UMUHIMU WA KUTAFUTA KUFAHAMU MAANA YA NDOTO AU MAONO ULIYOYAONA

 



Mungu hutumia njia nyingi kuzungumza na mtu, baadhi ya njia hizo na ndoto na maono, mara nyingi Mungu hutujulisha mambo mbalimbali kupitia ndoto na maono na wakati mwingine mwingine watu wengi hujikuta wakipuuzia maono na ndoto walioota.

 

à Sio jambo la busara kupuuzia ndoto na maono uliyoyaona ndio maana nakufundisha na kukuhamasisha kutafuta kujua maana ya ndoto uliyoota na maono uliyoyaona.

 

(Danieli 8:15)

15. Ikawa mimi, naam, mimi Danielii, nilipoyaona maono hayo, nalitafuta kuyafahamu, na tazama, alisimama mbele yangu mmoja mfano wa mwanadamu.

16. Nikasikia sauti ya mwanadamu katikati ya mto Ulai, iliyoita na kusema, Gabrieli, mfahamishe mtu huyu maono haya.

 

Mtumishi wa Mungu  Danieli alionyeshwa maono lakini hakuelewa maana ya maono hayo ndipo aliamua kutafuta kuyafahamu maono hayo, Danieli alitafuta kuyafahamu maono hayo kwa njia ya maombi (alikuwa anaomba Mungu amjulishe maana ya maono hayo)

 

NB: Watu wengi huota ndoto na kuona maono lakini si wengi ambao huwa wanaelewa maana ya ndoto walizoota na maono waliyoyaona, kila mtu anatakiwa kufahamu kuwa ni muhimu sana kutafuta kufahamu maana ya ndoto au maono uliyoyaona.

 

Mifano ya watu ambao waliota ndoto na hawakuelewa maana ya ndoto.

1.      Mfalme Farao (Mwanzo 41:8)

Mfalme Farao aliota ndoto ambayo hakuielewa ilimaanisha nini au ilikuwa na ujumbe gani, baada ya kuamka asubuhi akaamua kuwaita waganga wote wa Misri na watu wote wenye hekima lakini hawakuweza kumtafsiria ndoto yake.

 

àNi vema kufahamu kuwa kile ambacho Mungu ameongea na wewe, ni yeye peke yake awezaye kukupa tafsiri ya kile alichokuambia kwa hiyo usiwaendee waganga, wasoma nyota n.k hawataweza kukupa tafsiri ndio maana waganga na wenye hekima wa Misri hawakuweza kutafsiri ndoto ya  Mfalme Farao.

 

2.      Mfalme Nebukadneza ( Danieli 4:4-7)

Mfalme Nebukadneza alipoota ndoto ambayo hakuielewa aliwaita waganga na wachawi na wakaldayo  na wanajimu lakini hawakuweza kutafsiri ile ndoto kwa kuwa kile ambacho Mungu ameongea na wewe, ni yeye peke yake awezaye kukupa tafsiri ya kile alichokuambia kwa hiyo usiwaendee waganga, wasoma nyota n.k hawataweza kukupa tafsiri.

 

MAMBO YATAKAYOKUSAIDIA ILI UFAHAMU MAANA YA NDOTO ULIYOOTA AU MAONO ULIYOYAONA

1.      Muombe Mungu akujulishe tafsiri ya ndoto uliyoota au maono uliyoyaona.

(Danieli 8:14-15)

Danieli alipoona maono ambayo hakuyaelewa alimuomba Mungu amjulishe maana ya maono yale aliyoyaona, Mungu alimjulisha maana ya maono yale.

 

2.      Mueleze au msimulie mtumishi wa Mungu ndoto yako au maono yako.

(Mwanzo 41:14-37)

Mfalme Farao alimuhadithia mtumishi wa Mungu Yusufu ile ndoto aliyoota, mtumishi wa Mungu Yusufu akamtafsiria ile ndoto.

 

NB: Watumishi wa Mungu wanaweza kumuomba Mungu na Mungu akawajulisha tafsiri ya maono uliyoona na ndoto ulioota.

 

(Danieli 2:17-46)

Mfalme Nebukadneza aliwahi kuota ndoto lakini akaisahau ile ndoto baada ya wachawi, waganga, wakaldayo na wanajimu kushindwa kumtafsiria ile ndoto aliamua kuwaua wenye hekima wote wa Babeli, Danieli alimwomba Mfalme ampe muda naye atamjulisha tafsiri ya ile ndoto.

 

Baada ya Danieli kutoka mbele ya Mfalme, Danieli aliwapa taarifa wenzake ili wamuombe Mungu awajulishe ile ndoto na tafsiri yake, Mungu alimjulisha mtumishi wake Danieli ile ndoto na tafsiri yake.

 

àUkiota ndoto au ukiona maono ambayo haufahamu maana yake hebu waone watumishi wa Mungu uwaelezee, Mungu atawatumia watumishi wake kukupa tafsiri.

 

3.      Jenga tabia ya kusoma neno la Mungu (Biblia) mara kwa mara au mara nyingi (weka neno la Mungu kwa wingi moyoni mwako).

(Wakolosai 3:16)

Neno la Mungu linapokaa kwa wingi moyoni mwako ni rahisi kupata tafsiri ya maono na ndoto unazoziota.

Chapisha Maoni

0 Maoni