JIFUNZE KUPOKEA WAGENI KWA UONGOZI WA MUNGU




(Waebrania 13:2)
Kupokea wageni ni suala ambalo lipo katika mfumo wa maisha, kila mtu bila kujali umri wake, jinsia n.k huwa anapokea wageni.
Biblia inatuambia kuwa tuwafadhili wageni kwa kuwa kwa njia hiyo wengine wamewapokea malaika bila wao kujua, kwa hiyo biblia inataka tujue kuwa kupokea wageni ni suala la kiroho na ndio maana unaweza ukampokea mgeni na ghafla maisha yako yakasitwi.
Lakini katika kupokea wageni lazima uwe na tahdhari kwa kuwa hata shetani anaweza akatuma mtu na akaja kwako kama mgeni kwa hiyo pasipo kujua unaweza ujkajikuta umepokea pepo au umepokea jaribu maishani mwako ndio maana nakwambia jifunze kuwapokea wageni kwa uongozi wa Mungu. Nyumba nyingi zimevunjika kwa sababu ya mgeni au wageni, si ajabu kukuta mgeni alikuja kama mfanyakazi wa ndani (house boy/house girl) lakini baada ya muda akawa mama au baba mwenye nyumba, makanisa mengi yamevunjika kwa njia ya kupokea wageni, watoto wengi wameacha shule kwa sababu ya kupokea wageni au mgeni, watu wengi wamepoa kiroho kwa sababu ya kupokea wageni, watu wengi ndoto zao zimevurugika kwa sababu ya kupokea mgeni au wageni.
Je! tusipokee wageni? Jibu rahisi ni kwamba kupokea wageni sio vibaya ila lazima umpokee mgeni kwa kuongozwa na Mungu, yamkini ukajiuliza nitajuaje kama mgeni huyu ni sahihi kumpokea au sitakiwi kumpokea?
Yafuatayo ni mambo yatakayokufanya ujue mgeni wa kumpokea na mgeni usiyetakiwa kumpokea.
1.      Usiishie kumpokea mgeni kwa imani bali ni muhimu uangalie na amani ya Mungu(amani ya Kristo) inaamua nini moyoni mwako
(Waebrania 11:31)(Wakolosai
Yoshua alipowatuma wapelelezi kwenda kuupeleleza mjia wa Yeriko, Mungu alimwandaa Kahaba mmoja ili awapokee wageni  na kuwahifadhi (Yoshua2:1-12) lakini hakuwapokea hivihivi, bali kilichomfanya awapokee hao wageni ni “amani” aliyopata moyoni mwake juu ya hao wageni na “imani” aliyokuwa nayo juu ya wana wa Israeli (Waebrania 11:31), ukisoma (Yoshua2:1-12) utaona kilichomfanya Rahabu awe na imani juu ya wana wa Israeli ni kwa sababu alisikia matendo makuu ya Mungu wao hivyo basi hofu ya Mungu ikaingia ndani yake na hofu hiyo ikamfanya Rahabu akawa na imani na hawa watu akijua kuwa hakuna taifa linaloweza kusimama mbele yao.
Kosa ambalo watu wengi wanalolifanya katika kukaribisha wageni, ni kukaribisha wageni kwa imani bila kujali amani ya Mungu inaamua nini ndani yao na wengi wao wameishia kupata hasara, ukiendelea kusoma habari za Rahabu utaona kwa kuwa aliwapokea wageni kwa uongozi wa Mungu wa hao wageni ndio maana hakuangamizwa pamoja na watu wa Yeriko.
2.      Msikilize Roho Mtakatifu anasemaje juu ya mgeni au wageni unaotaka kuwapokea
(Matendo ya Mitume 10:17-20)
Wageni walikuja kuonana na Petro huku wakiwa na wito wa kumtaka Petro afuatane nao kwenda kwa Kornelio, walipofika pale alipokuwa Petro, Roho Mtakatifu akamwambia Petro afuatane na hao wageni kwa kuwa yeye ndiye amewatuma, ninachotaka uone hapo ni kwamba Roho Mtakatifu anaweza kukuongoza juu ya aina ya mgeni unayetakiwa kumpokea ili usije kupata hasara.
Kwa nini uwapokee wageni kwa uongozi wa Mungu?
1.      Ukimpokea mgeni unakuwa umempokea na Mungu wa mgeni huyo
(Mathayo 10:40)
Ni wakati ambapo Yesu alikuwa akiwapa maagizo Fulani wanafunzi wake juu ya utume wao na jambo mojawapo alilowaambia ndilo hili ninalotaka nikuoneshe kwenye hilo andiko hapo juu, Yesu aliwaambia kuwa “awapokeaye ninyi anipokea mimi” maana yake ni kwamba Yesu alihitaji wanafunzi wajue kuwa atakayewapokea anakuwa amemkaribisha Mungu, ndio maana ninakuambia ukimpokea mgeni unakuwa umempokea na Mungu wa mgeni.
Tafakari: Jaribu kufikiri umempokea mgeni ambaye ni ndugu yako na hamwamini M ungu wako, kama nguvu zako za kiroho zitakuwa kidogo kuliko nguvu za kiroho alizonazo huyo mgeni basi ni rahisi sana mungu wake akatawala kwenye nyumba yako na si ajabu mungu wa mgeni wako akawa na sauti kuliko Mungu wako.

