UTANGULIZI
Mungu alipomuumba mtu alitaka mtu aishi kwa kulitegemea neno la Mungu au sawasawa na neno la Mungu, neno la Mungu ndilo lilimfanya Adamu akaishi vizuri kwenye Bustani ya Edeni.
Shetani alipokutana na mwanamke alimuuliza "ATI HIVI NDIVYO ALIVYOSEMA BWANA MUNGU msile matunda ya miti yote ya Bustani? (Mwanzo 3:1)
Maana yake ni kwamba Kuna neno Mungu alisema lililowasaidia kuishi vizuri kwenye Bustani ya Edeni, shetani akamshawishi mwanamke akiuke (aasi) lile neno ambalo Mungu amesema kwa njia ya kula tunda, mwanamke alikula akampelekea mumewe naye akala wote wakamwasi Mungu kwa kutozingatia neno lake.
Baada ya kuasi neno la Mungu walipata madhara makubwa sana, uzao wa Adamu ulipata madhara makubwa sana kutokana na kuasi neno la Mungu walilopewa kuliishi.
Kwa hiyo neno la Mungu ni kila kitu kwenye maisha ya wanadamu, mtu akijitenga na neno la Mungu au akikiuka neno la Mungu anajitengenezea mazingira ya kuharibikiwa au kuangamia.
MAMBO UNAYOPASWA KUFAHAMU KUHUSU NENO LA MUNGU
1. Pasipo neno hakuna kilichofanyika (Yohana 1:1-2)
2. Mungu hulituma neno lake kufanya mambo mbalimbali (Zaburi 107:20)(Zaburi 147:18)(Isaya 55:11)
3. Mungu huliangalia neno lake ili alitimize (Yeremia 1:12)
4. Neno la Mungu ni taa (Zaburi 119:105)
5. Neno la MUNGU ni upanga wa kiroho au ni upanga kwa jinsi ya rohoni (Waefeso 6:17)(Waebrania 4:12-13)'
6. Neno la Mungu ni nyundo (Yeremia 23:29)
7. Neno la Mungu ni moto (Yeremia 23:29)
8. Neno la Mungu ni Mungu (Yohana 1:1)
9. Neno la Mungu huzaa imani au linabeba imani (Warumi 10:17)
NENO LA MUNGU KATIKA MALEZI
(Kumbukumbu la torati 6:6-9)
Huwezi kulea watoto vizuri bila neno la Mungu, ili ulee watoto wenye maadili lazima uwe na neno la Mungu.
Watoto wanapaswa kufundishwa neno la Mungu ili waishi sawasawa na mapenzi ya Mungu, wajue kile ambacho Mungu amesema.
NENO LA MUNGU KATIKA MAOMBI
Watu wengi hudhani wakilia sana wanapokuwa kwenye maombi basi Mungu atawasikia kutokana na kulia sana, lakini kila mtu anapaswa kufahamu kuwa Mungu analiangalia neno lake kwanza haangalii machozi yako (Yeremia 1:12)
Wana wa Israeli walimlilia Mungu kutokana na mateso waliyopata kule Misri, walipolia Mungu aliwasikia alipolikumbuka agano lake (Kutoka 2:23-25)
Wanafunzi wa Yesu walimuomba Mungu kwa kuhusianisha maombi yao na kile ambacho Mungu amesema (Matendo ya Mitume 4:23-31)yg
Kwa hiyo unapomuomba Mungu hakikisha unachoomba unakihusianisha na kile ambacho Mungu amesema kwenye neno lake.
NENO LA MUNGU KATIKA KAZI ZA MIKONO
Watu wengi hupuuza neno la Mungu katika kazi za mikono yao, lakini ni vema ufahamu kuwa kazi yoyote unayoiona duniani KUNA NENO NYUMA YA KAZI HIYO, KUNA NENO AMBALO NDILO MSINGI WA KAZI HIYO.
Mtume Petro alimwambia Yesu "kwa neno lako nitashusha nyavu" (Luka 5:1-5) yale maneno Yesu aliyosema ndiyo yaliyengeneza muujiza mkubwa kwenye kazi ya Petro.
