NAMNA YA KUANDAA MRADI KWA MUJIBU WA BIBLIA

 

Lengo la somo ni kumpa mtu maarifa ya uandaaji wa mradi na uandishi wa andiko la mradi kwa mujibu wa Biblia.

UTANGULIZI

Tutajifunza somo hili kupitia kisa cha mtumishi wa Mungu aitwaye Nehemia ambaye wazo na Mungu la kujenga kuta za Yerusalemu (Nehemia 2:11-12)

Nehemia hakuandika andiko la mradi ila alitekeleza mradi ambao wazo la mradi lilitoka kwa Mungu, ni sawa na kusema Mungu alianzisha mradi na kuutekeleza kupitia mtumishi wake Nehemia.

Habari ya Nehemia inatupa kufahamu mambo ya msingi kuhusu uandaaji na utekelezaji wa miradi mbalimbali hata isiyofanana na mradi alioutekeleza Nehemia.

SIFA ZA MRADI

1.    Wazo la mradi (Nehemia 2:12)

Wazo la mradi lilitoka kwa Mungu kutokana na kuharibiwa kwa mji wa Yerusalemu, kwa hiyo matatizo matatizo yaliyopo sehemu mbalimbali yanaweza kupelekea au yanaweza kusababisha kutokea kwa mawazo ya kuanzisha miradi mbalimbali.

Hivyo basi katika kuandaa miradi ni muhimu kuainisha tatizo au matatizo au changamoto.

2.    Aina ya mradi (Nehemia 2:5,17-18)

Mradi wa Nehemia ulikuwa mradi wa ujenzi (construction project). Wazo la mradi ndilo huamua aina ya mradi, hivyo basi kwa kuwa mawazo yanatofautiana, aina za miradi hutofautiana.

3.    Lengo au malengo ya mradi (Nehemia 2:12)

Lengo la mradi ule lilikuwa kurejesha hadhi ya mji wa Yerusalemu ili kuwaondolea aibu wayahudi (Nehemia 2:17-18). Unapoandaa mradi au andiko la mradi unapaswa kueleza malengo au lengo la mradi.

4.    Umuhimu wa mradi (Nehemia 2:17-18)

Mradi ule ulipaswa kutekelezwa ili kuwafanya wayahudi wasiendelee kudharaulika machoni pa mataifa, Nehemia aliwaambia wayahudi wajenge ili wasiwe shutumu (yaani ni aibu mji wao kuwa katika hali ile), ulikuwa mradi ambao ungerejesha heshima yao kama taifa. Hivyo basi unapoandaa mradi au andiko la mradi lazima lionyeshe umuhimu wa mradi huo yamkini ni kwa jamii, kwenye taasisi au kwenye taifa.

5.    Wanufaika wa mradi (Nehemia 4:1)

Wanufaika wa mradi walikuwa wayahudi. Hivyo basi unapoandaa mradi au andiko la mradi ni muhimu kuainisha wanufaika wa mradi.

6.    Eneo la mradi (Nehemia 2:11)

Eneo la mradi ni eneo ambapo mradi utatekelezwa, mradi wa Nehemia ulitekelezwa katika mji wa Yerusalemu. Hivyo basi unapoandaa mradi au andiko la mradi lazima uonyeshe mahali ambapo mradi utatekelezwa.

7.    Muda wa mradi (Nehemia 2:6)

Muda wa mradi ni muda ambao utatumika kutekeleza mradi kwa mfano mradi unaweza ukawa wa wiki moja, mwezi, miezi au miaka. Nehemia alieleza muda atakaoutumia kutekeleza mradi wake.

8.    Mahitaji ya mradi

Mahitaji ya mradi ni nyenzo zinazohitajika kutekeleza mradi, mradi wa Nehemia ulihitaji miti (Nehemia 2:7-8) na nguvu kazi (Nehemia 2:17-18)

9.    Usimamizi wa mradi (Nehemia 2:6)

Mradi wa Nehemia aliusimamia yeye akishirikiana na watu wengine, usimamizi wa mradi unahusiha mambo yafuatayo:-

a)    Kugawa majukumu na kuhakikisha kila mtu anatekeleza majukumu yake aliyopangiwa.

b)   Kazi zilizopangwa kufanyika zinafanyika kwa wakati husika.

c)    Ufuatiliaji, ufuatiliaji hufanyika ili kuona kama kazi zilizokusudiwa kufanywa na kupitia mradi zinafanyika na rasilimali zinatumika sawasawa na malengo yaliyopo.

d)   Tathmini hufanyika ili kuona kama mradi unatimiza au umetimiza lengo au malengo ya mradi.

Chapisha Maoni

0 Maoni