Mwl. Faraja Gasto ✍️✍️✍️
(Mathayo 6:10)
SEHEMU TATU ZA SOMO HILI
✓Kuyajua mapenzi ya Mungu.
✓Namna Mungu anavyowajulisha watu mapenzi yake.
✓Kuyatenda mapenzi ya Mungu.
UTANGULIZI
Mapenzi ya Mungu ni nini?
Mapenzi ya Mungu ni matakwa ya Mungu.
Mapenzi ya Mungu ni yale ambayo Mungu anayataka.
Mungu anataka mapenzi yake yatimizwe kama yanavyotimizwa huko mbinguni, mbinguni ni mahali pa Amani, furaha pia ni mahali panapovutia kwa kuwa mapenzi ya Mungu yanatimizwa yaani yanayofanyika huko ni yale ambayo Mungu anayataka tu.
Mungu anataka mapenzi yake yatimizwe katika maisha ya mtu mmojammoja, katika eneo fulani, familia, katika jamii, katika kanisa na katika taifa.
Mungu ana mapenzi yake kwenye mambo mbalimbali , katika kuchagua viongozi Mungu anayo mapenzi yake ana mtu anayemtaka yeye, katika kuoa na kuolewa Mungu ana mapenzi yake, katika kufanya kazi Mungu anayo mapenzi yake kuhusu nini ufanye nakadhalika. Mara nyingi mapenzi ya Mungu huwa sio mapenzi yetu ndio maana Mungu anataka mapenzi yake yatimizwe.
Kwa mfano kama Mungu angemruhusu Nabii Samweli achague mtu anayemtaka awe Mfalme Daudi asingechaguliwa ila Daudi alichaguliwa kwa mapenzi ya Mungu sio mapenzi ya Nabii Samweli (1 Samweli 16:4-12)
Kama Mungu angemruhusu Yesu achague njia ya kuwakomboa wanadamu Yesu asingechagua kufa msalabani kwa kuwa yeye mwenyewe aliomba kikombe kile kimuepuke ila alikubali kufa msalabani kwa kuwa hayo ndio yalikuwa mapenzi ya Mungu (Marako 14:32-36)
Kama Yesu angelishirikisha kanisa katika maamuzi kuhusu nini afanye kwa ajili ya Sauli aliyekuwa analitesa kanisa, naamini kanisa lingemwambia Yesu amuue Sauli kwa kuwa analiharibu kanisa lakini mapenzi ya Mungu ilikuwa sio kumuua Sauli bali kumuokoa awe mtumishi wa Mungu (Matendo ya Mitume 9:1-6)
Ndio maana Mungu anataka mapenzi yake yatimizwe, tuyatende mapenzi yake pia tuombe sawasawa na mapenzi yake (1 Yohana 5:14)
Bwana wetu Yesu Kristo aliyatenda mapenzi ya Baba yake, aliomba sawasawa na mapenzi ya Baba yake pia aliyaita mapenzi ya Baba yake ndio chakula (Yohana 4:31-34)
SEHEMU YA 1: KUYAJUA MAPENZI YA MUNGU
Ili uweze kuyatenda mapenzi ya Mungu lazima kwanza uyajue, kuyajua mapenzi ya Mungu ndio ufunguo mmojawapo wa kuyatenda mapenzi ya Mungu.
Zifuatazo ni baadhi ya mbinu zitakazokusaidia kuyajua mapenzi ya MUngu:-
✓SOMA BIBLIA
(Danieli 9:1-3) Nabii Danieli aliyajua mapenzi ya Mungu kuhusu mji wa Yerusalemu aliposoma kitabu cha Nabii Yeremia.
Kusoma Biblia kunatusaidia sisi kuyafahamu mapenzi ya Mungu.
✓MSIKILIZE ROHO MTAKATIFU ALIYE NDANI YAKO
(Matendo ya Mitume 16:6-7) Mitume walikuwa wakiyatenda mapenzi ya Mungu kwa kuwa walikuwa wakimsikiliza Roho Mtakatifu anasema nini juu ya jambo Fulani (Matendo ya Mitume 13:1-3)
✓OMBA MUNGU AKUJULISHE MAPENZI YAKE
Watumishi wa Mungu waliokuwa kwenye maombi Mungu aliwajulisha mapenzi yake (Matendo ya Mitume 13:1-3)
SEHEMU YA 2: NAMNA MUNGU ANAVYOWAJULISHA WATU MAPENZI YAKE
Mungu huwajulisha watu mapenzi yake kwa njia mbalimbali zifuatazo ni baadhi ya njia hizo
✓Kwa njia ya ndoto
Mungu alimjulisha Yusufu mapenzi yake kwa njia ya ndoto, Mungu alimjulisha Yusufu kuwa anataka Yusufu awe mtu mkuu kuliko ndugu zake (Mwanzo 37:5-11).
✓Kwa njia ya maono (Matendo ya mitume 10-1-8)(Matendo ya Mitume 16:9-10)
Kwa njia ya neno lake (Isaya 55:11)
Unapolisoma neno la Mungu, unapolitafakari au unapolisikia unaweza ukayafahamu mapenzi ya Mungu.
✓Kwa njia ya unabii
Mungu hujulisha watu mapenzi yake kupitia unabii ndio maana Biblia inasema tusidharau unabii (1 Wathesalonike 5:20)
✓Kwa njia ya uongozi wa Roho Mtakatifu (Warumi 8:14)
Roho Mtakatifu huwaongoza watu kuyatenda mapenzi ya Mungu ya aina mbalimbali.
✓Kwa njia ya Amani ya Kristo (Wakolosai 3:15) (Walilipi 4:7)
SEHEMU 3: KUYATENDA MAPENZI YA MUNGU
Kuyatenda mapenzi ya Mungu ni jambo jepesi sana pia ni jambo gumu sana, ni jambo jepesi pale tunapokubali na kutii mapenzi ya Mungu ila ni jambo gumu sana pale tunapoifanya mioyo yetu kuwa migumu, tunaporuhusu ubinadamu ututawale au pale tunapotaka kuongozwa na akili zetu au maoni ya watu.
Kwa mfano Mfalme Sauli alishindwa kuyatenda mapenzi ya Mungu kwa kuwa alisikiliza maoni ya watu (1 Samweli 15:24)
Adamu alishindwa kuyatenda mapenzi ya Mungu kwa kuwa alimsikiliza mkewe (Mwanzo 3:17)
Hivyo basi ili uweze kuyatenda mapenzi ya Mungu lazima uepuke mambo yafuatayo;-
Usitawaliwe na ubanadamu wako
Epuka kusikiliza maoni ya watu hata kama unawaheshimu sikiliza maoni ya Mungu
Epuka sana kutazama mambo ya nje, Nabii Samweli alitazama kwa macho ya kibinadamu akaanza kuendeshwa na akili zake katika kuchagua Mfalme lakini Mungu alimwambia usitazame mambo ya nje kwa kuwa mimi natazama moyo wa mtu (1 Samweli 16:6-10)
HITIMISHO
Mungu anataka tuyatende mapenzi yake kama jinsi mbinguni yanavyotimizwa mapenzi yake, yaani mapenzi ya Mungu ndio yatawale katika kila jambo, hivyo basi tutake kuyajua mapenzi ya Mungu katika kila jambo na kuyatenda mapenzi hayo.
0 Maoni