Mungu ameahidi watu wake mambo mengi sana, ameahidi kuhusu masuala ya afya, ulinzi, amani nakadhalika.
Kuna aina kuu mbili za ahadi za Mungu ambazo ni;-
1. Ahadi zenye masharti.
2. Ahadi ambazo hazina masharti.
AHADI ZENYE MASHARTI
Ni zile ahadi ambazo Mungu amesema "wewe ukifanya jambo fulani na yeye atafanya jambo fulani"
Ni kama mzazi unamwambia mtoto wako ukifaulu mtihani nitakununulia simu au begi jipya nakadhalika, na kwenye Biblia zimo ahadi zenye masharti.
Kwa mfano ilitolewa ahadi kwamba atakayemuua Goliathi, ataoa Binti wa Mfalme, atatajirishwa na pia familia yake haitalipa Kodi (1 Samweli 17:25). Ili ahadi hiyo itimizwe lazima umuue kwanza Goliathi.
Vivyo hivyo Mungu ameahidi mambo mengine ila ameweka masharti ili atimize ahadi hizo, kwa mfano Mungu ameahidi kwamba "tukimtumikia na tukashika maagizo yake atabariki maji yetu na chakula chetu, hakutakuwa na aliye tasa wala mwenye kuharibu mimba, atawafukiza maadui nakadhalika" (Kutoka 23:25-31). Hapo kuna masharti ili ahadi hizo zitimizwe kwako lazima utende kwanza alichosema Mungu.
Kwa mfano wanafunzi wa Yesu waliahidiwa kupewa Msaidizi ambaye ni Roho Mtakatifu ila waliambiwa wasitoke Yerusalemu mpaka ahadi hiyo itimie, ahadi ilikuwa na sharti la kuwataka wakae Yerusalemu (Matendo ya Mitume 1:4)
AHADI AMBAZO HAZINA MASHARTI
Mungu alimuahidi Ibrahimu kuwa atambariki na kumuongeza (Waebrania 6:13-15). Ahadi hiyo haikuwa na masharti yoyote.
Mungu aliahidi hayo kwa kuwa Ibrahimu alitii kumtoa mwanawe Isaka awe sadaka ya kuteketezwa, Mungu hakumwambia kwamba ukimtoa Isaka nitakubariki na kukuongeza ila aliambiwa amtoe Isaka, alipotii ndipo Mungu akatoa hiyo ahadi. Ahadi Ile haikuwa na masharti yoyote.
Mungu alimuahidi Sara kuwa atampa mtoto, hakukuwa na masharti yoyote iliyoambatana na ahadi hiyo (Waebrania 11:11), hakuambiwa ukifanya jambo fulani nitakupa mtoto ila Mungu aliahidi tu.
MAMBO YATAKAYOSABABISHA AHADI ZA MUNGU ZITIMIZWE KWAKO
1. Hakikisha unazijua ahadi za Mungu.
2.Uvumilivu (Waebrania 6:15), kuna ahadi za Mungu amepanga azitimize kwa wakati fulani kwa hiyo lazima uvumilie ili ahadi hizo zitimizwe kwako.
3. Amini kuwa aliyeahidi ni mwaminifu hawezi kusema uongo (Waebrania 11:11)
4. Hakikisha unafuata masharti ya ahadi za Mungu ikiwa ni ahadi zenye masharti, nimekufundisha kuwa kuna ahadi zingine za Mungu zina masharti, ili ahadi hizo zitimizwe kwako lazima uzingatie masharti hayo (vigezo na masharti lazima vizingatiwe).
5. Mkumbushe Mungu kwa maombi kuhusu ahadi zake.
(2 Mambo ya Nyakati 20:1-18) Mfalme Yehoshafati alimkumbusha Mungu ahadi yake kwamba aliahidi kuwapatia nchi ya maziwa na asali sasa kuna watu wamejipanga kuja kuwatoa kwenye nchi yao ambayo yeye aliwapa. Mungu alimsikia Mfalme Yehoshafati akawaambia Waisraeli wasiogope kwa kuwa hiyo vita ni ya Bwana.
Sio kwamba Mungu anasahau ndio maana anataka kukumbushwa ila kumkumbusha Mungu ni kuonyesha kuwa unajali kile ambacho aliahidi ndio maana unamuelezea.
6. Hakikisha uko mahali sahihi.
Soma mifano ifuatayo, mfano wa kwanza (Matendo 1:4) Yesu aliwaambia wanafunzi wake kuwa wakae Yerusalemu wasitoke mpaka ahadi ya Mungu itimie kwao, jambo linatujulisha kuwa kuna ahadi zingine za Mungu ili zitimie kwako lazima uwe mahali sahihi.
Mfano wa pili (Kutoka 3:8) Mungu alimwambia Musa akawatoe Waisraeli kule nchini Misri utumwani ili awapeleke nchi ya ahadi iliyojaa maziwa na asali, kwa hiyo ili Waisraeli waondokane na utumwa iliwalazimu kutoka pale Misri ili waende kwenye nchi ambayo ahadi za Mungu zingetimizwa kule.
HITIMISHO
Hayo ni mambo baadhi yatakayosababisha Mungu atimize ahadi zake kwako.

0 Maoni