✍️Faraja Gasto
LENGO LA SOMO: Ili unufaike au ufaidike na uwepo wa Mungu.
UTANGULIZI
Watu wengi wamekuwa hawanufaiki na uwepo wa Mungu kutokana na makosa mbalimbali ambayo wamekuwa wakiyafanya wakati wanapokuwa kwenye uwepo wa Mungu.
Uwepo wa Mungu unaweza kuwepo lakini watu wasinufaike na uwepo wake kutokana na sababu mbalimbali. Yakobo alisema "Mungu yupo hapa nami sikujua" (Mwanzo 28:16).
BAADHI YA MAKOSA AMBAYO WATU HUFANYA WANAPOKUWA KWENYE UWEPO WA MUNGU
✓KUTOTULIA KATIKA UWEPO WA MUNGU
(Luka 10:38-42)
Watu wengi wako kama Martha, hawanufaiki na uwepo wa Mungu kwa sababu ya kutokutulia au kuhangaika na mambo mengi wanapokuwa kwenye uwepo wa Mungu.
Wengine huhangaika na simu, kunyonyesha watoto, kuwaza wakitoka ibadani watakula nini, biashara zao zitaendaje KUTOKANA NA KUKOSA UTULIVU WENGI HAWAFAIDIKI NA UWEPO WA MUNGU
Kilichomsaidia Mariamu kunufaika na uwepo wa Yesu ni kutulia miguuni pake na katika kutulia akapata neno la Yesu.
(Zaburi 27:4)
Daudi alisema neno moja nimelitaka nalo ndilo nitalitafuta "nikae nyumbani mwa Bwana sikuzote"
✓KUHUKUMU WENGINE NA KUDHARAU WENGINE
Farisayo akiwa katika uwepo wa Mungu alianza kumuhukumu mtoza ushuru kuwa ni mwenye dhambi. (Luka 18:9-14). Yule Farisayo aliondoka kwenye uwepo wa Mungu hajapata chochote lakini yule mtoza ushuru aliondoka amehesabiwa haki.
Daudi alipokuwa katika uwepo wa Mungu anacheza, mkewe alimdharau Daudi akasema maneno ya dhihaka.
Wakati Hana alipokuwa katika uwepo wa Mungu ameumimina moyo wake kwa Bwana, Kuhani Eli alidhani Hana amelewa akamwambia "achana na pombe" (1 Samweli 1:9-17), kauli ya Eli ilikuwa na dharau ndani yake ndio maana Hana alijibu "Usimdhanie mjakazi wako kuwa ni mwanamke asiyefaa kitu" (1 Samweli 1:16)
(2 Samweli 6:16-23)
Sanduku la agano liliwakilisha uwepo wa Mungu, Sanduku la agano liliporudishwa Daudi alicheza sana lakini mkewe alimdharau Daudi.
Ni sawa na kusema kwamba wote walikuwa kwenye uwepo wa Mungu lakini Mikali hakufaidika na uwepo ule badala yake akamdharau Daudi.
Vivyo hivyo watu wengi wako kama Mikali wanapowaona wengine wameimimina mioyo yao kwa Bwana huwadharau, wanapowaona wengine wanamchezea Bwana huwadharau, kutokana na dharau huwa hawanufaiki na uwepo wa Mungu.
✓KUMZIMISHA ROHO MTAKATIFU
(1 Wathesalonike 5:19)
Wengine katika uwepo wa Mungu hujisikia kuomba lakini hawaombi, wengine huanza kutokwa machozi lakini wanajizuia, wengine hujisikia kupiga magoti lakini hawapigi, wengine hujisikia kunena kwa lugha lakini wanajizuia, wengine hujisikia kutoa sadaka lakini huwa wanaacha kutoa.
✓KUTOJIUNGANISHA NA UWEPO WA MUNGU
Mungu ni Roho, yuko katika roho kwa hiyo ili unufaike na uwepo wake lazima ujiunganishe na uwepo wake.
Baadhi ya mbinu za kujiunganisha na uwepo wa Mungu
*Lazima uamini kwamba Mungu yupo hapo ulipo (Waebrania 11:6)
*Kusifu na kuabudu (2 Mambo ya Nyakati 5:12-14)
*Maombi (Mwanzo 28:16-22)
Uwepo wa Mungu aliouona Yakobo alijiunganisha nao kwa maombi, ndio maana wakati Mungu alipomwambia Yakobo arudi kwao Mungu alimwambia "mimi ni Mungu wa kule Betheli ulikotia mafuta" (Mwanzo 31:13) . Maana yake ni kwamba Mungu alimwambia Yakobo "Mimi ni Mungu yule uliyeniomba ulipokuwa Betheli"
Yakobo alijiunganisha na ule uwepo wa Mungu kupitia maombi alipokuwa Betheli.
✓KUMPA IBILISI NAFASI
(Ayubu 1:6)
Shetani huwa ana tabia ya kukaribia pale watu wanapokuwa kwenye uwepo wa Mungu.
Biblia inasema huwa anakuja kwa nia ya kuua, kuiba na kuharibu (Yohana 10:10)
Namna gani watu wanampa nafasi wanapokuwa kwenye uwepo wa Mungu
*Kuruhusu mawazo ya shetani yaingie ndani ya mioyo yao.
*Kulala makanisani wakati ibada zikiendelea.
*N.k
HITIMISHO
Katika uwepo wa Mungu kuna mambo mengi ambayo mtu anaweza kuyapata endapo ataepuka makosa hayo niliyoeleza na mengine yanayoelezwa ndani ya Biblia.
Mungu akusaidie kutembea katika maarifa ili ufaidike na uwepo wa Mungu.
0 Maoni