✍️Faraja Gasto
UTANGULIZI
Watu wengi wamekuwa wanapata shida kuelewa Biblia pindi wanapoisoma, kutokana na kutokuielewa watu wengi wamekuwa sio wasomaji wa Biblia na wengine wamekuwa wanadai Biblia inajipinga yenyewe, mambo hayo yanatokana na kutokuielewa Biblia.
Kila mmoja anapaswa kufahamu kuwa mapenzi ya Mungu ni kuona watu wake wanaelewa ujumbe uliomo ndani ya Biblia.
Kutokuelewa huwa kunampa nafasi shetani ya kunyakua ufahamu uliongia ndani ya mtu (Mathayo 13:19)
AINA TATU ZA MBINU ZITAKAZOKUSAIDIA
✓ TAFUTA MTU WA KUKUFUNDISHA AMBACHO HAUJAKIELEWA AU MTU WA KUMUULIZA AMBACHO HAUJAELEWA
(Matendo ya mitume 8:31-35)
Katika andiko hilo tunaona habari ya towashi ambaye alikuwa anasoma kitabu cha Nabii Isaya na hakuwa anaelewa habari iliyoandikwa katika fungu alilokuwa anasoma lilikuwa linamhusu nani.
Filipo alipomuuliza je! umeelewa hayo unayoyasoma? yule mtu alikiri kwamba haelewi ndipo akamuomba Filipo amfundishe.
Filipo alipomfundisha ndipo akaelewa hatimaye akamwamini Bwana Yesu.
✓ MUOMBE MUNGU AFUNGUE AKILI ZAKO AU AZITIE NURU AKILI ZAKO UPATE KUELEWA MAANDIKO
Yesu alipokuwa akizungumza na wanafunzi wake aliwafunulia akili zao wapate kuelewa maandiko (Luka 24:45)
Alipowafunulia akili zao ili waelewe maandiko walianza kuyaelewa vizuri maneno ya Yesu.
Biblia imeweka wazi kuwa akili zinaweza kutiwa giza (Waefeso 4:18) jambo mojawapo linalotokea akili za mtu zikitiwa giza ni kwamba mtu anakuwa haelewi anachojifunza au anachofundishwa.
Kila mmoja anapaswa kufahamu kuwa Biblia ni kitabu kinachofundisha mambo mengi ikiwemo ya kiroho Kwa hiyo unahitaji msaada wa Mungu ili ukielewe.
✓ SOMA ANDIKO LOTE AU SOMA MWANZO WA SURA
Sio vema kusoma mistari michache bila kuanza mwanzo wa sura ndio maana wengine huwa wanaita sura za vitabu ni milango, unaposoma maandiko aanzia mlangoni kwa mfano kama unasoma kitabu cha Mathayo sura ya Saba mstari wa saba ni vema kuanzia mstari wa kwanza itakusaidia sana katika usomaji na kuyaelewa maandiko.
Tabia ya kunyofoa baadhi ya vifungu sio nzuri kiusomaji.
HITIMISHO
Ili uwe msomaji wa Biblia unayeelewa au ili uelewe pale unaposikia ujumbe uliomo ndani ya Biblia ni vema uzingatie mbinu hizo chache za msingi.
0 Maoni