Neno la Mungu linaleta ufunuo kwenye kazi za mikono, neno la Mungu linazaa maarifa, neno la Mungu linakupa hekima katika kazi zako nakadhalika.
NENO LA MUNGU KATIKA NDOA
Tunaishi katika nyakati ambazo ndoa nyingi zina matatizo makubwa sana yanayopelekea wanandoa kuachana, kuuana nakadhalika kwa sababu wanandoa wengi hawazingatii neno la Mungu (wamejitenga na neno la Mungu).
Neno la Mungu limeweka utaratibu mke ishije na mumewe na mume aishije na mkewe lakini wanandoa wengi hawazingatii neno la Mungu ndio maana matatizo ya ndoa yanazidi kukithiri nyakati hizi.
Kwa mfano Biblia imeweka utaratibu kuwa ukioa unapaswa kuondoka kwenu Ili ukaishi sehemu nyingine na mkeo (Mwanzo 2:24), lakini kumekuwepo watu ambao wanao halafu wanaendelea kuishi Kwa wazaxi wao matokeo yake wake zao wanajikuta wanadharauliwa na wifi zao au wanahitilafiana na mama wakwe wao.
Kwa mfano Biblia imeweka utaratibu kuwa mke anapaswa kumtii mumewe kama kumtii Bwana Yesu lakini huu ni utii ambao wanawake wengi hawana kabisa, Biblia imetueleza kuhusu mama yetu Sara na baba yetu Ibrahimu, mama yetu Sara alimtii Ibrahimu mpaka akawa anamwita Bwana (yaani mtawala au mtu mwenye hadhi anayestahili kuheshimiwa) (1 Petro 3:6)
NENO LA MUNGU KATIKA IBADA
NENO LA MUNGU (KWELI) ni msingi mmojawapo wa ibada halisi, huwezi kumuabudu Mungu kwa usahihi bila kuwa na neno la Mungu ndani yako ndio maana imeandikwa "Waabuduo halisi imewapasa kumwabudu Baba katika Roho na KWELI" (Yohana 4:24).
Neno la Mungu ndilo linakupa ufahamu kuhusu Mungu ni nani, umwabudu namna gani, nini kinatokea unapomwabudu Mungu, kwa nini umwabudu Mungu nakadhalika.
Neno la Mungu ndilo linakufanya kuwa na ufanisi katika kumuabudu Mungu.
NJAA YA NENO LA MUNGU
(Amosi 8:11)
Ni ile shauku ya ndani inayomfanya mtu kutaka kulisikia neno la Mungu. Njaa hii humfanya mtu alitafute neno la Mungu, atake kulisikia neno la Mungu.
(Matendo ya Mitume 13:6-7)
Liwali Sergio Paulo aliwaita watumishi wa Mungu nyumbani kwake wamfundishe neno la Mungu, alikuwa na shauku ndani yake ya kusikia neno la Mungu.
(Nehemia 8:1-18)
Hawa watu walienda Kwa watumishi wa Mungu ili walisikie neno la Mungu.
SIKUHIZI njaa ya neno la Mungu inapungua au kutoweka kabisa, watu wanaweza wakaomba masaa mawili lakini wakajifunza neno la Mungu dakika thelathini au chini ya dakika thelathini, watu wanaweza kuimba masaa kadhaa wakajifunza neno la Mungu kwa muda mfupi sana.
(Matendo ya Mitume 28:23)
Watu walimjia Mtume Paulo akawafundisha neno la Mungu siku nzima asubuhi hadi jioni.
HITIMISHO
Hakikisha neno la Mungu linakaa kwa wingi ndani yako kama unataka kuwa mtu mwenye hekima na busara, kama unataka kufanikisha mambo yako, kama unataka kuwa mume bora au mke bora au mlezi bora au kiongozi bora, kama unataka kutembea na Mungu, kama unataka kumjua Mungu nakadhalika.
0 Maoni