MAOMBI YA MUDA MREFU NA FAIDA ZAKE


 Faraja Gasto

YALIYOMO KATIKA SOMO

1. Mbinu za Kukusaidia uweze kuomba kwa muda mrefu

2. Faida za kuomba kwa muda mrefu

3. Mbinu anazotumia shetani ili kukufanya usiombe kwa muda mrefu

LENGO LA SOMO

1. Kukufanya uushinde uvivu wa kuomba kwa muda mrefu

2. Kukuwezesha kuomba kwa muda mrefu

KWELI KUU YA SOMO

Hakuna awezaye kuomba kwa muda mrefu bila msaada wa Roho Mtakatifu

UTANGULIZI

Kanisa la sasa linasumbuliwa na aina nyingi za uvivu ila kuna uvivu wa aina mbili ambo umekithiri

1. Uvivu wa kusikia neno la Mungu (Waebrania 5:11)

2. Uvivu wa kuomba kwa muda mrefu (Marko 12: 37)

Wakristo wengi wanapenda ukristo wa kutabiriwa, kuombewa na ukristo wa kuitikia amina ilihali hawataki kulipa gharama ndio maana makanisa mengi na wakristo wengi hawana nguvu za Mungu, makanisa yamebaki na majina ya kipentekoste lakini upentekoste umetoweka.

Wakristo wanataka wakiingia makanisani waombe dakika 5, 10 au 20 au wasali sala ya Bwana kisha waimbe masaa 2 n.k NI HATARI.

 

MAOMBI YA MUDA MREFU NI YAPI?

Ni maombi yanayochukua saa moja na zaidi. Yesu alimuuliza Petro Je! haukuweza kuomba hata saa moja? (MARKO 12:37)

Jiulize mara ya mwisho kuomba zaidi ya saa moja ni lini?

Jambo mojawapo lililomfanya Bwana Yesu akafanya mambo makubwa alipokuwa duniani ni maombi ya muda mrefu, Yesu alikuwa shujaa katika kuomba (prayer worrior)

Watu Wengi hawajaijua siri ya maombi ya muda mrefu ndio maana wanategea kuomba Kama Petro na wenzake walivyotegea pindi walipokuwa Ghetsemane.

Imekuwa si ajabu kuona hata viongozi wa makanisa ni wavivu wa kuomba, uvivu huo umeenda hadi kwa washirika hatimaye makanisa yamekuwa kama mazizi ya kufuga wakristo wavivu, wakristo wanaoweza kutikiswa na malango ya kuzimu, wakristo wanaorogwa na kurogeka.

Yesu hataki kuona uvivu huo ndio maana alimuuliza Petro, "haukuomba hata saa moja?

 

MBINU ZA KUKUSAIDIA KUOMBA KWA MUDA MREFU.

1. UWE NA KIU (HAJA) YA KUOMBA KWA MUDA MREFU.

Kiu ya kutaka mambo ya rohoni huwa inamvutia Mungu ili akupe haja ya moyo wake.

2. TENGA MUDA WA KUOMBA NA PIA TAFUTA MAHALI AMBAPO UTAPATA UTULIVU WA KUOMBA.

(Luka 6:12)

Yesu alikuwa na utaratibu wa kutenga muda wa kuomba na pia alikuwa anakwenda mahali pa faragha anaomba.

3. KUNENA KWA LUGHA KWA MSAADA WA ROHO MTAKATIFU.

(Warumi 8:26)

-Nilikuambia kuwa hakuna awezaye kuomba kwa muda mrefu bila msaada wa Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu unapompa nafasi katika maombi utashangaa kunena kwa lugha kunatokea wakati unaendelea kuomba.

4. WEKA NENO LA MUNGU KWA WINGI NDANI YAKO.

(Wakolosai 3:16)

- Kazi mojawapo ya neno la Mungu ni kukutengenezea kiu za aina tofauti ikiwemo na kiu ya kuomba.

Hizo ni mbinu nne zitakazokusaidia uombe kwa muda mrefu endapo utazitendea kazi utajikuta unaomba zaidi ya saa moja mfululizo.

