AMANI YA KRISTO NA KAZI YAKE KWA MKRISTO


 (Wakolosai 3:5)(Wafilipi 4:7)

UTANGULIZI 

Jina mojawapo la Bwana Yesu tunalloliona kwenye Biblia anaitwa "Mfalme wa amani" Isaya 9:6, siku moja aliwaambia wanafunzi wake "amani yangu nawaachieni amani yangu nawapa" Yohana 14:27.

Hiyo ndio amani ya Mungu au amani ya Kristo ambayo imetajwa kwenye hizi nyaraka (Wakolosai 3:5)(Wafilipi 4:7).

Mtu anapookoka anapewa amani ikae ndani yake kwa sababu mbalimbali ambazo nitafundisha kwenye fundisho hili.

KAZI YA AMANI YA KRISTO KWA MKRISTO

1. Kukujulisha kinachoendelea au kilichotokea kwenye ulimwengu wa roho.

(Wafilipi 4:6-7) wakati tunamuomba Mungu, Mungu anaweza kutumia amani kukujulisha kinachoendelea kwenye ulimwengu wa roho.

Soma ushuhuda wangu huu, sikumoja nilikwenda mahali fulani kwa ajili ya kumuomba Mungu kwa kuwa kuna jambo nilitaka Mungu anisaidie, wakati naendelea kuomba nilisikia amani ya Kristo ikitanda moyoni mwangu kisha nikajisikia kuacha kuomba.

Ile amani kutanda moyoni mwangu ilikuwa inanijulisha kuwa kwenye ulimwengu wa roho kuna jambo limetendeka. 

Baada ya siku kadhaa Mungu alinijibu yale mambo ambayo nilimuomba.

Vivyo hivyo ikitokea umejikuta umekosa amani na ukitafakari hakuna jambo baya ambalo limekupata au haujasikia habari mbaya lakini umejikuta umekosa amani huo ni ujumbe unaambiwa kuwa kwenye ulimwengu wa roho kuna jambo linaendelea ambalo litakusesha amani.

Kwa mfano ukisoma (Marko 14:34-42) Yesu amekosa amani, huzuni ikatanda ndani yake hiyo ilikuwa ni taarifa anapewa kuwa kwenye ulimwengu wa roho kuna jambo linaendelea, utaona Yesu alipoanza kuomba aliomba ili asife msalabani, hayo maombi hayakuwa sahihi, hilo linadhihirisha kuwa kuna jambo lilikuwa linaendelea kwenye ulimwengu wa roho Ili kuhakikisha Yesu hafi msalabani.

Yesu aliomba hivyo hakujibiwa bali aliendelea kuwa na huzuni hatimaye akaomba "si kama nitakavyo Mimi bali utakavyo wewe" malaika alikuja kumtia nguvu (Luka 22:41-42).

Ushuhuda wa mama yangu kuhusu amani ya Kristo, siku moja alijikuta amekosa amani kabisa na hakuelewa kwa haraka maana yake nini aliamua kumuomba Mungu, mdogo wangu aliporudi kutoka shuleni akamwambia mama kuwa amenusurika kugongwa na gari, yale aliyoomba mama yangu ndio yalimnusuru mdogo wangu asigongwe na gari. 

Kwa hiyo ukijikuta umekosa amani ndani yako fahamu kuwa kuna jambo linaendelea kwenye ulimwengu wa roho, hakikisha unamuomba Mungu kama Yesu alivyofanya.

2. Kuyathibitisha mapenzi ya Mungu.

Biblia inasema tusiwe wajinga bali tufahamu mapenzi ya Mungu (Waefeso 5:17), kazi ya amani ya Mungu ni kukujulisha mapenzi ya Mungu.

Ukitaka kufanya jambo lolote ambalo sio mapenzi ya Mungu, jambo mojawapo ambalo hutokea utajikuta umekosa amani ndani ya Mungu, kukosa amani ni ujumbe unajulishwa kuwa jambo unalotaka kufanya sio mapenzi ya Mungu.

Umepanga kusafiri lakini umejikuta umekosa amani, acha kusafiri au muombe Mungu akujulishe kwa nini umejikuta umekosa amani.

Kuna mtu unataka kumuoa au akuoe lakini umejikuta umekosa amani, acha kuoa au kuolewa au muombe Mungu akujulishe kwa nini umejikuta umekosa amani.

3. Ni kulinda moyo na nia yako.

(Wafilipi 4:7) Kazi mojawapo ya amani ya Kristo ni kulinda moyo wako na nia ili tuendelee kumshika Yesu Kristo.

Wanafunzi wa Yesu walipata mateso makali sana lakini pamoja na misukosuko bado waliendelea na kazi ya kushuhudia habari za Yesu, jambo mojawapo lililowasaidia kuendelea kumshika Yesu ni amani ya Kristo iliyokuwa ndani yao, waliteswa lakini bado wana amani ndani yao.

Yamkini unapitia wakati mgumu sana lakini bado amani ya Kristo imetanda moyoni mwako, kazi ya amani hiyo ni kulinda moyo wako ili misukosuko isikutoe kwa Bwana Yesu.

Mwimbaji mmoja akaimba "nionapo amani kama shwari ama nionapo shida......... Ni salama rohoni mwangu" hiyo ni amani ya Kristo ambayo inamsaidia kudumu katika Kristo Yesu japo kuna misukosuko.

4. Ni kukusaidia kuamua.

(Wakolosai 3:15) kazi mojawapo ya amani ya Kristo ni kukusaidia kuamua vizuri, kama unataka kuwa mtu unayefanya maamuzi mazuri hakikisha unazingatia amani ya Kristo inaamua nini moyoni mwako.

Kama amani ya Kristo inakugomea kufanya jambo fulani, acha kufanya.

HITIMISHO

Katika kuishi kwako hapa duniani hakikisha unazingatia amani ya Kristo inaamua nini moyoni mwako.

Amani ya Kristo ni sauti ya Mungu ndani yetu kuhusu mambo mbalimbali.

Chapisha Maoni

0 Maoni