JINSI YA KUSHINDA VITA VYA KIROHO AMBAVYO SHETANI ANATUMIA USINGIZI KAMA SILAHA YAKE


 Lengo la somo hili sio kukufanya usilale bali ni kukupa ufahamu au kukuongezea ufahamu kuhusu usingizi na namna shetani anavyotumia usingizi kufanya vita vya kiroho.

UTANGULIZI

Yako mambo mengi ambayo husababisha mtu kupata usingizi ikiwemo kuchoka, uzee, ujauzito, Dawa zinazosababisha mtu apate usingizi nakadhalika.

Mungu, shetani na wanadamu hutumia usingizi kufanya mambo mbalimbali kwenye maisha ya watu.

Kwa mfano Mungu alipotaka kumuumba mwanamke alimletea Adamu usingizi mzito (Mwanzo 2:21), Adamu alipokuwa amelala akatolewa ubavu mmoja Kisha ubavu ule ukatumika kutengeneza mwanamke.

Wanadamu wanapotaka kufanya aina fulani za upasuaji (operation) huwa wanahakikisha mtu analala usingizi.

Shetani naye huwaletea watu usingizi ili wasisome maandiko ya Biblia au wasisikie mahubiri ndio maana utaona kuna watu huwa wanalala wakati wa mahubiri (Matendo ya mitume 20:7-12).

Shetani hutumia usingizi ili kuhakikisha mtu au watu hawamuombi Mungu ndio maana utasikia kuna wengine wakitaka kuomba hujikuta wanaanza kusinzia (Mathayo 14:32-41).

Kuna watu wakitazama filamu au wakitazama runinga huwa hawasinzii ila wakishika Biblia ili wasome au wakitaka kumuomba Mungu wanajikuta wanaanza kusinzia, hiyo ni vita ya kiroho anayopigana shetani.

Samsoni alipokuwa amelala alinyolewa nywele zake zilizokuwa zinasababisha anakuwa na nguvu za ajabu (Waamuzi 16:18-19).

Usingizi ni silaha ya kiroho.

MAMBO BAADHI UNAYOPASWA KUFAHAMU KUHUSU USINGIZI

1. Usingizi ni roho (Isaya 29:10)(Warumi 11:8)

2. Usingizi ni kitu cha kiroho ambacho huwa kinampata mtu, Biblia inasema Mungu akamletea Adamu usingizi mzito (Mwanzo 2:21) maana yake ni kwamba usingizi ni kitu cha kitu kinatoka kwenye ulimwengu wa roho, Biblia inasema usingizi huwa unakuja na kumpata mtu (Ayubu 33:14-15) usingizi huwa unakuja kutoka kwenye ulimwengu wa roho.

3. Mlango wa usingizi ni macho (macho ni mlango wa usingizi) usingizi huwa unaingia ndani ya mtu kupitia macho yake (Zaburi 132:4)(Muhubiri 8:16) ndio maana utaona mtu akianza kusinzia macho yanaanza kuwa mazito (Marko 14:40).

4. Usingizi ni sehemu ya kifo (sio kifo ila ni sehemu ya kifo), kwa mfano tunapolala mara nyingi huwa ni kama tunakufa kwa muda. 

5. Usingizi unaweza kusababisha kifo (Zaburi 13:3), Biblia imehusianisha usingizi na kifo (Waefeso 5:14). Shetani anaweza kutuma kusababisha kifo.

NAMNA YA KUSHINDA VITA VYA KIROHO AMBAVYO SHETANI ANATUMIA USINGIZI KAMA SILAHA YAKE

1. Kemea roho ya usingizi, Biblia inasema usingizi ni roho (Isaya 29:10)(Warumi 11:8).

2. Epuka mikao inayovutia usingizi, Biblia inaeleza mikao ambayo inavuta usingizi, baadhi ya mikao hiyo (a). Kujilaza (Zaburi 3:5)(Yona 1:5) kujilaza ni kulala huku unasubiri usingizi ukupate, unapojilaza unavuta usingizi (b). Kukunja mikono (Mithali 6:10)(Mithali 24:33).

3. Hakikisha unapata muda wa kupumzika, watu wengi wana muda wa kulala ila wengi hawana muda wa kupumzika. Kupumzika ni tofauti na kulala wanaotumia lugha ya kingereza wanatumia maneno haya mawili REST yaani kupumzika na SLEEP yaani lala au kulala maana yake ni kwamba kulala na kupumzika ni mambo mawili tofauti.

Kupumzika ni kuacha kufanya kazi au shughuli fulani ili kutulia (Mwanzo 2:2-3), Mungu alitoa agizo la kupumzika kwa wana wa Israeli. 

Watu ambao hawapati muda wa kupumzika huwa wanasumbuliwa na usingizi.

4. Usiache macho yako kuingiwa na usingizi (Zaburi 132:4). Usingizi unapokuja huwa kuna dalili zinaanza kuonekana ikiwemo macho kuwa mazito (Marko 14:40) nakadhalika ili usiweze kulala unapaswa kuhakikisha unapoona dalili za usingizi nawa uso wako kwa maji, au kunywa maji, kama umekaa simama rukaruka au tembeatembea, wengine huweka miguu kwenye maji, hizo ni baadhi ya mbinu za kuhakikisha hauruhusu usingizi ukupate mpaka ufanye jambo unalotaka kufanya. Mfalme Daudi alisema alijzuia kusinzia kwa sababu kuna lengo alikusudia kulitimiza, japo Biblia haijaeleza alitumia njia gani kujizuia kusinzia ila tunaambiwa hakuruhusu usingizi umpate mpaka atakapotimiza lengo lake . Ukweli ni kwamba hauwezi kuacha kulala au unaweza kujizuia kulala kwa nyakati fulani.

5. Muombe Mungu azishike kope zako (Zaburi 77:4), Mungu akizishika kope za macho yako hauwezi kusinzia.

HITIMISHO

Zipo silaha nyingi za kiroho ambazo shetani huzitumia kufanya vita vya kiroho, silaha mojawapo ni usingizi, unapotaka kusoma neno la Mungu halafu ukajikuta unapata usingizi fahamu kuwa hiyo ni vita vya kiroho, unapotaka kumuomba Mungu halafu ukijikuta unapata usingizi fahamu kuwa hiyo ni vita vya kiroho, unapotaka kusikiliza mahubiri au mafundisho halafu ukajikuta unapata usingizi fahamu kuwa hiyo ni vita vya kiroho.

Hivyo basi ukitaka kushinda vita hivyo fuata maelekezo ya Biblia.


Chapisha Maoni

2 Maoni