 

FAIDA ZA KUOMBA KWA MUDA MREFU

Nitakuonyesha faida chache ili kukutengenezea kiu ya kuomba.

1. UTAZUNGUKWA NA UTISHO WA MUNGU

Kati ya kitu ambacho watu wanakikosa ni utisho wa Mungu Kwenye maisha yao.

(MARKO 5:1-12)

Yesu alikuwa anapita tu ghafla mapepo yakaanza kulalamika (kujishtukia) Yesu alikuwa amezungukwa na utisho ulioyatikisa mapepo.

(Esta 4:12-17, 5:1-3)

Wayahudi walipotangaziwa kuwa watauawa walifanya maombi ya muda mrefu kwa kufunga kwa muda wa siku tatu, yale maombi yaliachilia utisho wa Mungu kwa Malkia Esta hata akaingia kwa Mfalme kinyume na utaratibu kitu cha ajabu ni kwamba Mfalme hakukumbuka kuhusu sheria za kifalme badala yake akajikuta AMELAINIKA HATA AKAMWAMBIA ESTA HATA NUSU YA UFALME WANGU NITAKUPA, kilichomlainisha Mfalme hata akawa tayari kugawa nusu ya ufalme ni UTISHO WA MUNGU uliotokana na maombi ya muda mrefu.

Maombi ya muda mrefu yanawalainisha wagumu, wabishi n.k anza kuomba utashangaa matokeo ya maombi haya.

 

2. UTAISHINDA HOFU YA KIFO

Hofu ni silaha kubwa sana anayoitumia shetani kukabiliana na watu, hususani hofu ya kifo, ukiishinda hii basi utakuwa umemuweza shetani kwa viwango vikubwa

(Marko 14:32-41)

Shetani aliitumia hofu ya kifo kupambana na Yesu, ile hofu ilipomzunguka akajikuta anataka kuahirisha kufia msalabani ilibidi Roho Mtakatifu aingilie kati ili kumfanye Yesu aingie kwenye maombi ya muda mrefu ili ile hofu itoweke, ilipotoweka akawa tayari kufia msalabani.

(Wafilipi 1:21)

Paulo aliishinda hii hofu kwa kuwa alikuwa anaomba kwa muda mrefu ndio maana ilifika hatua akaona kifo si kitu "KUISHI NI KRISTO NA KUFA NI FAIDA"

Dawa ya hofu ya kifo ni maombi ya muda mrefu.

 

3. YATAIMARISHA MAHUSIANO YAKO NA MUNGU NA MUNGU ATAKUFUNULIA SIRI ZAKE NA ZA WANADAMU

(Yohana 4:4-19)

Yesu alifunuliwa maisha ya huyo mwanamke kuwa ana wanaume watano na hata aliye naye sio wa kwake, huyo mwanamke alishtuka kukutana na mtu asiyemfahamu ila anayajua maisha yake.

USHUHUDA

Wakati fulani niliwahi kukutana na mtumishi wa Mungu kutoka Uganda lakini aliniambia mambo ya maisha yangu japo hakuwa ananifahamu.

Ninachotaka uone hapo ni kwamba ukijizoeza kuomba maombi ya muda mrefu utashangaa mahusiano yako na Mungu yataimarika mpaka Mungu atakuwa anakuvujishia siri zake na za wanadamu.

(Yohana 1:47-50)

Yesu alipomuona Nathanaeli, Yesu alinena habari za Nathanaeli mpaka Nathanaeli akamuuliza "umenitambuaje? Yesu akamwambia nilikuona ulipokuwa chini ya mtini.

Maombi ya muda mrefu yanakufanya ufunuliwe maisha ya watu.

 

5. YATAKUFANYA UPATE MAMLAKA FULANI NA PIA YATAONGEZA MAMLAKA YAKO KATIKA ULIMWENGU WA ROHO

Sina uhakika kama watu wengi wanafahamu kuwa mamlaka zina viwango katika ulimwengu wa roho ndio maana utaona Yesu alisema "mamlaka YOTE nimepewa"

Kwa maana hiyo ni kwamba unaweza kuwa na mamlaka lakini usiwe na mamlaka yote.

