(2 Wakorintho 10-3-5)
UTANGULIZI
Wazo ni nini?
Wazo ni neno lililomo ndani ya moyo wa Mungu, shetani au mwanadamu.
Kuwaza ni kuzungumza moyoni.
Mungu ana mawazo yake (Isaya 55:8) pia shetani ana mawazo yake (2 Wakorintho 10:3-5), Mungu huwapa wanadamu mawazo yake kwa sababu mbalimbali pia shetani huwapa wanadamu mawazo kwa lengo la kuwaharibu na kuwaangamiza kabisa.
Vita vya kiroho vya mawazo hivi ni vita vya kila siku ambavyo kila mtu anapaswa kupigana kila siku.
BAADHI YA MAMBO UNAYOPASWA KUFAHAMU KUHUSU MAWAZO YA SHETANI
a). Shetani anapompa mtu wazo anakusudia kuona mtu huyo anaharibikiwa au kuangamia kabisa au wazo hilo liwe sababu yaw engine kuharibikiwa au kuangamia kabisa.
(Matendo ya mitume 5:1-10) Shetani alimpa wazo Anania, Anania akamshirikisha mkewe lile wazo wakalitendea kazi hatimaye wote walikufa.
b). Msongo wa mawazo ni mojawapo ya silaha ya shetani ya kuharibu na kuangamiza maisha ya watu ndio maana kuna watu wamepatwa na magonjwa mbalimbali kwa sababu ya msongo wa mawazo, kuna watu wamejikuta wanadhoofika kwasababu ya msongo wa mawazo, kuna watu wamejiua kwa sababu ya msongo wa mawazo.
Wengine wanapokuwa na msongo wa mawazo huwa wanakunywa pombe ili kuondoa mawazo lakini baada ya nguvu ya pombe kuisha wanajikuta bado msongo wa mawazo uko palepale, wengine huwa wanameza dawa za usingizi ili wapate usingizi wasiwe na mawazo lakini baada ya kutoka usingizini wanajikuta bado wana msongo wa mawazo.
Unachopaswa kujua ni kwamba hii ni vita ya kiroho huwezi kuishinda kwa mbinu za kimwili utaumia.
(Mathayo 15:17-20) Mawazo mabaya hutoka kwa shetani , mawazo mabaya ni mawazo yote yanakinzana na neno la Mungu.
c). Hata kama umeokoka (umemwamini na kukiri kwa Yesu ni Bwana) haimzuii shetani kukupa mawazo yake (Matendo ya mitume 5:1-10) Anania na mkewe walikuwa wameokoka lakini shetani alimpa Anania wazo lililomuua yeye na mkewe.
d). Mawazo ya shetani yanalenga kumtia mtu unajisi (Mathayo 15:17-20)
BAADHI YA MBINU ZA KUSHINDA VITA AMBAVYO SHETANI ANATUMIA MAWAZO KAMA SILAHA
a). Weka neno la Mungu kwa wingi ndani yako.
(Waebrania 4:12) Neno la Mungu li jepesi kuyatambua mawazo yaliyomo moyoni mwa mtu, ukiwa na neno la Mungu litakusaidia kuyatambua mawazo ya Mungu na mawazo yasiyotoka kwa Mungu.
b). Yajue mapenzi ya Mungu.
(Mathayo 16:21-23) Yesu alijua mapenzi ya Mungu yalikuwa yeye afe msalabani ili kuwaokoa wanadamu, Petro alipotoa mawazo yaliyo kinyume na mapenzi ya Mungu, Yesu alijua kabisa hayo mawazo ya Petro hayajatoka kwa Mungu.
d). Jizoeze kuutakasa moyo wako kwa damu ya Yesu na kuangusha mawazo yoyote ambayo yameingia moyoni mwako ambayo yametoka kwa shetani (2 Wakorintho 10:5)
e). Samehe waliokukosea.
Kutokusamehe husababisha uchungu kukaa moyoni, uchungu ukikaa moyoni unamfanya shetani kupata nafasi ya kumjaza mtu mawazo ya aina mbalimbali ikiwemo kulipa kisasi nakadhalika.
(Waefeso 4:26) Biblia inasema jua lisizame kabla haujaondoa uchungu moyoni, kusamehe ni mbinu ya kuondoa uchungu moyoni.
f). Fahamu kuwa ulikuja duniani bila kitu na utaondoka bila kitu.
Mara nyingi yanapotokea mambo mabaya kama vile kupata hasara, kupoteza mali nakadhalika watu wengi hujikuta wamenaswa na ibilisi katika mawazo, ibilisi huwapa watu mawazo mengi sana hatimaye wengine huona kana kwamba hakuna haja ya kuendelea kuishi.
(Ayubu 1:20-22) Ayubu alipatwa na mambo mabaya sana ikiwemo kupoteza mali zote lakini alisema “nilitoka tumboni niko uchi”
Ni muhimu ujue kuwa kama ulitoka tumboni hauna mali, hauna mke wala mume, hauna mtoto vivyo hivyo ukiondoka duniani kila kitu utakiacha hivyo basi unapopoteza usijidhuru kutokana na msongo wa mawazo wala usimpe ibilisi nafasi kupitia mawazo.
Biblia inasema Ayubu hakumuwazia Mungu kwa upumbavu (Ayubu 1:22)
g). Ukijikuta una msongo wa mawazo na haujui cha kufanya tafuta watumishi wa Mungu wakusaidie na ufungue moyo wako kwa kuwaambia yaliyomo moyoni.
(Zaburi 39:2-3) Daudi anatueleza kuwa mawazo yaliyokuwa moyoni mwake yalifanya moyo wake ukawa mzito na alipokuwa akiwaza alisikia moto unawaka ndani yake na hakumwambia mtu yeyote hatimaye maumivu yalizidi.
Hiyo hali inawakuta watu wengi sana, wengi wanapokuwa na mawazo wanajikuta wana maumivu kwenye mioyo, mioyo inakuwa mizito wengine hujikuta wamepatwa na magonjwa mbalimbali kutokana na msongo wa mawazo.
Hivyo basi unapokuwa na msongo wa mawazo tafuta mtumishi au watumishi wa Mungu waeleze yaliyomo moyoni mwako wakusaidie, usikae na vitu moyoni vikakuumiza.
0 Maoni