KUFANYA KAZI PAMOJA NA MUNGU


Utangulizi

Mungu alipomuumba mtu, alitaka kushirikiana na mtu katika kazi.

Kwa mfano

●Mungu alitengeneza bustani ya Edeni kisha akamuweka Adamu ailime na kuitunza (Mwanzo 2:15)

●Mungu aliumba wanyama na ndege akamletea Adamu awape majina (Mwanzo 2:19)

Tangu mwanzo Mungu alifanya kazi pamoja na mtu, hata sasa Mungu anataka tufanye kazi pamoja naye.

Kufanya kazi pamoja na Mungu ni;-

●Kufanya kazi kwa kushirikiana na Mungu.

●Kufanya kazi kwa kutumia akili za Mungu, mawazo ya Mungu na nguvu za Mungu.

●Kufanya kazi sawasawa na neno la Mungu au bila kwenda kinyume na neno la Mungu.

MAKUNDI MAKUU MAWILI YA KAZI

●Kazi za huduma (Waefeso 4:11-12)

Kufundisha, kuhubiri, kuponya wagonjwa nakadhalika.

●Kazi za mikono (Waefeso 4:28)

Kazi za kuajiriwa, kujiajiri, biashara, kilimo nakadhalika.

NB: Katika kazi zote hizo (kazi za huduma na kazi za mikono) Mungu yuko tayari kufanya kazi pamoja nasi ikiwa tutampa nafasi.

KWA NINI UFANYE KAZI PAMOJA NA MUNGU (BAADHI YA SABABU)

●Kwa sababu wengine wanafanya kazi na shetani.

(Matendo ya mitume 16:16) huyo binti alikuwa na pepo wa uaguzi, kupitia pepo huyo aliwasaidia watu katika kazi zao.

Wapo watu ambao wameweka vitu vya kishetani kwenye biashara, kwenye ofisi zao nakadhalika.

Kama haufanyi kazi pamoja na Mungu huwezi kuwashinda watu hao, huwezi kufanikiwa zaidi ya hao watu.

●Kwa sababu kila kazi ina upinzani.

-Hata mwizi ana mpinzani wake aitwaye askari polisi.

-Kwenye biashara kuna upinzani, wale wanaofanya biashara kama yako ni wapinzani wako hata kama hawapingani nawe moja kwa moja.

-Mahali pa kazi kuna upinzani, wapo wanaotaka hicho cheo ulichonacho au hiyo nafasi uliyo nayo, Danieli aliinukiwa kule kazini (Danieli 6:1-25)

Isaka alikuwa mkulima, watu wake walichimba visima lakini wapinzani wa Isaka walivifukia (Mwanzo 26:13-25)

Tunapofanya kazi pamoja na Mungu anatusaidia kuwashinda wapinzani wetu.

●Ili usidhulumiwe haki zako.

-Yakobo alifanya kazi kwa Labani, kama Mungu asingekuwa pamoja na Yakobo, Labani angemdhulumu Yakobo (Mwanzo 31:41-42)

MADHARA YA KUFANYA KAZI BILA MUNGU

●Utafanya kazi ya kuchosha.

(Luka 5:5) Petro alimwambia Yesu tumefanya kazi lakini ni kazi ya kuchosha.

Kazi ya kuchosha ni pale ambapo unafanya kazi lakini haupati matunda ya kazi zako, unatumia nguvu nyingi lakini haupati matokeo mazuri, unafanya kazi lakini unaishia kudhulumiwa nakadhalika.

Petro alipogundua wanafanya kazi ya kuchosha alimwambia Yesu aseme neno, neno la Yesu lilisababisha wakapata faida.

●Hautafaidika na kazi zako.

(Luka 12:16-21) huyu mtu alifanya kazi kwa bidii lakini alikufa kabla hajala matunda ya kazi zake.

NAMNA YA KUFANYA KAZI NA MUNGU

●Mpende Mungu.

-Mungu hufanya kazi na wanaompenda (Warumi 8:28)

Kumpenda Mungu ni kushika neno lake, ni kufanya anachotaka au anachoelekeza.

●Msikilize Mungu au uwe na neno la Mungu.

(Luka 5:5) Petro alimwambia Yesu "kwa neno lako nitaenda kuvua" Petro alifuata kile alichoambiwa na Yesu.

(Kumbukumbu la torati 28:1-10) Ukitii kile ambacho Mungu anasema, Mungu atakuwa pamoja na wewe kwenye mambo yako.

Mungu hufanya kazi na watu wanaofuata neno lake (Marko 16:20).

Fanya yale ambayo Mungu anakuongoza kufanya.

HITIMISHO

Mungu yuko tayari kufanya kazi na walioajiriwa (Mwanzo 39:2-3)

Mungu yuko tayari kufanya kazi na wafanya biashara (Mithali 3:13-14)

Mungu yuko tayari kufanya kazi na watumishi wa madhabahu na wale wenye huduma (Marko 16:20)

Mungu yuko tayari kufanya kazi na wakulima (Mwanzo 2:15)

Mungu yuko tayari kufanya kazi na mtu yeyote ambaye yuko tayari kutembea naye (Amosi 3:3)

Chapisha Maoni

0 Maoni