MKRISTO ASHINDAYE


 
Mambo nitakayofundisha katika somo hili
●Mambo baadhi unayopaswa kufahamu kuhusu ushindi
●Mambo unayopaswa. kuyashinda kama Mkristo.
●Mbinu kadhaa za kukusaidia kushinda.
●Faida kadhaa za kushinda.

UTANGULIZI
Yapo mambo mengi ambayo yamewashinda watu, baadhi ya mambo hayo ni kama vile:-
▪Maisha, wengine wanasema maisha ya mjini yametushinda tunarudi kijijini.

▪Mawazo mabaya, wengine wameshindwa kabisa kuwaza mabaya wanajikuta wamekuwa waraibu wa mawazo mabaya.

▪Wengine wameshindwa kuacha madawa ya kulevya, pombe, matumizi ya sigara nakadhalika kutokana na sababu mbalimbali.

▪Wengine kusamehe kumewashinda, kila wakikumbuka waliyotendewa wanajawa uchungu na ghadhabu na wameshindwa kusamehe kabisa.

NB: Mapenzi ya Mungu ni kutuona tukiwa washindi katika mambo yote kwa kuwa Mungu ni Mungu wa washindi, anatembea na washindi, ataishi mbinguni na washindi, anatufundisha mambo mengi ili tuwe washindi, Mungu ni mshindi, kushinda ni kawaida yake, ni tabia yake.

Soma maandiko haya (Warumi 8:37)(1 Wakorintho 15:57)(2 Samweli 8:6)(2 Wafalme 5:1)(Ufunuo wa Yohana 2:7)(Ufunuo wa Yohana 2:11)(Ufunuo wa Yohana 2:17)(Ufunuo wa Yohana 2:26)(Ufunuo wa Yohana 3:5)(Ufunuo wa Yohana 3:12)(Ufunuo wa Yohana 3:21)(Ufunuo wa Yohana 21:7)

MAMBO BAADHI UNAYOPASWA KUFAHAMU KUHUSU USHINDI

1. Ushindi unaanzia rohoni na kushindwa kunaanzia rohoni, Mungu ndiye huwapa watu kushinda
(2 Samweli 8:6)(2 Wafalme 5:1)
-Ukishinda kwa jinsi ya rohoni lazima ushindi utadhihirika kwa jinsi ya mwilini.

2. Huwezi kushinda kama haumjui unayeshindana naye au unachoshindana nacho.

(Waefeso 6:13) Mtume Paulo aliwaambia Waefeso ili wajue wanachoshindana nacho kwa kuwa kama hawajui wanachoshindana nacho hawawezi kushinda.

(Mwanzo 4:6-7)
Mungu alimwambia Kaini dhambi inamuwinda kwa hiyo anatakiwa kuishinda, Mungu alitaka Kaini ajue anachoshindana nacho ili iwe rahisi kwake kushinda.

3. Kinachokuahinda nguvu kitakushinda, kama unataka kushinda lazima ukishinde nguvu unachoshindana nacho au umshinde nguvu unayeshindana naye.

(Luka 11:21-22) Yesu alizungumzia suala la nguvu na mchango wake katika ushindi wa mtu, maana yake ni kwamba anayekushinda nguvu atakushinda, kinachokushinda nguvu kitakushinda.

Nguvu ziko za aina nyingi sana kwa mfano hekima ni nguvu, mamlaka ni nguvu, mali na fedha ni nguvu, akili ni nguvu, maarifa ni nguvu nakadhalika.

4. Huwezi kushinda kama hauoni ushindi nafsini mwako au ndani yako.

(Hesabu 13:30-33) Wale wapelelezi kumi hawakuona ushindi ndani yao bali waliona kushindwa, walijiona kama mapanzi, kutokana na kuona kushindwa ndani yao waliangamia wote kule jangwani.

Lakini Yoshua na Kalebu ambao walikuwa miongoni mwa wapelelezi waliona ushindi ndani yao, Kalebu aliwaambia watu twaweza kushinda bila shaka (Hesabu 11:30).

Mtu anayeona ushindi atakiri ushindi pia atatamka ushindi hata kama mazingira yanaonyesha anaweza kushindwa.