Ninapozungumzia mamlaka katika ulimwengu wa roho ni ule uwezo wa kuamuru (authority to command) jambo na likatekelezwa kama jinsi ulivyoamuru.

(1 Wafalme 17:1)

Cheki kauli ya kibabe aliyoitoa Eliya akasema "hakutakuwa na mvua kwa miaka mitatu na nusu isipokuwa KWA NENO LANGU" Eliya hazungumzii unabii anazungumza kulingana na mamlaka aliyonayo katika ulimwengu wa roho, kwamba ana mamlaka ya kuamua mvua inyeshe ama isinyeshe.

Sasa usidhani kuokoka kunakufanya uwe na mamlaka yote, maombi ya muda mrefu ni njia mojawapo kubwa ya kupata mamlaka za aina mbalimbali na kuongeza mamlaka yako ya rohoni.

 

6. YANAFUNGUA MAMBO YALIYOFUNGWA NA PIA YANAFUNGUA VIFUNGO VYA KIMWILI NA KIROHO

Wapo watu wamefungwa fahamu zao, wapo wana magonjwa yatokanayo na vifungo, wapo waliofungwa matumbo wasizae watoto, na pia wapo waliopo magerezani kwa makosa ya kusingiziwa, uonevu na hila za shetani.

Maombi ya muda mrefu hayafungui vifungo vya kiroho tu bali hata vya kimwili.

(Matendo ya mitume 12:5-16)

Petro alipokamatwa akawekwa gerezani, kanisa lilifanya maombi ya muda mrefu hatimaye malaika alikwenda pale gerezani akamtoa Petro kutoka gerezani.

Ni vema ufahamu kuwa maombi ya muda mrefu ni maombi ya hatari sana kwa shetani ndio maana shetani hawapi watu nafasi ya kufanya maombi ya namna hiyo.

Ukweli ni kwamba kifungo chochote kinaweza kufunguliwa hatimaye mtu au watu wakawa huru, mbinu mojawapo ya kufungua vifungo ni maombi ya muda mrefu.

(Yakobo 5:17)

Eliya alifunga na kufungua mvua kwa maombi ya muda mrefu.

Fanya haya maombi utashangaa.

 

MBINU ANAZOTUMIA SHETANI ILI KUWAFANYA WATU WASIOMBE MAOMBI YA MUDA MREFU

1. SHETANI HUWAFANYA WATU WAWE NA KAZI NYINGI ILI WAKOSE MUDA WA KUOMBA

Mwili wako una nafasi katika kukufanya uombe kwa muda mrefu, ndio maana shetani huwa anahakikisha unakuwa na kazi nyingi ambazo zitauchosha mwili wako ili usiombe na hata ukiomba uombe kwa muda mfupi.

Hata kama una majukumu mengi yanayouchosha mwili fahamu kuwa kazi mojawapo ya Roho Mtakatifu ni KUKUSAIDIA KUUSHINDA UDHAIFU WA MWILI ili uombe kwa muda mrefu (Warumi 8:26)

Mwili wako hautaki mambo ya Mungu ila Roho iko tayari (Marko 14:38) kwa hiyo usije ukausikiliza mwili utakukwamisha katika maombi, mwili hautaki kufunga, mwili unataka upumzike ukiusikiliza hautaomba maombi ya muda mrefu.

(Wagalatia 5:17)

Ukitaka uombe kwa muda mrefu hakikisha hauupi nafasi mwili ukuhubirie.

Usikubali Kuwa na kazi nyingi zinazokunyima muda wa kufanya maombi ya muda mrefu, jifunze kuulazimisha mwili utii ya rohoni.

 

2. ATAHAKIKISHA MIOYO INAKOSA UTULIVU NA UJASIRI KWA MUNGU KWA KUTEKA FIKIRA ZA MTU AU WATU

(Mathayo 15:8)

Kuna uwezekano mkubwa mtu akawa anaonekana anaomba lakini moyo wake haupo hapo kwenye hayo maombi, ukiomba huku moyo uko kwingine unakuwa unaropoka tu.

Ndio maana unaweza kushangaa mtu anaomba huku anapiga miayo n.k shetani anaanza kukuletea mawazo mengine, anaanza kukutafakarisha mambo mengine, shetani anaanza kukukumbusha mambo mengine.

