Mungu amekuwa akiwasafirisha watu au amekuwa akiwapeleka watu kwenye kusudi lake kupitia usafiri wa aina mbalimbali.
1. Usafiri uliompeleka Yona kule Ninawi ulikuwa Nyangumi, Yona alimezwa na Nyangumi ikampeleka mpaka Ninawi kulitumikia kusudi la Mungu (Yona 1:17)(Yona 2:10)
2. Matatizo, kuna matatizo ambayo Mungu amekuwa akiyaruhusu yampate mtu ili aende kwenye kusudi la Mungu, matatizo hayo hutumika kama chombo cha usafiri cha kumpeleka mtu kwenye kusudi la Mungu.
(Mwanzo 37:18-36)(Mwanzo 39:1-23)
Yusufu alipatwa na matatizo mengi sana ikiwemo kuzushiwa kifo, kuuzwa kule Misri na kuwekwa gerezani yote hayo yalikuwa matatizo lakini Mungu aliyatumia kama vyombo vya usafiri vya kumpeleka Yusufu kwenye kusudi la Mungu.
(1 Samweli 9:3-27)(1 Samweli 10:1-27)
Kupotea kwa punda za Mzee Kishi babaye Sauli ndio kulimpeleka Sauli kupakwa mafuta na kuanza kulitumikia kusudi la Mungu.
3. Ndoa, ndoa ni chombo kikubwa cha kiroho ambacho Mungu na shetani wamekuwa wanakitumia kuwapeleka watu sehemu mbalimbali.
Mungu amekuwa akiitumia ndoa kuwapeleka watu kwenye kusudi lake, kwa mfano ndoa ya Mfalme Ahasuero na Malkia Esta ile ndoa ilimpa nguvu Malkia Esta ya kulitumikia kusudi la Mungu.
Ona Mordekai alichomwambia Esta (Esta 4:14) Kwa maana wewe ukinyamaza kabisa wakati huu, ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine; ila wewe utaangamia pamoja na mlango wote wa baba yako; walakini ni nani ajuaye kama wewe hukuujia ufalme kwa ajili ya wakati kama huo?
Maana yake ni kwamba Mordekai alikuwa anamkumbusha Esta kwamba Mungu aliruhusu aolewe kwa ajili ya kuwaokoa wayahudi dhidi ya maadui zao.
HITIMISHO
Nimeeleza mambo machache kuhusu aina za usafiri au vyombo vya usafiri ambavyo Mungu huvitumia kuwapeleka watu kwenye kusudi lake.
Hivyo basi, si kila tatizo litakalokupata uanze kumkemea shetani, mengine Mungu huyaruhusu ili kukupeleka mahali fulani kwa ajili ya kusudi lake.
Ndoa ni chombo cha usafiri, ni vema kumshirikisha Mungu suala la kuolewa kwako au kuoa kuolewa ili ndoa isikupeleke pabaya.
0 Maoni