MAONO NA MBEBA MAONO


 MAONO NI NINI?

1. Ni picha aliyonayo mtu moyoni mwake au ndani yake kwa ajili ya jambo fulani.

2. Ni wazo alilonalo mtu kwa ajili ya kesho yake au kesho ya wengine.

3. Ni mzigo uliomo ndani ya mtu kwa ajili ya jambo fulani.

AINA ZA MAONO

Kuna aina nyingi sana za maono baadhi ni kama vile;-

1. Maono ya kisiasa.

Yamkini mtu anatamani kugombea urais, ubunge, udiwani au nafasi fulani ya uongozi katika jamii, au mtu anataka kuanzisha programu ya kulea vipaji vya kisiasa nakadhalika.

2. Maono ya kielimu.

Yamkini mtu anataka kujiendeleza kimasomo, kujenga shule, chuo, kusaidia watu wafikie ndoto zao za kielimu nakadhalika.

3. Maono ya kiuchumi.

Yamkini mtu anataka kuanzisha biashara, anataka kukuza mtaji, kuongeza mauzo ya bidhaa, kutoa huduma fulani kwenye jamii ili kutengeneza kipato nakadhalika.

4. Maono ya kihuduma.

Yamkini mtu anataka kujenga taasisi ya dini, kuwanunulia watu vitabu vya kidini, kutafsiri vitabu vya kidini katika lugha mbalimbali, kuboresha mifumo ya sauti ndani ya jengo la kanisa, kuboresha sekta ya uimbaji na muziki nakadhalika.

5. Maono ya kijamii.

Yamkini mtu anataka kujenga hospitali, kituo cha afya, kuanzisha kituo cha kulea watoto waliotelekezwa, kusaidia makundi maalumu kama vile wajane, yatima, watu wanaoishi katika mazingira magumu nakadhalika.

VYANZO VYA MAONO

1. Kuna maono yanayotoka kwa Mungu, soma kitabu cha Maombolezo 2:9.

2. Kuna maono yanayotoka ndani ya mtu au watu, soma kitabu cha Yeremia 23:16.

Kwa mfano Mfalme Daudi alikuwa na maono ya kumjengea Mungu hekalu, hayo maono hayakutoka kwa Mungu, yalitoka ndani ya Mfalme Daudi mwenyewe (1 Mambo ya Nyakati 29:1-7)

3. Kuna maono yanayotoka kwa shetani (sitazungumzia sana maono haya kwa wakati huu), soma kitabu cha Yeremia 14:14, Maombolezo 2:14.

JINSI WATU WANAVYOPATA MAONO

Nitaeleza mambo machache japo yapo mengi, watu hupata maono kwa njia hizi zifuatazo;-

1. Kupitia mawazo.

Njia mojawapo ambayo maono huja ndani ya mtu ni njia ya mawazo, ndio maana ukianza kuwauliza watu sasa hivi kuhusu mawazo yao si ajabu kusikia mawazo ambayo yatagusa moyo wako kwa namna ya ajabu.

2. Kupitia neno la Mungu.

Kila ambaye husoma na kujifunza neno la Mungu, jambo mojawapo ambalo atalipata kutoka kwenye neno la Mungu ni maono. Kwa mfano kuna wakati nilipata maono ya kuanzisha jambo fulani wakati nasoma kitabu cha 2 Wakorintho 8:1-6).

3. Wakati wa maombi.

Wakati mwingi pindi watu wanapokuwa kwenye maombi, mtu au watu wanaweza kujikuta wamepata maono fulani.

4. Roho Mtakatifu akiachilia maono.

Biblia inasema Roho Mtakatifu naye humpa mtu au watu maono fulani kwa ajili ya makusudi mbalimbali, soma (Yoeli 2:28, Ezekiel 11:24)

5. Mbingu zinapofunuka au macho ya mtu yanapofumbuliwa (Ezekieli 1:1).

KWA NINI WATU WENGI WANAKUFA NA MAONO YAO HAYAJATEKELEZEKA

Ziko sababu nyingi zinazosababisha watu wengi kutotekeleza maono hatimaye wanakufa bila kuyatekeleza, baadhi ya sababu ni;-

1. Kutojali maono.

Unapopata maono lazima uyajali maono hayo, baadhi ya njia zinazoonyesha unajali maono uliyopata ni kuyaandika maono, kuyapa kipaumbele na uzito.à

Wakati mwingine watu huacha kujali maono kwa kuwa ni makubwa kuliko uwezo wao wa kielimu, kiuchumi nakadhalika, napenda nikuambie kuwa maono ya Daudi ya kujenga hekalu yalikuwa makubwa sana kuliko uwezo wake japo alikuwa Mfalme.

