KUKUA KIROHO

KUKUA KIROHO

Sifa mojawapo ya kibaiologia ya kiumbe hai ni KUKUA (GROWTH), hivyo basi kiumbe hai kinapaswa kukua.

Kiumbe hai kisipokua basi kitakuwa na matatizo yanayosababisha kisikue.

(2 Wakorintho 5:17) Kila aliyemwamini Yesu ni kiumbe kipya ni kiumbe hai kwa kuwa amezaliwa uoya kwa jinsi ya rohoni (1 Petro 2:2) hivyo basi  anapaswa kukua kiroho.

NB: Kama jinsi ambavyo mzazi hafurahii kuona mtoto aliyemzaa amedumaa, vivyo hivyo Mungu hafurahii kuona mtoto aliyemzaa amedumaa.

KUKUA KIROHO NI NINI?
1. Ni kuongezeka kwa vitu vya rohoni ndani ya mtu (ufahamu wa rohoni, mafunuo n.k)

2. Ni mabadiliko chanya katika utu wa ndani (kiroho) ambayo yanaathiri au yanaonekana katika utu wa nje (kimwili).

Mabadiliko hayo ni pamoja na;-
▪Kuongezeka nguvu rohoni
▪Kuongezeka hekima
▪Kuongezeka kwa uwezo wa kupambanua mema na mabaya
▪Kuongezeka imani
▪Kuongezeka neema
▪Kuongezeka ufahamu wa rohoni
▪Kuyajua mapenzi ya Mungu
▪Kuishi kwa imani
▪Kuelewa sauti ya Mungu anapozungumza na mtu kwa njia mbalimbali.

AINA KADHAA ZA UKUAJI WA KIROHO
1. Kukua katika neema (2 Petro 3:18)
-Kwanza ni kuijua neema uliyopewa au waliyopewa watu wengine (Wagalatia 2:9) na namna ya kuenenda katika neema hiyo au neema hizo (neema ziko za namna mbalimbali 1 Petro 4:10)

2. Kukua katika kumjua Bwana Yesu (2 Petro 3:18)
-Kumjua Yesu ni nani, uwezo wake nakadhalika.

(Mathayo 8:37) Wanafunzi wa Yesu walikuwa naye sikuzote lakini kuna namna walikuwa hawajamjua waliyenaye, alipozikemea pepo na bahari walisema "huyu ni mtu wa namna gani hata pepo na bahari zinamtii" jambo hilo liliongeza kitu ndani yao wakazidi kuujua uwezo wake.

3. Kukua katika karama za Roho Mtakatifu (1 Wakoritho 12:1)
-Kuzifahamu karama za Roho Mtakatifu na jinsi zinavyofanya kazi.

BAADHI YA ISHARA ZINAZOONYESHA KUTOKUKUA KIROHO
1. Tabia za mwilini (1Wakorintho 3:1-7)

2. Kuendelea na mambo ya kitoto (1 Wakorintho 13:11)
-Kwa mfano tukiona mtu mzima anachezea midoli au anachezea makopo tutasema amechanganyikiwa.

Vivyo hivyo mtu ambaye ameokoka lakini hakui kiroho huwa anaendelea kufanya mambo ya kitoto kama vile kuzira au kuacha kufanya kazi ya Mungu kwa kuwa hajasifiwa au kupongezwa, kuacha kuomba kwa kuwa wengine hawaombi, kuacha kutoa kwa kuwa wengine hawatoi nakadhalika.

3. Kutokuwa na maendeleo katika maisha ya mtu binafsi na ndani ya kanisa.
(3 Yohana 1:2) Ukuaji wa kiroho huwa unaathiri maisha yetu ya kimwili, katika maisha ya kimwili lazima yaonekane maendeleo ya kimwili yaani kutoka hatua moja kwenda nyingine.

Kwa mfano ukiona kanisa lolote liko vilevile na miaka inaenda ujue hapo watu hawakui kiroho.

Ushuhuda kuhusu utoto na athari zake, sikumoja nilikuwa natembea na mtoto wangu nikiwa nimemshika mkono, wakati tunatembea Roho wa Mungu aliniambia "ukitembea na mtoto hauwezi ukafika kwa wakati unakokwenda kwa kuwa mwendo wa mtoto na mwendo wako ni tofauti kwa hiyo ukitaka uwahi kufika unakoenda itakubidi kumbeba mtoto. Ndivyo ilivyo katika kanisa likiwa na watoto wachanga kiroho itachukua muda mrefu kupata maendeleo.

BAADHI YA SABABU KWA NINI WATU HAWAKUI KIROHO
1. Kutopata chakula au kutopenda kula.
(Mathayo 4:4)
-Ukuaji wa kimwili au kiroho unategemea mambo mengi ikiwemo lishe bora.

Neno la Mungu ni chakula cha kiroho ambacho watu wanapaswa kulishwa na kukila wao wenyewe kwa njia ya kusoma na kujifunza neno la Mungu.

Watu wasipolishwa (wasipofundishwa), watu wasipokula (wasiposoma na kujifunza neno la Mungu) hawawezi kukua kiroho.

2. Kutokuwa na ushirika na Roho Mtakatifu au kutokufuata uongozi wa Roho Mtakatifu (Tito 3:5)
-Tulifanywa viumbe vipya kupitia Roho Mtakatifu, hivyo basi hatuwezi kukua bila Roho Mtakatifu.

Lazima tufuate Roho Mtakatifu anavyotuongoza.

HATUA ZA KUCHUKUA ILI UWEZE KUKUA KIROHO
1. Tamani kukua au uwe na shauku ya kukua.
-Mambo ya kiroho hayatatokea kwako kama hauyatamani au hauna shauku nayo ndio maana Biblia inasema "yatamanini maziwa ya akili"

Mtu anayetamani kukua lazima awe na bidii ya kusoma na kujifunza neno la Mungu, ikiwa kuna jambo halielewi anawajibika kuuliza ili aelewe.

2. Uwe mtendaji wa neno la Mungu (Yakobo 1:22-23)
-Neno la Mungu lina nguvu ila hauwezi kuona nguvu zake kama haulitendei kazi.

Hauwezi kuujua utamu wa chakula ikiwa haujawi kula hicho chakula, kuhadithiwa jinsi chakula fulani kilivyo kitamu haikufanyi wewe kuujua utamu wake.

3. Jizoeze kula vyakula vya watu wazima na kufanya mambo ya watu wazima kiroho.

-Kuna vyakula vya watoto wachanga kiroho (1 Petro 2:2)(1 Wakorintho 3:1-)

-Kuna vyakula vya watu wazima kiroho (Waebrania 5:14)

-Kuna kujizoeza kufanya mambo fulani (1 Timotheo 4:8)(Waebrania 5:14)

Kujizoeza mambo ya kiutu uzima ni kujizoeza kufunga na kuomba, kuamka alfajiri unamuomba Mungu, kuamka usiku unamuomba Mungu, kutenga muda wa kutafakari, kujifunza neno la Mungu nakadhalika.

Ukijoeza mambo hayo utajipata unaanza kukua kiroho.

HITIMISHO
Zipo faida nyingi sana za kukua kiroho pia zipo hasara za kutokukua kiroho ambazo ni pamoja na kudanganywa na kupotezwa na mafundisho ya uongo (ya kishetani).

 

Chapisha Maoni

0 Maoni