vizuri” lakini Mungu anamwambia asijali kwa kuwa yeye ndiye aliyekiumba kinywa, ninachopenda uone hapa ni kwamba shetani anaweza kukamata fikra za mtu ambaye Mungu amempa jukumu la kukutoa kwenye hali Fulani na mtu huyo akaanza kutazama udhaifu wa kimwili alionao na akashindwa kuchukua hatua na ndivyo ilivyokuwa kwa Gideoni akaanza kumwambia Mungu kuwa jamaa lao ni maskini sana n.k ndio maana nakwambia ni muhimu kuombea fikra za watu hao ili wasitazame udhaifu wao yaani wachukue hatua bila kujali udhaifu wao.

6.      Waombee watu hao utii juu ya kile ambacho Mungu anawataka wafanye kwa ajili yako
(Yona 1:1-17)
Mungu alimtuma Yona aende Ninawi ili awaambie watu kuwa baada ya siku 40 mji wa Ninawi utaangamizwa, lakini tunaona Yona alikimbilia sehemu nyingine akikwepa agizo la Mungu, nahitaji nikutafakarishe kitu, Yona aliambiwa aende Ninawi kwa kuwa baada ya siku arobaini Ninawi itaangamizwa alipokaidi agizo la Mungu, Mungu aliandaa samaki wa kummeza na alikaa ndani ya tumbo la samaki kwa muda wa siku 3 kwa hiyo 40-3 maana yake zilikuwa zimebaki siku 37, lakini Yona alipowaambia ujumbe aliotumwa tunaona watu walitubu na hatimaye Mungu alisamehe uovu wao kwa hiyo tunapata kujua kuwa kama Yona asingefika pale Ninawi, mji wa Ninawi ungeangamizwa, ndio maana nakwambia ni muhimu kuwaombea utii watu ambao Mungu amewatoa kwa ajili yako.
7.      Waombee Mungu awape uzima au afya njema watu ambao Mungu ametoa kwa ajili yako
(Kutoka 1:8-22, 2:1-10)
Shetani alipogundua kuwa wakati wa wana wa Israeli kutoka utumwani umewadia kwa kuwa mtoto ambaye atawatoa utumwani amezaliwa, shetani alijipanga na akamtumia Mfalme Farao kuja na ajenda ya kuua watoto wot ee wa kiume, lengo la shetani ilikuwa ni kumuua Musa kabla hajaanza kulitumikia kusudi la Mungu.
SWALI: Je! huwa unawaombea watoto wako na ambao sio wa kwako? Na kama huwa unaombea wa kwako tu anza kuwaombea na wengine na kama huan watoto jifunze kuombea kizazi chako na vizazi vya watu wengine.
(Mathayo 2:13-16)
Shetani alipoona Yesu amezaliwa ambaye anakwenda kuwa ukombozi kwa ulimwengu, shetani akamtumia Mfalme Herode ili kuua watoto wote wa kiume ili Yesu asije kutimiza kusudi la Mungu hapa duniani. Ndio maana nakwambia ni vema kuwaombea uzima na afya njema watu ambao Mungu amewatoa kwa ajili ya kitu kitakachogusa maisha yako.

8.      Omba Mungu awaondolee kila aina ya kikwazo kinachoweza kuwakwamisha katika kutimiza kusudi la Mungu
(2 Wafalme 4:8-16)
Utaona katika andiko hilo huyo mama alikuwa hana motto, Mungu alichofanya ni kutengeneza mazingira yatakayomfanya nabii Elisha awe anapita karibu na Yule mama, Yule mama alipokuwa akimuona nabii Elisha alihisi kwamba ni mtumishi wa Mungu na ndani yake akawa anapata msukumo wa kufanya kitu kwa ajili yake na siku moja ikabidi amshirikishe mumewe ili wafanye kitu kwa ajili ya mtumishi wa Mungu huyo, wakaafikiana kuwa wamjengee chumba, waweke na taa na meza humo ndani ili kila akipita pale awe anaingia humo ndani kupumzika, siku moja Elisha akiwa amepumzika katika kile chumba ghafla Gehazi anaambiwa amuite Yule mama na akaambiwa aombe chochote lakini Yule mama akabaki anajumuma ndipo Mungu aliweka wazo ndani ya Gehazi kwamba huyo mama apewe motto na akaambiwa kuwa mwakani atapata mtoto. Ninataka nikutafakarishe jambo kupitia kisa hiki, jaribu kufikiri kama huyu mama angekuwa na mgogoro kwenye ndoa yake je! Elisha angekaribishwa pale ndani? Na je! Elisha asingekaribishwa pale ndani unahisi wangepata mtoto?. Ndio maana nakwambia kuwa ni vema uombe Mungu awaondolee vikwazo watu ambao Mungu anawaleta maishani mwako ili kukufanikisha katika jambo Fulani, kama huyo mama angekuwa na mgogoro na mumewe ni wzi kuwa mgogoro huo ungekuwa kikwazo cha wao kupata mtoto.
Jambo la kufahamu: Mungu anapokuletea mtu au watu lazima ujifunze kuchangamkia fursa ili kile ambacho Mungu amekusudia ukipate, watu wengi Mungu anawapa watu lakini hawachangamkii fursa mwishowe wale watu wamaondoka na vitu ambavyo Mungu alikusudia waviache kwako na ndio maana maandiko yanasema ni muhimu ujifunze kuwakaribisha wageni kwa kuwa kwa kufanya hivyo wengine wamewakaribisha malaika bila wao kujua (Waebrania 13:2), kama huyo mama ((2 Wafalme 4:8-16) asingechukua hatua ya kumkaribisha Elisha ni wazi kuwa angekufa bila kuzaa japo Mungu alimletea mtu ambaye angesababisha yeye azae ila kwa kuwa alichukua hatua ndio maana mwishowe alipata mtoto.

Chapisha Maoni

0 Maoni