(Mwanzo 39:1-6)
Yusufu alipoanza kuishi kwenye nyumba ya Potifa ghafla kuna mambo mema yalianza kutokea kwenye nyumba ya Potifa Kwa kuwa Yusufu alikuja kwenye nyumba ya Potifa akiwa na Mungu wake kwa hiyo Mungu wa Yusufu akaanza kufanikisha mambo mbalimbali kwenye nyumba ya Potifa, Potifa alipoona kuwa mambo yanakwenda vizuri akakabidhi kila kitu kwa Yusufu ispokuwa mke wake.
Kupitia hilo jambo napenda niwape changamoto waajiri(employers), waajiri wengi wamekuwa wakiajiri watu kwa vigezo mbalimbali ikiwemo elimu, uzoefu n.k si vibaya ila ni muhimu unapoajiri mtu ni vema ujifunze kupima kwanza matokeo yanayotokea katika kazi yako baada ya kuajiri je! ni matokeo chanya au hasi, na ni vema kabla haujampa mtu mkataba wa kazi umuajiri kwa mapatano kuwa atafanya kazi mwaka mmoja au miwili na ndani ya huo muda utakuwa ukipima matokeo yanayotokea baada ya kumuajiri na endapo utaona matokeo chanya basi mpe mkataba wa kazi, kuna watu wana elimu ndogo sana lakini ukiwaajiri utashangaa mambo yako yatakavyoanza kwenda vizuri(huu ni mtazamo wangu tu).
2.      Asiyewatunza watu wa nyumbani mwake huyo ameikana imani
(1 Timotheo 5:6)
Katika kipengele hiki nahitaji kuzungumzia suala la kupokea wageni katika ngazi ya familia, nimeshuhudia na kusikia familia mbalimbali anapokuja mgeni ghafla watoto wanaanza kulala kwa majirani au wakati mwingine wanalala kwenye mkeka au wanatandikiwa godoro chini ilihali kitanda anaachiwa mgeni, sio vibaya ikiwa watoto watakuwa wameridhia lakini endapo watoto wataridhia huku wakinung’unika basin i vema ujue badala ya mgeni kuwa Baraka, mgeni huyo atakuwa chanzo cha laana kwenye familia au nyumba hiyo na ndio maana ni muhimu kumpokea mgeni kwa uongozi wa Mungu kwa kuwa ukimpokea mgeni kwa uongozi wa Mungu, Mungu atakupa hekima ya kutumia ili mambo yaende vizuri hata kama nyumba ni ndogo.
Wakati mwingine utashangaa mgeni akija ndipo vyakula vizuri vinaandaliwa siku hiyo watu watakula tambi, pilau, kuku n.k lakini kama mgeni hayupo utashangaa watu hawali chakula kizuri, sasa unabaki unajiuliza ina maana mgeni ana thamani sana kuliko watoto wako au mke wako, kwa hiyo katika mazingira ya namna hiyo usitegemee Baraka kwa kuwa wanafamilia watakuwa na manung’uniko juu ya hali ya maisha ya hapo nyumbani. Wakati mwingine wengine wanakopa fedha ili wawalishe vizuri wageni lakini wageni wakiondoka utashangaa watoto wanaweza wakaambiwa hali ni ngumu kwa hiyo wale chakula chochote kitakachokuja na wakati mwingine watoto huambiwa kuwa “anayetaka vitamu akaemee”. Ni vema juhudi ambayo huwa tunakuwa nayo katika kuwaandalia wageni vitu vizuri tuwe na juhudi hizohizo na zaidi katika kuzitunza familia zetu kwa “asiyewatunza watu wa nyumbani mwake kwanza ameikana imani tena ni mbaya kuliko mchawi, mpunga pepo n.k.

3.      Ukimpokea mgeni nyumbani kwako bajeti yako inabadilika
Kuna watu wamejikuta wakiwa kwenye lindi la madeni kwa sababu ya wageni kwa kuwa unapopokea mgeni lazima uongeze na bajeti yako na ikiwa mgeni amefika kwako na ukampokea huku bajeti yako ni ndogo ghafla utajikuta kwenye madeni kama huyu mtu ambaye ametajwa kwenye (Luka 11:5-6).

Chapisha Maoni

0 Maoni