MAANDAMANO KIBIBLIA


 ✍Faraja Gasto

Nimeona vema nitoe elimu kidogo kuhusu maandamano kwa mujibu wa Biblia kwa kuwa kumekuwa na mkanganyiko na upotoshaji wa baadhi ya watu, wengine wanasema maandamano yanaharibu utukufu wa Mungu, wengine  wamekuwa wanadai maandamano yanaharibu amani nakadhalika.

IKO HIVI

Biblia inaripoti kuwa hapa duniani maandamano yalianza zamani sana, Mungu amekuwa akiratibu na kusimamia maandamano kupitia watu, shetani amekuwa akiratibu na kusimamia maandamano kupitia watu pia watu wenyewe wamekuwa wakiratibu na kusimamia maandamano yao.

MSISITIZO: Yapo maandamano yameripotiwa na Biblia ambayo yaliratibiwa na kusimamiwa na Mungu mwenyewe kupitia watu.

Nirejee kisa kimoja tu cha MAANDAMANO YA WAKOMA WANNE YALIYORATIBIWA NA KUSIMAMIWA NA MUNGU.

(2 WAFALME 7:3-16)

Kutokana na torati iliyokuja kwa mkono wa Musa, wakoma walitakiwa kutengwa nje ya mji na hicho ndicho kiliwapata wakoma hao wanne kwenye andiko hilo.

Sikumoja wale wakoma wanne wakiwa nje ya mji walikotengwa walifanya kikao, katika kikao kile walitathmini hali ya usalama wao wakagundua kuwa "wakiendelea kukaa pale walipo watakufa kwa njaa halikadhalika wakienda kwa maadui wa taifa lao watauawa".

Kupitia kikao kile waliazimia ni heri kwenda kwa maadui wa taifa lao ambao wana chakula kuliko kukaa pale.

NB: Ukisoma habari ya hao wakoma utagundua aliyeratibu na kusimamia maandamano yao ni Mungu, baada ya wao kuanza maandamano yao ghafla Mungu akawasikizisha maadui wa taifa lao kishindo cha magari ya vita hatimaye maadui wa taifa lao wakakimbia (2 WAFALME 7:5-7), hawakujua yalikuwa maandamano ya wakoma wanne tu tena maandamano ya watu wenye njaa wanaotafuta chakula tena watu waliojikatia tamaa.

HIVYO BASI si kila aina ya maandamano yanakatazwa kibiblia.

Maandamano yanayokatazwa na Mungu ni maandamano ya kutenda uovu.

"Usiandamane na mkutano kutenda uovu; wala usitie ushahidi wako katika neno lo lote kwa kugeukia kando na kuandamana na mkutano ili kupotoa hukumu" (KUTOKA 23:2)

Chapisha Maoni

0 Maoni