MAMBO YATAKAYOKUSAIDIA USICHOKE KUTENDA MEMA

 
                     ✍️Faraja Gasto

Ziko aina nyingi za kuchoka, aina mojawapo ya kuchoka ni kuchoka kuwatendea watu mema. 

Watu wengi wamejikuta wamechoka kuwatendea watu mema kwa kuwa walipowatendea watu mema watu hao waliwalipa mabaya, walipowasaidia watu wakafanikiwa watu hao hawakulipa fadhila, watu hao waliwanenea mabaya nakadhalika.

Ni kweli kabisa unapotenda mema halafu ukalipwa mabaya moyo huumia mpaka inafika hatua unajuta kutenda wema, lakini Biblia inasema "Wala tusichoke kutenda mema" Wagalatia 6:9

FAHAMU MAMBO HAYA KUHUSU KUTENDA MEMA

1. Kutenda mema ni kupanda mbegu.

Wagalatia 6:9

"Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho"

Unapotenda mema unakuwa umepanda mbegu ndio maana Biblia inasema ukitenda mema ipo siku wema huo utazaa matunda.

2. Kutenda mema ni utumishi kama ulivyo utumishi mwingine.

Waefeso 2:10

"Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo"

Kila mmoja anapaswa kufahamu kuwa kutenda mema ni utumishi kama ulivyo utumishi mwingine (kuhubiri injili, kufundisha neno la Mungu, kuombea, kutoa sadaka nakadhalika) maana tuliumbwa kwa ajili ya kutenda mema wala sio mabaya, hivyo basi kutenda mema ni kumtumikia Mungu, unapochoka kutenda mema ukaacha kutenda mema maana yake ni kwamba umeacha aina hii ya utumishi.

3. Unapoacha kutenda mema unakuwa umeacha kupanda mbegu.

Wagalatia 6:9

"Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho"

BAADHI YA MAMBO YATAKAYOKUSAIDIA USICHOKE KUTENDA MEMA

1. Tenda wema kama utumishi, usitende wema kama kumfanyia mtu.

(Mathayo 6:1)

Yesu alifundisha ukitenda mema tenda kama unafanya utumishi kwa Mungu maana Mungu atakupa thawabu, usifanye ili uwafurahishe watu, usifanye kama unamfanyia mtu bali fanya kama utumishi wako Kwa Mungu.

Kwa sababu ukifanya kama unamfanyia mtu, mtu asipokushukuru utaumia moyo, asipolipa fadhila utaumia moyo, asipokumbuka wema uliomfanyia utaumia moyo. Hivyo basi tenda wema kama utumishi hata kama uliyemtendea wema asipokushukuru asipolipa fadhila hautaumia moyo maana ulifanya kama utumishi kwa Mungu.

2. Tenda wema ukiwa hauna matarajio yoyote kutoka kwa wanadamu bali Kwa Mungu.

Wagalatia 6:9

"Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho"

Ukitenda wema huku ukitarajia kupewa sifa usipopewa sifa utaumia moyo, ukitenda wema huku unatarajia kuambiwa asante usipoambiwa asante utaumia moyo, hivyo basi unapotenda mema tenda mema ukiwa hautarajii chochote kutoka kwa wanadamu bali kwa Mungu peke yake.



Chapisha Maoni

0 Maoni