MALAIKA WA MUNGU - SEHEMU YA KWANZA


 

UTANGULIZI

Katika somo hili tutajifunza mambo mengi kuhusu Malaika kwa lengo la kuelewa uhusiano wa Malaika wa Mungu na maisha yetu ili tupokee mambo mbalimbali ambayo Mungu huwapa Malaika watuletee maana Mungu hutumia watu, wanyama, ndege, vitu pia hutumia malaika kutekeleza majukumu mbalimbali hapa duniani.

Tutafahamu mambo mbalimbali kuhusu Malaika, namna wanavyotenda kazi na mambo yatakayokusaidia kupokea mambo mbalimbali kutoka Kwa Mungu kupitia malaika.

Kuna makundi makuu mawili ya Malaika

(Ufunuo wa Yohana 12:7-9)

a). Malaika waasi (pepo)

Hawa ni wale walioasi kwa kuongozwa na Ibilisi (Lucifer)

b). Malaika wa Mungu 

Hawa ni wale waliobaki chini ya Mamlaka ya Mungu Muumbaji.

MAMBO BAADHI YA MSINGI YA KUFAHAMU KUHUSU MALAIKA WA MUNGU

1. MALAIKA WALIUMBWA KABLA MTU HAJAUMBWA.

Ukisoma kitabu cha Mwanzo sura ya 1 na 2 sura hizo zinazungumzia sana uumbaji wa vilivyomo duniani lakini sura hizo hazizungumzii uumbaji mwingine uliohusisha kuumbwa kwa Malaika nakadhalika lakini Malaika waliumbwa kabla ya mtu yeyote kuwako duniani.

(Mwanzo 3:24)

Adamu na mkewe walipoasi, Mungu aliweka Malaika upande wa Mashariki wa Bustani ya Edeni, hii inatupa kufahamu kuwa Malaika waliumbwa kabla mtu hajaumbwa.

2. MALAIKA WANA MAJINA YAO.

Mbinguni Kuna Malaika wengi sana na kila Malaika ana Jina lake (Waebrania 1:4)(Waamuzi 13:17-18).

Tunaona katika Biblia Mungu amekuwa akimtumia Malaika ambaye anajulikana kwa waswahili kama Gabrieli kuwapasha watu habari mbalimbali (Luka 1:19)(Danieli 9:21)

Pia tunaona katika Biblia, katika masuala ya vita Malaika ambaye amekuwa akionekana kuongoza vita Kwa Kiswahili anaitwa Mikaeli (Ufunuo 12:7)(Danieli 10:21)

3. MALAIKA WAKO WENGI NA WAKO KATIKA MAKUNDI TOFAUTI TOFAUTI.

Kwa mfano MAKERUBI na MASERAFI sio Jina la Malaika mmoja, ni majina ya makundi ya Malaika wenye vyeo (ranks) hivyo vinavyowafanya waitwe Makerubi au Maserafi (Isaya 6:2-3,6)(Mwanzo 3:24), soma pointi namba 9 Kwa ufafanuzi Zaidi kuhusu vyeo vya Malaika.

Shetani ni Malaika aliyekuwa kwenye jamii ya Malaika wanaoitwa kwa kiswahili Makerubi au wenye cheo cha kerubi (Ezekieli 28:14-15)

Sisi wanadamu tupo wa aina nyingi na makundi tofauti kwa mfano Kuna wanadamu wazungu, wachina, waafrika, waarabu nakadhalika, hata Malaika wako wengi na wako katika makundi tofauti tofauti.

NB: Simaanishi Kuna Malaika wazungu, waafrika nakadhalika ila ni ninachotaka ufahamu Malaika wako wengi na wako wa jamii tofautitofauti kama tulivyo wanadamu.

4. MALAIKA WANA LUGHA ZAO ZA AINA MBALIMBALI.

(1 Wakorintho 13:1a)

Mtume Paulo kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu aligusia suala la Malaika, Malaika na wao wana lugha zao kama jinsi sisi wanadamu tulivyo na lugha zetu za aina mbalimbali.

NB: Japo Malaika wanaweza kuongea lugha za wanadamu lakini mwanadamu hawezi kuongea (kunena) kwa lugha za Malaika bila kuwezeshwa na Roho Mtakatifu, pia ni vema kufahamu kuwa mtu anaweza kunena Kwa lugha za wanadamu, mtu anaweza kunena Kwa lugha za Malaika, mtu anaweza kunena kwa Lugha zisizo za wanadamu wala zisizo za Malaika Kwa kuwezeshwa na Roho Mtakatifu tu.

5. MALAIKA WANAPOKEA MAAGIZO AU MAELEKEZO KUTOKA KWA MUNGU TU.

Ushuhuda

Niliwahi kusikia mwimbaji mmoja anasema "anamtuma Malaika Gabrieli na Malaika Mikaeli wakawasababishie matatizo maadui zake"

Tatizo la mwimbaji yule ni ufahamu, hili ni tatizo la watu wengi kwa kuwa hawajapata ufahamu kuhusu utendaji kazi wa Malaika.

(Mathayo 26:53)

Yesu ameweka wazi kuwa Malaika wanatenda Kazi Kwa maelekezo au maagizo ya Mungu peke yake ndio maana hata yeye wakati akiwa mwanadamu alijua kabisa hawezi kuwaagiza Malaika bali anatakiwa kuomba Kwa Mungu (Baba yake) ikiwa atataka msaada wa Mungu kupitia malaika.

