UTANGULIZI
Ili uweze kuwa kiongozi bora lazima uwe na nyenzo mbalimbali za kukusaidia kuwa kiongozi bora, baadhi ya nyenzo hizo ni maarifa, hekima, ushawishi nakadhalika.
Kuna mambo ili uyafanikishe wewe kama kiongozi lazima uwe na ushawishi au ujue kushawishi watu ili wakubaliane wewe au wakubaliane na mpango wako.
Suala la kushawishi watu linahitaji maarifa, lazima uwe na maarifa au akili ya kukusaidia kushawishi watu bila kuwalazimisha kwa nguvu.
Kuna tofauti ya kulazimisha na kushawishi, kushawishi ni kumfanya mtu akubaliane na wewe kwa hiari yake mwenyewe. Kulazimisha ni kumfanya mtu akubaliane na wewe lakini sio kwa hiari yake.
KISA CHA SHEKEMU NA BABAYE NAMNA WALIVYOWASHAWISHI WAHIVI
Wahivi walikuwa wakazi wa nchi ya Kanaani hapo zamani, Shekemu aliwahi kuwa mkuu wa nchi wakati fulani.
Sikumoja alimwona Binti wa kiisraeli aitwaye Dina akalala naye akambikiri, kisha akamwambia baba yake kuna binti amempenda anataka amuoe kwa hiyo waende kwao na binti yule.
Walipofika kwao na binti wakajieleza kisha kaka zake na Dina wakawaambia hatutakubali dada yetu aolewe na watu wasiotahiriwa kwa hiyo kama Shekemu anataka kumuoa dada yetu basi yeye na watu wake watahiriwe.
Shekemu na babaye wakakubali sharti hilo kisha wakaja kwa watu wao wakawashawishi mpaka watu wakakubaliana nao, soma kisa hicho hapo chini,
"Basi, Hamori na mwanawe, Shekemu, wakaenda kwenye lango la mji, mahali pa mikutano, wakaongea na watu wao wakisema, “Watu hawa ni marafiki zetu. Tuwakaribishe waishi nchini mwetu na kufanya biashara, kwa sababu tunayo nchi ya kututosha sisi na wao pia; kisha tutaoa binti zao na kuwaoza binti zetu. Lakini wao watakubali kuishi nasi na tutakuwa jamaa moja kwa sharti hili: kwamba tutamtahiri kila mwanamume miongoni mwetu kama wao walivyotahiriwa. Je, hamwoni kwamba mifugo yao na mali yao yote itakuwa mali yetu? Haya, tukubaliane nao ili wakae pamoja nasi.” Wanaume wote waliokusanyika penye lango la mji huo wakakubaliana na Hamori na mwanawe Shekemu. Kisha, wanaume wote wakatahiriwa" Mwanzo 34:20-24 Biblia ya Habari Njema.
Walipowashawishi wale watu kwa maneno hayo hatimaye wale watu walikubali na wakatahiriwa wote.
MBINU MOJAWAPO YA KUWASHAWISHI WATU
Ni kutumia watu wenye ushawishi mahali fulani. Ukweli ni kwamba kila mahali (kila eneo na kila taasisi) kuna watu wenye ushawishi kwa wengine.
Shekemu hakwenda peke yake kuwashawishi wahivi, bali alikwenda pamoja na baba yake, babaye alikuwa miongoni mwa watu wenye ushawishi kwenye eneo hilo.
Watu wenye ushawishi ni pamoja na watu wanaokubalika mahali fulani, watu wanaoheshimika mahali fulani, watu wenye fedha na mali, wasomi, wazazi, wazee, viongozi wa kimila, viongozi wa dini nakadhalika.
HITIMISHO
Kuna mambo hautayafanikisha wewe kama kiongozi kama hauna ushawishi au kama huna maarifa kuhusu namna ya kuwashawishi watu.
Ushawishi ni nyenzo mojawapo itakayokusaidia kiongozi kufanikisha mambo mbalimbali uliyoyakusudia.
Usipojua kushawishi na usipojua namna ya kuwatumia watu wenye ushawishi hautafanikisha jambo lolote unalokusudia kulifanikisha.

0 Maoni