(Mwanzo 3:1-7)
UTANGULIZI
Shetani anafanya kazi zake ili kuua, kuharibu na kuiba (Yohana 10:10) katika kufanya kazi hizo hutumia nyenzo mbalimbali kama silaha zake, chakula ni nyenzo mojawapo ambayo shetani hutumia kuua, kuharibu na kuiba.
Tangu mwanzo tunaona katika Biblia shetani alihakikisha Adamu na mkewe wanakula chakula Mungu aliwazuia wasile (Mwanzo 3:1-7) walipokula maisha yao yakaharibika pia shetani akafunguliwa mlango wa kufanya uharibifu, wizi na mauaji hapa uliwenguni.
Kila mmoja anapaswa kufahamu chakula ni silaha mojawapo katika vita vya kiroho, silaha hiyo hata Mungu anaitumia, kwa mfano Mungu anasema “adui yako akiwa na njaa mlishe akiwa na kiu mnyweshe, kwa kufanya hivyo utampalia makaa ya moto kichwani” (Warumi 12:20). Biblia inatuambia Nabii Elisha alimwambia Mfalme ayape chakula majeshi ya Shamu (2 Wafalme 6:18-23) Biblia inasema walipokula chakula wakaondoka majeshi hayo hayakuja tena kupigana na Israeli.
Shetani naye ameendelea kutumia chakula kuua, kuharibu na kuiba vitu mbalimbali kutoka kwa watu mbalimbali ndio maana kuna watu huwa wanaota ndoto wanalishwa vyakula au wanapewa chakula, wengine huwa hawaelewi maana yake, somo hili litawasaidia watu kuelewa kuhusu mambo ya msingi ya vita vya kiroho kupitia vyakula.
NAMNA SHETANI ANAVYOTUMIA CHAKULA KAMA SILAHA YAKE
1.Shetani anatumia chakula kutega mitego yake.
(Hesabu 25:1-3) Shetani aliwanasa wana wa Israeli kupitia chakula wakaungamanishwa na madhabahu ya miungu ya Baali Peori iliyoabudiwa na wamoabi.
Kwa mfano watu wengi wanapotaka kuua panya huwa wanatumia chakula, kwenye kile chakula wanaweka sumu au wanaweka chakula ndani ya mtego, panya akiingia ndani ya mtego ili ale chakula atanaswa na ule mtego. Shetani naye hutumia chakula kutega mitego yake ili kuua, kuharibu na kuiba.
2.Shetani anatumia chakula kuingiza roho Fulani ndani ya mtu au watu.
(Hesabu 25:1-3) wana wa Israeli walikaa Shitimu siku moja wakaalikwa kwenye sherehe, walipokula kile chakula roho ya uzinzi iliwaingia wakaanza kuzini na wanawake wa Moabu.
3.Shetani anatumia chakula kuchukua alichonacho mtu.
(2 Wakorintho 4:4) Shetani anaitwa mungu wa dunia, mtu ndiye aliumbwa awe mungu wa dunia lakini alipoasi kupitia chakula alichokula shetani aliipata ile mamlaka ya kuwa mungu wa dunia hii.
(Mwanzo 25:29-34) Esau alimuuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza kupitia chakula, Esau alipokula kile chakula kuna kitu kilihama kutoka kwake kwenda kwa Yakobo. Shetani naye huwa anatumia vyakula kuchukua alichonacho mtu.
4.Shetani hutumia chakula kuua mtu.
(Mwanzo 3:1-7) Shetani alihakikisha wanakula lile tunda maana shetani alijua wakila lazima watakufa. Hata leo shetani ameendelea kuua watu kupitia vyakula, wengine wamewekewa sumu kwenye vyakula wakafa, wengine wamewekewa vitu vibaya kwenye vyakula na wakaharibikiwa kabisa.
5. Shetani hutumia chakula kumuunganisha mtu na madhabahu za kishetani.
Biblia imeweka wazi kuwa kuna vyakula mtu akila vinamuunganisha na madhabahu yaani kunakuwepo ushirika kati ya mtu na madhabahu Fulani (1 Wakorintho 10:18)
(Hesabu 25:1-3) Shetani alitumia vyakula kuwaungamanisha wana wa Israeli na madhabahu ya miungu ya Baali Peori iliyoabudiwa na wamoabi.
6.Shetani hutumia chakula kuharibu afya na miili ya watu ili wafe.
Kwa mfano kuna watu ambao chakula chao kikuu ni chips mayai na soda, vyakula kama hivyo vikitumika kwa muda mrefu lazima vilete madhara kwenye afya na mwili wa mtu.
Kuna watu maumbo ya miili yao hayaeleweki au yameharibika kutokana na kula ovyoovyo, wengine ni wanene kupita kiasi kutokana na mitindo mibaya ya kula, kuna watu wana matumbo makubwa (vitambi) kutokana na mtindo mbaya wa kula. Hiyo yote ni mikakati ya shetani ya kumuharibu mtu kupitia vyakula.
NAMNA YA KUSHINDA VITA VYA KIROHO AMBAVYO SHETANI ANATUMIA CHAKULA KAMA SILAHA
1.Mungu akikuzuia usile chakula Fulani au usile kwa mtu Fulani au usile mahali Fulani hakikisha unamtii Mungu.