Kwa kuwa maono yalikuwa makubwa kuliko uwezo wake wa kiuchumi alichofanya alianza kuweka akiba kidogo kidogo kwa ajili ya kutimiza maono yake, kuna watu waliposikia yale maono wakamuunga mkono(1 Mambo ya Nyakati 29:2-9).

Wewe kama mbeba maono lazima ujali maono yako hata kama unaona ni makubwa kuliko uwezo wako, elimu yako, nguvu zako nakadhalika.

2. Kutomtegemea Mungu bali wanadamu.

Ukweli usiopingika ni kwamba kuna maono ili yatekelezwe lazima fedha itumike, kama mbeba maono hana fedha na amekosa watu wa kuyafadhili maono hayo anaweza kujikuta hajayatekeleza maono hayo.

Lakini ukimtegemea Mungu yeye atayafadhili maono yako maadamu yawe maono mema, Mungu atayafadhili maono aliyokupa.

Kwa mfano Nehemia alikuwa na maono ya kujenga Kuta za Yerusalemu na malango yake yaliyoharibiwa, kuna vitu alikuwa anahitaji ili kutimiza maono hayo, Nehemia alimuomba Mungu, Mungu alichofanya alimgusa Mfalme Artashasta na akampatia mahitaji yatakayomuwezesha kutimiza maono yale (Nehemia 1:11, Nehemia 2:1-8).

3. Kutojua kwamba kuna vita dhidi ya kila maono na mbeba maono au kupuuzia suala la vita dhidi ya maono na mbeba maono.

Unapokuwa na maono fulani si ajabu kukutana na vikwazo vya aina mablimbali, si ajabu kukutana na watu wa kukuvunja moyo nakadhalika.

Nehemia alikuwa na maono ya kujenga kuta za Yerusalemu na malango yake, wakati wameanza ujenzi ghafla wakainuka watu waliotaka kuikwamisha kazi ile kwa njia mbalimbali (Nehemia 4:1-23)(Nehemia 6:1-12).

4. Kuchukua hatua ili kuyaendea maono na kuyatekeleza.

Kuna maono ili yatimie lazima uzingatie taratibu za kisheria na miongozo mbalimbali, lazima ufuate taratibu hizo (Nehemia 2:7-9).

Fahamu kuwa, mara nyingi kila jambo huanza katika udogo au katika udhaufu, hakuna mti unaokua siku moja, hakuna mtu anayezaliwa akiwa mtu mzima, wote tunazaliwa tukiwa watoto wadogo, hivyo basi usiogope kuanza kuchukua hatua ndogongogo. 

Kuna wakati unaweza ukashindwa au ukavunjwa moyo au ukafanya jambo halafu watu wakapuuza au kudhihaki, usiogope - songa mbele hata mbegu haiwezi kuzaa isipokufa au isipooza kwanza, mbegu huwekwa ndani (kwa mfano mbegu zinazosababisha watoto kutungwa ndani ya tumbo huwekwa ndani) lakini baada ya muda matunda ya mbegu hizo huonekana.

Mbegu za mimea huwekwa chini ya ardhi lakini baada ya muda huzaa matunda mbalimbali, hivyo basi usiogope au usivunjwe moyo na mchakato wa kuyaendea maono yako.

5. Kutoyafadhili maono.

Kila mmoja anapaswa kufahamu kuwa anayetakiwa kufadhili maono yako ni wewe mwenyewe kwanza, wengine wanaweza kujitokeza Mungu akiwagusa ila mfadhili namba moja ni wewe mwenyewe (1 Mambo ya Nyakati 29:2-9)

Mungu anaweza kukufadhili lakini akikupa maono, hayo maono yanakuwa yako unapaswa kuyafadhili wewe. 

6. Kuahirisha mambo.

Kuna ile sauti huwa inakwambia utafanya hata kesho, utaenda hata kesho muda bado upo, watu wengi hukubaliana na sauti hiyo ya shetani, hatimaye wanajikuta hawafanyi chochote mpaka siku wanaingia duniani.


Chapisha Maoni

0 Maoni