Biblia inasema wapo watu wabaya, wanaitwa wabaya kutokana na matendo yao na mawazo yao (mawazo mabaya) Mithali 28:5, Yeremia 15:21, Ezekieli 30:12, Habakuki 1:4.
Mahali pa kazi popote kuna watu wema au watu waadilifu na watu wabaya, watu wabaya ndio wale wanaopenda kupindisha mambo, watu wanaopenda kutenda kinyume na utaratibu wa kazi kwa ajili ya maslahi yao, kufanya njama za wizi wa mali, watu wasiofurahia wengine wakipandishwa vyeo au wakiongezewa mishahara, wale wanaopambana kuwatoa wengine kwenye nafasi zao za kazi ili wazichukue wao, wale wanaopambania maslahi yao binafsi badala ya maslahi ya umma au maslahi ya taasisi, wale wanaoisababishia hasara taasisi, kampuni, serikali nakadhalika
Kwenye Biblia tunaona visa vya watu wabaya mahali pa kazi alipokuwa anafanya kazi Nabii Danieli, alipokuwa anafanya kazi Mordekai nakadhalika.
VISA VYA WATU WABAYA MAHALI PA KAZI
✓MAHALI PA KAZI KWA NABII DANIELI (Danieli 6:1-25)
Nabii Danieli alikuwa afisa wa serikali ya Mfalme Dario, Mfalme Dario alichagua watu watatu akiwemo Danieli ambao walikuwa na jukumu la kuhakikisha serikali haipati hasara. Biblia inasema Danieli alifanya kazi vizuri hatimaye Mfalme Dario akakusudia kumfanya kuwa kiongozi wa ufalme wote (ni kama waziri mkuu au mkuu wa kazi za ufalme wa Dario).
Wale waliokuwa wanaoisababishia hasara serikali hawakumpenda mtu anayekwamisha mambo yao hatimaye wakakusudia kumuangamiza kabisa ili wao waendelee na ufisadi wao.
Walitengeneza mazingira ya kumsababishia kesi ambayo itamfanya Danieli afe hatimaye Danieli alijikuta amepata kesi iliyooelekea kuhukumiwa kutupwa kwenye tundu la Simba wakati ili afe kabisa waendelee na mambo yao, Danieli alikuwa kikwazo kikubwa sana wakaamua kukiondoa.
Kama si Mungu kumtetea Danieli angekufa.
✓MAHALI PA KAZI KWA MORDEKAI (Esta 3:1-11)
Mordekai alikuwa anafanya kazi kwa Mfalme Ahasuero (Esta 2:21-23), wakati fulani Mfalme Ahasuero alimwongezea cheo Hamani Kisha ikatolewa amri kwamba kila mtu atapaswa kumwinamia na kumsujudia Hamani (Esta 3:1-2).
Mordekai alikuwa kinyume na amri hiyo kwa kuwa wayahudi hawakuruhusiwa kumsujudia mwanadamu bali Mungu peke yake. Hamani alipoona Mordekai amekataa kumsujudia aliamua kutengeneza mazingira ya kuwaangamiza wayahudi wote.
Vivyo hivyo wapo watu mahali pa kazi hupenda kuheshimiwa, hupenda kuwa kama miungu watu mahali pa kazi ndivyo ilivyokuwa Kwa Hamani.
✓MAHALI PA KAZI PA MUSA (Hesabu 16:1-3)
Wakati Musa akiendelea na kazi ya kuwaongoza Wana wa Israeli kuelekea Kanaani, liliinuka kundi la watu ambao wako kinyume naye waliodai kuwa Musa anapaswa kuacha kuwaongoza waisraeli.
Vivyo hivyo mahali pa kazi wapo watu ambao huwainukia au kuwa kinyume na watu waadilifu kwa ajili ya maslahi yao binafsi.
NAMNA YA KUKABILIANA NA WATU WABAYA MAHALI PA KAZI
✓Hakikisha Mungu anakuwa upande wako (Warumi 8:31)
Jambo mojawapo lililomsaidia Mfalme Daudi kuwa salama na kuwashinda watu wabaya ni kwa sababu Mungu alikuwa upande wake (Zaburi 118:6-7).
