NGUVU ZA MUNGU ZINAVYOWEZA KUKUSAIDIA KUPATA HAKI ZAKO

 



(LUKA 18:1-8)

Mambo nitakayokufundisha katika somo hili

1.      Mambo yanayosababisha watu wasipate au wakose haki zao.

2.      Kuzijua haki zako kwa mujubu wa neno la Mungu (Biblia)

3.      Nguvu za Mungu zinavyoweza kukusaidia kupata haki zako.

Utangulizi

Ukisoma andiko la Luka 18:1-8 utapata kuona mambo kama matano

a).Kumuomba Mungu siku zote bila kukata tama (Luka 18:1)

b).Kuifahamu haki (Luka 18:5)

Huyo mwanamke mjane alidai haki yake kwa kuwa alikuwa na uhakika ni haki yake.

c).Haki inaweza kuzuiliwa au kuachiliwa (Luka 18:4)

Kadhi (hakimu) alikuwa anakataa kumpa mjane haki yake ilihali alikuwa akifahamu kweli mjane ana haki.

d).Haki inaweza kupatikana endapo kutakuwa na bidii au jitihada za kuidai

 (Luka 18:5-6)

Huyo mjane asingedai haki yake kwa bidii asingeipata.

e).Mungu huwapatia haki upesi watu wanaomlilia mchana na usiku  (Luka 18:1-7)

HAKI NI NINI?

Haki ni kile unachostahili kukipata au kupewa na mamlaka Fulani baada ya kutimiza wajibu Fulani.

àSisi wote tuliomwamini Yesu kuna haki zetu ambazo tunastahili kuzipata au kupewa na Mungu baada ya kutimiza wajibu Fulani, kwa hiyo ukitaka Mungu akupatie haki zao ni muhimu kutimiza wajibu wako kwake au wajibu wako sawasawa na neno lake.

 

MAMBO YANAYOSABABISHA WATU WASIPATE AU WAKOSE HAKI ZAO.

Watu wengi wamekuwa wakikosa haki zao kwa sbabu ya mambo makuu mawili

v  Kwa sababu yao wenyewe

v  Kwa sababu ya shetani

Nami nikuonyeshe angalau mambo kadhaa yanayosababisha watu wasipate haki zao.

1.     Dhambi

Ukisoma 2 Wakorintho 4:4 utagundua kuwa shetani anaitwa mungu wa dunia hii kwa kuwa baada ya Adamu na mkewe kutenda dhambi alipoteza haki yake ya kumiliki na kutawala katika dunia kwa hiyo shetani akachukua uhalali wa kumiliki na kutawala ndio maana wakati shetani anamjaribu Yesu, shetani aliwahi kumwambia Yesu kuwa “ukinisujudia nitakupa milki zote za ulimwengu” – Mathayo 4:8-10, Yesu hakumbishia shetani kwamba hana uwezo wa kumpa milki za ulimwengu kwa kuwa Yesu alijua ni kweli shetani alipata uhalali juu ya milki za ulimwengu baada ya Adamu na mkewe kutenda dhambi, Yesu alijibu “nenda zako shetani maana imeandikwa msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake”

(Yeremia 5:25)

Mungu aliwaambia wana wa Israeli kuwa maovu yao na dhambi zao zimesababisha wasipate mema, kwa mantiki hiyo ni kwamba dhambi na maovu huwa ni vizuizi (barriers) vinavyosababisha wanadamu wasipate aina Fulani ya mema kutoka kwa Mungu.

Kwa hiyo kila mtu anatakiwa kufahamu kuwa dhambi huwa zinasababisha mtu asipate haki zake kutoka kwa Mungu aliyemuumba.

2.     Kutokuwa na nguvu za kumdhibiti shetani ambaye huiba au hupora haki za watu.

Shetani ni kama jambazi, kuna wakati hutumia hila kukamilisha mipango yake na kuna wakati hutumia nguvu ili kupata anachotaka ndio maana utagundua kuwa jambazo huwa haombi bali huwa ananyang’anya kwa nguvu, ndivyo alivyo shetani huwa anawanyang’anya watu haki zao kwa nguvu kama hauna nguvu za kumdhibiti huyu adui atakuibia tu.

(Luka 11:21-22)

Biblia imeweka wazi kuwa mtu mwenye nguvu alindapo mali zake, mali zake zitakuwa salama lakini akija mwenye nguvu kuliko yeye atamnyang’anya mali alizonazo na kuzifanya kuwa za kwake.

Kwa mantiki hiyo ni kwamba ili uweze kumdhibiti shetani asikuibie aui asichukue haki zako kwa nguvu lazima uwe na nguvu kumshinda yeye na ili uwe na nguvu kumshinda shetani lazima umwamini Yesu Kristo maana yeye ana nguvu zaidi ya shetani, Yesu akiwa ndani yako na Roho wake akiwa ndani yako unakuwa na nguvu kuliko shetani.

Ukiwa na nguvu kuliko shetani utakuwa na mamlaka ya kumuamuru aachie haki zako, arudishe alichokuibia ambacho ni haki yako. Shetani ni kama Yule kadhi dhalimu ambaye alikuwa akizuia haki ya yule mjane huwa hataki watu wapate haki zao, ukiwa ndani ya Yesu ni rahisi kumkabili na akaachia haki zako.