(Mwanzo 3:1-7) Mungu alimwambia Adamu usile matunda ya mti ulio katikati ya bustani wala usiyaguse maana siku utakayokula matunda ya mti huo utakufa hakika, tunaona baada ya Adamu na mkewe kula lile tunda kulitokea matatizo makubwa duniani ikiwemo na kifo.
(1 Wafalme 13:7-26) Mungu alimwambia mtumishi wake aende Betheli kupeleka ujumbe akamwambia asile wala kunywa kule Betheli lakini yule Nabii alishawishiwa kula chakula na kunywa maji kule Betheli, alipokula na kunywa akaanza safari ya kurudi alikotoka simba walimuua.
2.Epuka ulafi.
(Wagalatia 5:19-21)(Warumi 13:13) tafsiri rahisi ya ulafi ni “tamaa ya chakula” au “kula bila mpangilio” yaani ni pale ambapo mtu anataka kula kila anachokiona mbele yake. Kula bila mpangilio kunasababisha kujaza mwilini vitu ambavyo havitakiwi. Watu walafi hupatwa na matatizo mbalimbali ikiwemo unene uliopitiliza nakadhalika.
3.Boresha mfumo wako wa kula.
Kuboresha mfumo wako wa kula ni kuhakikisha unakula kwa wakati au unazingatia muda wa kula, kuna vyakula vya aina tofauti na kwa mpangilio mzuri.
(1 Wafalme 17:2-6) Mungu aliwatuma Kunguru walimletea chakula Nabii Eliya asubuhi na jioni yaani kwa wakati huo Nabii Eliya alikuwa anakula mara mbili kwa siku, alikula nyama na mkate asubuhi pia alikula nyama na mkate jioni.
Mungu alimuwekea Nabii Eliya mpangilio mzuri wa kula kutegemeana na aina ya chakula alichokuwa anakula.
4. Mshukuru Mungu na kubariki chakula kabla haujala au ombea chakula.
(Mathayo 14:19) Yesu alishukuru kisha akabariki chakula baada ya hapo watu wakaketi kula chakula, pia Biblia inasema chakula kinaweza kutakaswa kwa kuomba (1 Timotheo 4:3-5). Kabla haujala chochote hata kama ni chakula kidogo sana hakikisha unakiombea au unakibariki kabla ya kula, wengine wanapokula jojo, pipi, karanga na vyakula vingine vidogo huwa hawaombei au kuvibariki.
Msisitizo: Mungu akikuzuia usile chakula Fulani au usile chakula kwa mtu Fulani au usile chakula mahali Fulani hakikisha hauli, hata ukiombea chakula au kubariki chakula lazima kitakuletea madhara kwa kuwa haujamtii Mungu.
5.Jipatie maarifa kuhusu vyakula.
(Hosea 4:9) Biblia inasema “watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa” maarifa ni ya muhimu sana katika maisha yetu ya kila siku, aina mojawapo ya maarifa ambayo kila mtu anapaswa kuwa nayo ni maarifa ya vyakula ili aweze kujilinda dhidi ya magonjwa na matatizo mbalimbali.
(2 Wafalme 4:38-41) Biblia inasema mtu mmoja alipika chakula asichokifahamu vyema, chakula kile kilitaka kuwaangamiza lakini Nabii Elisha alipata ufunuo wa kukifanya chakula kile kisiwe na madhara. Ni muhimu sana kujipatia maarifa kuhusu vyakula ili ufahamu ulaji sahihi wa chakula fulani ili kisije kukuletea madhara.
6.Muombe Mungu akupe kuelewa ndoto ambazo zinahusiana na masuala ya vyakula.
Ziko ndoto nyingi zinazohusiana na vyakula, baadhi ya ndoto hizo ni kuota unapewa chakula, kuota nafaka, kuota wanyama wa kufugwa kama vile ng’ombe, mbuzi, kondoo nakadhalika.
Ni muhimu sana kuelewa ndoto za vyakula ili iwe rahisi kushughulikia ndoto ambazo zinaleta mambo mabaya au taarifa za mabaya dhidi yako.
(Mwanzo 40:16-22) aliota nyungo tatu za mikate myeupe ziko kichwani, ungo wa juu ulikuwa na kila aina ya chakula kwa ajili ya Farao ndege wakala vile vyakula. Ukiisoma tafsiri ya ndoto ile utaona chakula kilimuwakilisha Yule aliyeota ndoto, alipoona ndge wanakula kile chakula maana yake alitakiwa kuuawa kisha ndege waile nyama yake.
(Mwanzo 42:) Mfalme Farao aliota ng’ombe wanene na wembamba, masuke manene na membamba, ukiisoma tafsiri ya ndoto yake utaona ilimaanisha kuna miaka saba ya njaa inakuja duniani na kuna miaka saba ya shibe. Kwenye ndoto ile Mungu alitumia vyakula kumueleza Mfalme Farao nini kinakwenda kutokea duniani.
Nimekutazamisha mambo hayo machache ili upate picha kidogo kuhusu ndoto za vyakula na umuhimu wa kuelewa maana yake ili iwe rahisi kushughulikia ndoto ambazo zina taarifa ya mambo mabaya yanayokusudiwa kukupata.
HITIMISHO
Nimefundisha somo hili ili kukuwekea msingi wa ufahamu kuhusu vita vya kiroho pale ambapo shetani hutumia chakula kama silaha yake ili uwe mshindi katika vita hivyo.
Ninaamini Mungu ataendelea kukufunulia mambo mengine usomapo Biblia.
0 Maoni