KUWAOMBEA WATU WANAOGUSA MAISHA YAKO


Faraja Gasto ✍️


UTANGULIZI

Biblia imeweka wazi kuwa sisi hatujui kuomba itupasavyo au kuomba kama jinsi tunavyopaswa kuomba (Warumi 8:26)


Kila mmoja anapaswa kufahamu kuwa kila mtu amebeba hatima ya maisha ya watu wengine, kwa hiyo kuna watu wako nyuma yako wanategemea sana uwepo wako, mafanikio yako nakadhalika.


Kwa mfano mama mjamzito amebeba maisha ya mtoto aliyeko tumboni huyu mama anaweza kuamua kuua mtoto kwa kuwa maisha ya mtoto huyo yako mikononi mwake, pia mtoto aliyeko tumboni amebeba Maisha ya mama yake ndio maana ikitokea mtoto akakaa vibaya tumboni lazima mama apate matatizo.


MIFANO YA WATU WALIOBEBA HATIMA YA MAISHA YA WATU WENGINE


✓ MUSA

Mungu alimuagiza Musa awatoe waisraeli utumwani, kwa hiyo kutoka kwa wana wa Israeli kulitegemea sana uwepo na ujasiri wa Musa (Kutoka 3:1-10)


✓YOSHUA

Mungu alimwambia Yoshua "ni Wewe utakayewafikisha watu hawa katika nchi ya Kanaani" , kwa hiyo ili waisraeli wafike Kanaani walitegemea sana uwepo na ujasiri wa Yoshua (Yoshua 1:1-7)


✓YESU KRISTO

Ukombozi wa wanadamu ulitegemea sana uwepo wa Yesu Kristo na utii wake kwa Mungu BABA yake (Warumi 5:17-19)


✓YONA

Usalama wa mji wa Ninawi ulitegemea sana utii wa Yona kwa kuwa Yona aliambiwa baada ya siku arobaini mji utaangamizwa (Yona 3:1-10), Kama Yona asingefika Ninawi ndani ya siku zile arobaini ukweli ni kwamba mji Ninawi ungeangamizwa kwa kuwa Yona ndiye alipewa ujumbe wa kuwaambia watubu la sivyo baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa.


YUSUFU

Yusufu alipokuwa Gerezani alimwambia mfungwa mwenzie ukitoka usinisahau (Mwanzo 40:14) lakini yule mtu akamsahau kabisa Yusufu.


Kutoka kwa Yusufu Gerezani kulitegemea Sana yule mtu kumkumbuka Yusufu ndio maana baada ya Mfalme Farao kuota ndoto na akakosekana mtafsiri, yule Jamaa akakumbuka kuna mtu gerezani anaweza kutafsiri ndoto ndipo Yusufu akaletwa kutafsiri hatimaye akatolewa Gerezani.


✓WAPELELEZI

Wapelelezi walipotumwa na Musa, taifa liliwategemea kuleta taarifa zitakazosaidia wao kufika Kanaani lakini waliporudi walikuja na taarifa mbaya zilizopelekea wana wa Israeli kuuawa (Hesabu 13:32-33, 14:26-33)


Kosa walilofanya wapelelezi kumi lilipelekea waisraeli wengi kufa.


✓MTUME PETRO

Uimara wa mitume wengine ulutegemea Sana uimara wa Petro ndio maana Yesu alimuombea Petro maombi maalumu kwamba "imani yake isitindike ili atakapoongoka awaimarishe ndugu zake" (Luka 22:32)


MAMBO YA KUWAOMBEA WATU HAO


✓Waombee ujasiri wa kuyatenda mapenzi ya Mungu bila hofu au waombee Mungu awape ujasiri wa kutenda yale anayotaka wayatende.


Laiti kama Musa angekosa ujasiri wa kwenda kwa Mfalme Farao basi waisraeli wangeendelea kukaa nchini Misri.


Laiti kama Yesu Kristo angekosa ujasiri wa kwenda kufia msalabani huu wokovu tusingekuwa nao (tusingepata wokovu)


✓Waombee wakumbuke wanayopaswa kuyakumbuka.


(Mwanzo  40:14,41:9)

Mkuu wa wanyweshaji alipaswa kumkumbuka Yusufu lakini akamsahau na alipomsahau Yusufu aliendelea kukaa gerezani lakini ALIPOKUMBUKA MAKOSA ALIYOFANYA AKAMKUMBUKA YUSUFU, 

 kumbukumbu hizo ndizo ziliepelekea Yusufu akatoka Gerezani.


✓Waombee Mungu awainue

Kwa mfano Danieli alipoinuliwa aliwasaidia ndugu zake kupata kazi kwenye utawala wa Mfalme Nebukadneza (Danieli 2:48-49)


Zile kazi walizipata kwa sababu ya Danieli.


✓Waombee Mungu awaimarishe kiafya, kiuchumi, kiakili nakadhalika


 Yesu alimuombea Petro Imani yake isitindike ili atakapoongoka awaimarishe wengine kwa kuwa uimara wa wengine ulitegemea uimara wa Mtume Petro (Luka 22:32)


✓Waombee Mungu awasaidie kuepuka makosa mbalimbali 


Kwa mfano kosa mojawapo alilolifanya Yoshua ni kutoandaa mtu wa kukaa kwenye nafasi yake (Musa alimuandaa Yoshua lakini Yoshua hakuandaa mtu) kutokana na kosa hilo ndio maana kukawa na waamuzi badala ya kiongozi.


Kosa mojawapo alilofanya Yusufu ni kutowasaidia ndugu zake kupata kazi na kusoma wakati alikuwa afisa mkubwa wa Serikali ndio maana baada ya Yusufu kufa walitaabika sana kwa kuwa maisha yao yalitegemea sana uwepo wa Yusufu kwenye ile nafasi ilibidi Mungu amlete Musa ambaye alisomea hapo Misri ndio akatumiwa kuwatoa waisraeli.


HITIMISHO

Watu ambao wamebeba maisha yako unapaswa kuwaombea kama jinsi ambavyo tumeona maana wao wakitimiza wajibu wao sawasawa na mapenzi ya Mungu, kuna faida mbalimbali utazipata ikiwemo usitawi wa kiroho na kimwili nakadhalika.

Chapisha Maoni

0 Maoni