(2 Wafalme 6:16-18)

Elisha alikuwa analindwa na Mungu kupitia malaika, wakati Fulani Jeshi lilimzunguka ili kumkamata lakini akamuomba Mungu awapige kwa upofu. Japo Malaika walikuwa wakimzunguka lakini hakuwaagiza Malaika washambulie lile Jeshi badala yake Elisha alimuomba Mungu awapige upofu ni kwa sababu alijua kuwa yeye hana Mamlaka ya kuwapa Malaika maagizo bali ni Mungu tu aliyemuwekea hao Malaika wamlinde.

NB: Kama wanadamu wangekuwa na Mamlaka ya kuwapa Malaika maelekezo au maagizo hakuna ambaye angekuwa masikini Kwa kuwa ungeweza kuwaagiza Malaika wazunguke duniani wakusanye Pesa zilizoangushwa na watu wakuletee. Kwa hiyo achana na habari za kuwaagiza Malaika, wewe muombe Mungu yeye atawaagiza Malaika cha kufanya.

6. MALAIKA HAWAOI WALA HAWAOLEWI.

(Marko 12:25)

Suala la kuoa na kuolewa liko hapa duniani tu, mbinguni hakuna ndoa zinazofungwa ndio maana Biblia inasema tukienda mbinguni hakutakuwa na kuoa Wala kuolewa, tutakuwa kama Malaika kwa kuwa wao hawaoi wala hawaolewi.

7. MALAIKA HAWATENDI KAZI ZAO BINAFSI BALI WANATENDA KAZI AMBAZO WANATUMWA NA MUNGU KUZIFANYA TU.

(Waebrania 1:13-14)

 8. MALAIKA WANAZIDIANA UTUKUFU, UWEZO NAKADHALIKA.

Ninaposema Malaika wanazidiana utukufu, uwezo nakadhalika namaanisha kuna Malaika ambao wana uwezo ambao Malaika wengine hawana, kuna Malaika ambao wana vitu ambavyo Malaika wengine hawana, soma (Ufunuo wa Yohana 10:1-2) (Ufunuo wa Yohana 18:1)

(Danieli 10:11-13)

Malaika aliyetumwa kumletea Danieli majibu alikutana na upinzani mkali sana muda wa siku 21 akashindwa kupita kwenye anga lile, ilibidi Mungu amtume Malaika Mikaeli mwenye uwezo Zaidi ya yule aliyetumwa kuleta majibu.

9. MBINGUNI KUNA VYEO VYA AINA MBALIMBALI HATA MALAIKA WANA VYEO TOFAUTITOFAUTI.

Kwa mfano mbinguni kuna wazee 24 hicho ni cheo, mbinguni kuna wenye uhai wanne hicho ni cheo, mbinguni kuna Mfalme wa Wafalme na Bwana wa Mabwana hicho ni cheo cha Bwana Yesu Kristo, si hivyo tu Kuna vyeo vingi sana. Kwa mfano cheo (rank) cha kuwa Mfalme wa Wafalme na Bwana wa Mabwana, Yesu alipata cheo hicho baada ya kufufuka, alipokamilisha Kazi aliyotumwa na Baba yake ndio alipata cheo hicho (Mathayo 28:18-20)(Ufunuo wa Yohana 16:13-16)(Wafilipi 2:1-10).

Malaika nao wana vyeo vyao (madaraja) ya aina mbalimbali, kumbuka Malaika Wanaongozwa katika mfumo wa kijeshi ndio maana utaona katika Biblia Mungu anajiita Bwana wa majeshi pia Yesu alisema mbinguni Kuna majeshi ya Malaika (Mathayo 27:53)

Kwa mfano mbinguni Kuna Malaika wana vyeo vinavyowafanya waitwe MASERAFI, MAKERUBI nakadhalika, kumbuka kerubi sio Jina la Malaika ni Jina la cheo (rank) alichonacho Malaika pia Serafi sio Malaika bali ni cheo (rank) alichonacho Malaika ndio maana MASERAFI ni wengi sio mmoja (Wana majina Yao) pia Makerubi ni wengi sio mmoja (Wana majina Yao).

NB: Kumbuka Malaika waasi (pepo) nao wanatofautina uwezo nakadhalika, pia pepo Wana vyeo vyao (ranks) ndio maana unaona katika Biblia neno "majeshi ya pepo wabaya" (Waefeso 6:12), kama pepo wako katika mfumo wa majeshi ni vema ufahamu majeshi Yao yanatofautiana, na vyeo vyao vinatofautiana, Mamlaka zao zinatofautiana nakadhalika ndio maana Yesu alipozungumzia habari za pepo alisema pepo akimtoka mtu Kisha akapata fursa ya kurudi, huwa anarudi akiwa na pepo wengine waovu kuliko yeye (Luka 11:24-26) maana yake ni kwamba hata pepo wanazidiana uwezo wa kutenda kazi.

10. MALAIKA WANA MAMLAKA ZA AINA TOFAUTITOFAUTI.

Yesu alisema Mamlaka yote ya mbinguni na duniani alipewa yeye alipokamilisha Kazi aliyotumwa kufanya hapa duniani (Mathayo 28:18)

Malaika nao wana Mamlaka zao tofautitofauti, Mamlaka hizo ndizo zinaweka tofauti kati ya uwezo na utukufu wa Malaika ndio maana nilikuambia Malaika wanatofautina uwezo, Utukufu nakadhalika.

Soma muonekano wa huyu Malaika (Ufunuo wa Yohana 10:1)

Soma muonekano wa huyu Malaika (Ufunuo wa Yohana 18:1)

Nimekupa mifano hiyo ili kukutazamisha namna Malaika wanavyotofautiana Mamlaka.


Chapisha Maoni

0 Maoni