MAMBO UNAYOPASWA KUYASHINDA KAMA MKRISTO

1.Dhambi (Mwanzo 4:6-7)
-Uwezekano wa kushinda dhambi upo ikiwa utaamini inawezekana kushinda dhambi na ikiwa utampa Mungu nafasi ya kukusaidia na kukuongoza kushinda dhambi za aina mbalimbali.
(Mwanzo 39:7-12) Biblia inasema mke wa mwajiri wake Yusufu alivyomshika Yusufu akamwambia alale naye, Yusufu alikimbia - kukimbia ilikuwa ni mbinu ya kuishinda dhambi ile.

2. Ubaya (Warumi 12:21)
Kuushinda ubaya kwa wema maana yake ni kwamba unapotendewa jambo baya usilipize kisasi wala usilipe mabaya bali lipa wema au tenda wema.

3.Ulimwengu (1 Yohana 5:4)
-Ulimwengu una mambo mengi ambayo yako kinyume na Mungu kama vile anasa, mitindo mbalimbali ya kuishi, kuvaa nakadhalika, kila mkristo anapaswa kuushinda ulimwengu na mambo yake.
(2 Timotheo 2:14) Mtume Paulo alisema "Dema alimuacha kwa kuwa aliupenda ulimwengu" kilichosababisha Dema aache kazi za Mungu alizokuwa akifanya na Mtume Paulo ni kuupenda ulimwengu huu.

4. Shetani na ufalme wake (Waefeso 6:12)
-Uwezekano wa kumshinda shetani upo kabisa, soma (Ufunuo wa Yohana 12:11)(1 Yohana 2:14).

5. Mwili (Wagalatia 5:17)
-Mwili hautaki kufanya mapenzi ya Mungu ila unapaswa kulazimishwa kuyatenda mapenzi ya Mungu, kila mtu anapaswa kuuweza mwili wake ili awe mshindi (1 Wathesalonike 4:4)

MBINU KADHAA ZA KUKUSAIDIA KUSHINDA MAMBO HAYO HAPO JUU

1. Msikilize Mungu au uwe na neno la Mungu (Mathayo 4:4)
- Yesu alimshinda shetani kwa kutumia neno, vivyo hivyo ili na sisi tuweze kuwa washindi katika mambo mbalimbali lazima tuwe na neno la Mungu.

2. Maombi 
Mfalme Nebukadneza alitoa amri wenye hekima wa Babeli wauawe kwa kuwa hawakumtafsiria ndoto aliyoota (Danieli 2:12-16) lakini Danieli kwa kuahirikiana na wenzake walimuomba Mungu (Danieli 2:17-19)  kupitia maombi yale Mungu alimfunulia Danieli ndoto ile na tafsiri yake.

Maombi ya wakina Danieli yaliwaepusha  wenye hekima wa Babeli wasiuawe.

Maombi yanaweza kuwasaidia watu kuwa washindi dhidi ya mambo mbalimbali kama vile mauti, hofu nakadhalika.

3. Roho Mtakatifu (Zekaria 4:6)
-Mungu alimwambia Zerubabeli kuwa upinzani unaomkabili hawezi kuushinda kwa nguvu bali kwa Roho Mtakatifu.

Hivyo basi ili tuwe washindi katika mambo mbalimbali lazima tumpe Roho Mtakatifu nafasi ya kutuongoza na kutusaidia ili tuwe washindi.
Kuna wakati mtu anaweza kutumia akili na nguvu zake lakini akajikuta ameshindwa, ni muhimu sana kumpa nafasi Roho Mtakatifu akuongoze ili uwe kushinda.

(Matendo ya mitume 6:9-10) Watu walishindana kwa hoja na Stefano lakini aliwashinda kwa sababu Stefano alikuwa na Roho Mtakatifu aliyemsaidia kuwakabili kwa hoja wale waliokuwa wakijadiliana naye.

FAIDA KADHAA ZA KUSHINDA
1. Ushindi unaleta raha na zawadi au tuzo (taji).
-Hakuna anayepewa tuzo,taji au zawadi bila kushinda. 

2. Ushindi unaleta heshima.
Kwa mfano tunapochagua viongozi kwenye chaguzi mbalimbali, wale wanaoshinda kwenye uchaguzi huwa tunaanza kuwaita WAHESHIMIWA kwa kuwa ushindi unaleta heshima.

Chapisha Maoni

0 Maoni