(1 Yohana 3:21)

Shetani anajua kuwa ukiomba huku moyoni unahukumiwa lazima utapoteza ujasiri wa kuomba na ukipoteza ujasiri wa kuomba hauwezi kuomba kwa muda mrefu, na hiyo ni vita ya shetani na moyo wako ili usije ukaomba kwa muda mrefu.

Ukiwa katika maombi halafu unajikuta una mawazo mengine au unahukumiwa, jifunze kuomba kwa kupaza sauti ili kuzima sauti za shetani, hiyo itakusaidia kuomba kwa muda mrefu.

Moyo wako una nafasi katika maombi marefu.

 

3. ATAKUFANYA AU ATAWAFANYA MUOMBE KWA AKILI KWA KUWATAZAMISHA MAHITAJI MENGI ILI MYAPELEKE KWA MUNGU KWA NJIA YA MAOMBI

Umeshawahi kutaka kuomba ukajikuta una mahitaji mengi ya kuombea halafu ukajikuta unaomba kila hitaji kwa dakika 5 au 10? au umeshawahi kwenda kwenye maombi halafu kiongozi wa maombi akataja mahitaji zaidi ya manne ya kuombea huku muda wa maombi ni saa moja au mawili au matatu, ukweli ni kwamba watu huwa wanaomba kwa dakika chache na wengine huwa wanaomba ili wamalize maombi.

Angalizo: hatutakiwi kuomba ili tumalize maombi, tunatakiwa kuomba ili tujibiwe maombi kwa hiyo usizoee kuwa na mahitaji mengi ya kuombea kwa wakati mmoja, ni heri kuomba hitaji moja kwa muda mrefu kuliko kuombea mahitaji mengi kwa dakika chache.

Ifike hatua watu tuzijue fumbo za shetani (Ufunuo 2:24), itatusaidia kumkabili shetani na hila zake.

 

4. ATAWAONDOLEA KUNIA MAMOJA (ATAWAGAWANYA)

Ukweli ni kwamba umoja una nafasi ya kuwafanya watu waombe maombi ya muda mrefu hususani ndani ya kanisa ndio maana Yesu alituombea umoja (Yohana 17:20-21)

Ukitazama makanisani utashangaa watu wanapenda maombi mepesi mepesi tu, na ikitokea umeleta agenda ya maombi ya muda mrefu utashangaa upinzani utainuka wa kutosha, tena si ajabu hata viongozi wa kanisa wakainuka kuwa wapinzani wako, hiyo yote inadhihirisha kuwa kanisa limeshavamiwa na watu hawajajua kuwa wamevamiwa.

Hata yakitangazwa maombi ya umoja (ya mapatano) si ajabu kuona watu hawaji na hata viongozi wa makanisa hawaji kabisa, ni hatari kwa kanisa kukosa maombi ya muda mrefu.

Washirikishe wengine somo hili ili wainuke mashujaa wa maombi (prayer worriors).

 

5. ATAHAKIKISHA ANAZUIA UTENDAJI KAZI WA ROHO YA UNABII

roho ya unabii ni nini?

Biblia inasema ushuhuda wa Yesu ni roho ya unabii (Ufunuo 19:10)

kati ya silaha hatari kwa shetani ni ushuhuda wa Yesu, shetani hapendi watu waambiwe ushuhuda wa Yesu.

Ushuhuda wa Yesu una nguvu za ajabu ndani yake ndio maana watu wengi shetani amewamwagia uvivu wa kushuhudia.

Maombi ya muda mrefu yanawapa watu nguvu, ujasiri na yanawatengenezea mazingira ya kutoa ushuhuda wa Yesu.

(Matendo ya mitume 2:1-41)

Wanafunzi wa Yesu Waliposhukiwa na Roho Mtakatifu walijikuta wamekuwa na maombi ya muda mrefu yaliwafanya wakapata ujasiri na yakatengeneza mazingira kwa ajili ya kutoa ushuhuda wa Yesu.

Mungu akubariki kwa hayo machache, zidi kusoma Biblia utafunuliwa siri za maombi ya muda mrefu.

 

Chapisha Maoni

4 Maoni