Kama Mungu asingekuwa upande wa Danieli hakika angekufa kule kwenye tundu la Simba lakini Mungu alimuokoa kwa kuwa Mungu alikuwa upande wake.
Mungu anaweza kuwa upande wako au kuwa kinyume na wewe kutegemeana na sababu mbalimbali, mambo baadhi yanayomfanya Mungu awe upande wa mtu mahali pa kazi ni (a) haki (uwe mwenye haki - tenda haki), (b) maombi, lazima uwe mtu unayemuomba Mungu kwa kuwa maadui ni wengi kuliko marafiki (Zaburi 69:4) (c) kumtegemea Mungu.
✓Epuka kutenda makosa yanayoweza kuwapa watu wabaya nafasi au sababu ya kukusababishia matatizo.
(Danieli 6:4) Biblia inasema wafanyakazi wenzake na Danieli walitafuta sababu na kosa watakalolitumia kumshitaki Danieli lakini hawakuona kosa lake wala hawakupata sababu za kumshitaki Danieli kwa kuwa ALIKUWA MWAMINIFU.
Ili usiwape nafasi ya watu wabaya kukusababishia matatizo hakikisha unakuwa mwaminifu katika kuzingatia muda wa kazi (muda wa kuingia kazini na muda wa kutoka kazini), hakikisha unakuwa mwaminifu katika kuzingatia taratibu za kazi yako, uwe mwaminifu kuzingatia kiapo Cha kazi yako ikiwa kazi yako ina viapo nakadhalika.
✓Kuwashusha vyeo au kuwafukuza kazini.
Shetani alipotaka kuinuka kinyume cha Mungu, Mungu alimfukuza kutoka mbinguni (Ufunuo wa Yohana 12:7-9).
Jambo hilo linatufundisha mambo mengi sana ikiwemo namna ya kukabiliana na watu wabaya, kama una nafasi au mamlaka inayokuruhusu kuwafukuza watu wabaya ni heri kuwafukuza watoke mahali pa kazi wasije wakawafundisha ubaya wengine, tunaona Mungu hakumfukuza shetani peke yake bali alimfukuza pamoja na malaika waliomuunga mkono.
(Esta 3:1-2) Biblia haituambii nini kilisababisha Mfalme Ahasuero kumwongezea cheo Hamani ila Biblia inaeleza kilichotokea baada ya Hamani kuongezewa cheo, alitaka kuwaangamiza wayahudi wote kwa kuwa myahudi mwenzao alikataa kumsujudia.
Habari hiyo inafundisha mambo mengi ikiwemo suala la kumpandisha mtu fulani cheo linaweza kusababisha akaanza kujiona yeye ni mungu mtu, ndivyo ilivyo mahali pa kazi kuna wengine huwa wanajiona ni miungu watu na mwisho wao huwa ni mbaya sana.
Hivyo basi inapofika hatuna mtu akaanza kujiona ni mungu mtu kama kuna uwezekano wa kushushwa cheo ni heri kumshusha cheo au kumfukuza kabisa.
HITIMISHO
Ziko mbinu nyingi za kibiblia za kukabiliana na watu wabaya mahali pa kazi, nimefundisha mbinu tatu tu unaweza kuendelea kujifunza mbinu zingine zilizoandikwa kwenye Biblia.
Watu wabaya wapo kila eneo la kazi, wanasababisha mambo mengi mabaya kutokea mahali pa kazi au kwa wafanyakazi hivyo basi kuna haja ya kukabiliana nao.
Fahamu kuwa ukipandishwa cheo au ukiongezewa mshahara au ukipata mafanikio yoyote kazini ikiwemo kukubalika Kwa mwajiri wako, wapo watakaokuinukia ili kukutoa kwenye nafasi hiyo au kukuchonganisha na mwajiri wako ili uweze kuwakabili watu kama hao hakikisha Mungu anakuwa upande wako kama nilivyofundisha kuhusu namna ya kukabiliana na watu hao pia hakikisha hauwapi watu hao nafasi au sababu ya kukushitaki au kukutendea mabaya.
0 Maoni