Katika makala hii nitafundisha mambo yafuatayo;-
1. Baadhi ya mifano ya viongozi waliojali furaha ya watu wanaowaongoza.
2. Baadhi ya ishara zinazoonyesha mtu au watu hawana furaha.
3. Madhara ya kuongoza watu ambao hawana furaha.
MIFANO MITATU KUHUSU VIONGOZI WALIOJALI FURAHA YA WATU WAO
MFANO WA 1: (Mwanzo 40:7)
Yusufu alikuwa kiongozi katika gereza, wakati fulani aligundua kuwa baadhi ya watu anaowaongoza hawana furaha, nyuso zao zinaonyesha hawana raha hata kidogo, Yusufu alitaka kufahamu kwa nini hao watu hawana furaha, Yusufu alipowahoji aligundua kilichosababisha wakakosa furaha ni ndoto walizoota.
MFANO WA 2: (Nehemia 2:1-9)
Mfalme Artashasta alizoea kuona Nehemia akiwa mchangamfu lakini alipoona mabadiliko kwa Nehemia aligundua kuwa Nehemia hana furaha, kuna jambo linasababisha anakosa furaha akataka kujua shida ni nini, ndipo Nehemia akamweleza Mfalme jambo linalosababisha anakosa furaha.
MFANO WA 3: (Kutoka 33:11-15)
Mungu aligundua Musa amekosa furaha kabisa, Musa alipokwenda katika hema ya kukutana na Mungu alikuwa na huzuni sana, Mungu alimwambia Musa uso wangu utakwenda pamoja nawe nami nitakupa raha.
Mungu kama kiongozi wa wana wa Israeli alijua kama kiongozi aliyemweka kuwaongoza Wana wa Israeli akikosa furaha basi itakuwa vigumu sana kuwaongoza waisraeli.
BAADHI YA ISHARA ZINAZOONYESHA WATU HAWANA FURAHA
1. Mabadiliko ya hulka au uso wa mtu kukosa uchangamfu.
(Nehemia 2:2-3) Mfalme Artashasta alizoea kumuona Nehemia katika hali fulani, alipoona mabadiliko, uso wake umepoteza uchangamfu aliouzoea aligundua huyu mtu hana furaha.
2. Malalamiko.
Mara nyingi malalamiko ni zao la mambo mengi, jambo mojawapo linalosababisha kuwepo kwa malalamiko ni ukosefu wa furaha, watu ambao hawana furaha huwa na malalamiko.
(1 Wafalme 12:1-4) jamii ya Waisraeli walikuwa na malalamiko yaliyotokana na jinsi Mfalme Sulemani alivyosababisha maisha ya watu kuwa magumu katika nchi kupitia kodi nakadhalika, malalamiko hayo waliyapeleka kwa Mfalme Mpya ambaye ni mwanaye lakini naye akayapuuza malalamiko yao. Watu ambao hawana furaha hawakosi malalamiko.
BAADHI YA MADHARA YA KUONGOZA WATU AMBAO HAWANA FURAHA
1. Ufanisi na weledi wao kazini hupungua.
2. Ni rahisi sana watu hao kukusaliti au kuasi.
Malalamiko ya jamii ya wana wa Israeli yalipopuuzwa na Mfalme Rehoboamu, Waisraeli waliasi, soma (1 Wafalme 12:18-19)
"Ndipo mfalme Rehoboamu akampeleka Adoramu, aliyekuwa juu ya shokoa, nao Israeli wote wakampiga kwa mawe hata akafa. Mfalme Rehoboamu akafanya haraka kupanda katika gari, ili akimbilie Yerusalemu. HIVYO ISRAELI WAKAASI juu ya nyumba ya Daudi.
3. Watu ambao hawana furaha ni mzigo kwako kama kiongozi.
Kuongoza watu ambao hawana furaha ni mzigo pia ni hatari sana kwako kiongozi, jambo mojawapo lililosababisha kiongozi Musa kupatwa na matatizo na misukosuko mikubwa ikiwemo kutaka kuuawa hatimaye akashindwa kufika Kanaani ni kwa sababu aliongoza watu ambao hawana furaha, Waisraeli hawakuchukulia kutolewa Misri kama ukombozi wao bali walichukulia kama mwanzo mpya wa mateso ya aina zingine.
4. Watu ambao hawana furaha hawatawaliki na hawaongozeki (sio rahisi kukubali wanapoongozwa).
Kwa mfano kazi mojawapo ya Roho Mtakatifu ni kutuongoza (Warumi 8:24), lakini huyo Roho anapokuwa ndani ya mtu huzalisha kitu kinaitwa "tunda la Roho" na tunda la Roho mojawapo ni FURAHA (Wagalatia 5:22).
HITIMISHO
Haikanushiki, ni kweli huwezi kumfurahisha kila mtu lakini unapaswa kufahamu kuwa ni wajibu wako kama kiongozi kuhakikisha watu unaowaongoza wana furaha, sio tu wale wanaokupenda na kukuunga mkono bali hata wale wasiokuunga mkono.
Furaha ni nguvu ya wanaoongozwa pia ni mtaji wa kiongozi katika kuendelea kuongoza vizuri. Kama unaowaongoza hawana furaha huwezi kuwaongoza vizuri pia tarajia mabaya kwenye uongozi wako.
Kiongozi mzuri ni yule anayejali furaha ya anaowaongoza, anayelia na anaowaongoza, anayeshiriki furaha na huzuni za anaowaongoza.
NB: Kiongozi asiyejali furaha ya anaowaongoza ATARAJIE KUPATWA NA MABAYA, ATASABABISHA MABAYA KUTOKEA, KAMA NI KIONGOZI WA NCHI ATARAJIE KUMALIZA MUDA WAKE WA KUKAA MADARAKANI KWA AIBU NA FEDHEHA AU KUKATALIWA NA ANAOWAONGOZA, KUPOTEZA USHAWISHI WAKE, HESHIMA YAKE NAKADHALIKA.

0 Maoni