3.     Kutofahamu haki.

(Wagalatia 4:1-2)

Mwana asiyezijua haki zake hana tofauti na mtumwa, kwa hiyo sisi kama wana wa Mungu tunatakiwa kuzifahamu haki zetu ili tusiishi kama watumwa.

KUZIFAHAMU HAKI ZAKO KWA MUJIBU WA NENO LA MUNGU.

Kama nilivyotangulia kusema kuwa kuna haki ambazo tunatakiwa kuzipata kutoka kwa Mungu ambaye ni Baba zetu na Mungu wetu tunayemtumikia, haki hizo tutazifahamu endapo tutakuwa na bidii ya kusoma neno la Mungu (Biblia) ndio maana ni muhimu sana kuwa na Biblia na kuisoma kila mara, Biblia itakusaidia kuzifahamu haki zako.

(Luka 15:11-12)

Huyu mtoto alifahamu kuwa ni haki yake kupewa urithi na baba yake kwa kuwa alifahamu haki zake ndio maana alikuwa na ujasiri wa kumuomba baba yake ampe urithi.#

Nimekutazamisha hilo ili ufahamu kuwa kuzifahamu haki zako kwa mujibu wa neno la Mungu kutakusaidia kuomba au kutakupatia ujasiri wa kumuomba Mungu, na huu ndio ujasiri tulio nao kwa Mungu kwamba tukiomba lolote sawasawa na mapenzi yake yeye anatusikia (1 Yohana 5:14)

Baadhi ya haki zako kwa mujibu wa neno la Mungu

1.      Haki ya kulindwa dhidi ya kila silaha na ulimi unaoinuka kinyume chako (Isaya 54:17)

2.      Haki ya kujazwa na kuongozwa na Roho Mtakatifu baada ya kumwamini Yesu (Matendo ya mitume 2:37-39)

3.      Haki ya kuishi maisha ya amani na furaha au maisha yasiyo na huzuni (Isaya 53:4-5)

Yesu alikufa msalabani ili sisi tuliomwamini tuishi maisha yasiyo na huzuni.

4.      Haki ya kuondolewa magonjwa, chakula chako na maji yako vibarikiwe, haki ya kuzaa na haki ya kuishi miaka aliyokupangia Mungu (Kutoka 23:25-26)

 

 

 

 

NGUVU ZA MUNGU ZINAVYOWEZA KUKUSAIDIA KUPATA HAKI ZAKO.

(Luka 18:2-5)

Biblia inasema Yule kadhi dhalimu alikuwa akikataa kumpa mjane haki yake, jaribu kufikiri umekwenda mahakamani kudai haki yako halafu hakimu akawa hataki kukupa haki yako na ilihali anafahamu kuwa wewe ndiwe mwenye haki, naamini utakuwa na uchungu sana lakini uchungu ule hauwezi kukusaaidia kupata haki yako ndio maana nakufundisha kuwa nguvu za Mungu zinaweza kukusaidia kupata haki zako.

Unatakiwa kufahamu kuwa shetani ni kama jambazi, shetani ni kama Yule kadhi dhalimu ambaye alikuwa anakataa kumpa mjane haki yake, endapo utamkabili shetani kwa  njia ya maombi lazima alegee au alainike na kuachia haki zako alizoiba au alizopora.

Usidhani shetani ataachia haki zako kwa urahisi, ni mpaka umbane umkabili katika ulimwengu wa ndipo anaweza kuachia haki zako alizozishika ndio maana Biblia inasema katika Waefeso 6:10-12

10. Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. 11. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. 12. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.

(Kutoka 6:1)

“Bwana akamwambia Musa, Sasa utaona nitakavyomtenda Farao; maana kwa mkono hodari atawapa ruhusa kwenda zao, na kwa mkono hodari atawafukuza katika nchi yake”

 

Haikuwa rahisi kwa Mfalme Farao kuwaruhusu wana wa Israeli kutoka katika nchi ya Misri ndio maana Mungu alimwambia Musa kwa mkono ulio hodari Mfalme Farao atawapa ruhusa muondoke.

 

Nakuhamisisha kujenga tabia ya kumkabili shetani kwa njia ya maombi kwa msaada wa Roho Mtakatifu ili iwe rahisi shetani kuachia haki zako alizodhulumu au alizopora au alizozizuia.

Kama wengine wameridhika na hali walizonazo, wameridhika na kukandamizwa na kuonewa na shetani, wewe usiridhike chukua hatua ya kumkabili shetani katika ulimwengu wa roho kwa njia ya maombi kwa msaada wa Roho wa Mungu ili aachie kila haki yako aliyozuia au aliyoiba.

Ninakuhakikishia kuwa nguvu za Mungu zitaingilia kati kukusaidia kupata haki zako, simama na neno la Bwana ambalo ni upanga wa Roho (Waefeso 6:17b) lazima shetani atasalimu amri na kuachilia haki zako.

Chapisha Maoni

0 Maoni