HEKIMA KAMA KIFAA CHA UOKOZI


 ✍️ Faraja Gasto


UTANGULIZI

Hapa duniani kuna aina nyingi sana za vifaa vya uokozi (vinavyotumiwa katika kuokoa) baadhi ya vifaa hivyo ni mtungi wa kuzimia moto (fire extinguisher), boya (buoy), mitungi ya gesi ya oksijeni (gas cylinders), jaketi la maisha (life jacket) na kamba (string).


Pia katika ulimwengu wa roho kuna aina mbalimbali za vifaa vinavyotambuliwa kama vifaa vya uokozi, kifaa kimojawapo ni HEKIMA.


MIFANO YA KIBIBLIA INAYOTUSAIDIA KUFAHAMU HEKIMA KAMA KIFAA CHA UOKOZI


MFANO WA 1: HEKIMA ILIVYOOKOA MJI


(Mhubiri 9:13-15)

Biblia inaeleza habari ya mji uliokusudiwa kushambuliwa lakini hekima ya mtu mmoja aliyekuwa ndani ya ule mji ilitosha kuuokoa mji ule.


Kutokana na hekima ile mji ukabaki salama hivyo basi kila mmoja anapaswa kufahamu kuwa hekima ni kifaa cha uokozi (hekima inaweza kumuokoa mtu, kuokoa taasisi, kuokoa uzao, kuokoa biashara, kuokoa nchi nakadhalika).


"hekima ni bora kuliko silaha za vita" (Mhubiri 9:18a)


MFANO WA 2: HEKIMA YA YESU ILIVYOMUOKOA MWANAMKE ASIUAWE


(Yohana 8:2-11)

Yesu alipokuwa hekaluni akaletwa mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, kwa mujibu wa torati ilikuwa mwanamke akifumaniwa katika uzinzi alipaswa kuuawa.


Wale washitaki walitaka kusikia Yesu anasemaje kuhusu jambo lile, Yesu aliwaambia "asiye na dhambi awe wa kwanza kumtupia jiwe huyu mwanamke" waliposikia neno hilo (neno la hekima) wakashitakiwa na dhamiri zao wakaamua kuondoka zao.


Hekima ya Yesu ilimuokoa yule mwanamke asiuawe. 


MFANO WA 3: HEKIMA ILIVYOIOKOA NCHI YA MISRI DHIDI YA MIAKA SABA YA NJAA 


(Mwanzo 41:1-7)

Mungu alimjulisha Mfalme Farao mambo yajayo yaani ujio wa miaka saba ya shibe na miaka saba ya njaa japo Mfalme Farao hakuelewa ndoto ile.


Alipopatikana mtu (Yusufu) wa kutafsiri ile ndoto, Yusufu alimwambia Mfalme atafute mtu mwenye akili na hekima (Mwanzo 41:33)


Hekima aliyokuwa nayo Yusufu iliiokoa nchi dhidi ya njaa ya miaka saba, nchi ya Misri ndio nchi pekee ambayo haikuathirika na ile njaa ya miaka saba.


MFANO WA 4: HEKIMA INAYOMUOKOA CHUNGU DHIDI YA NJAA 


(Mithali 6:6-8)

Biblia inaeleza habari za mdudu aitwaye chungu, Biblia inaeleza jinsi hekima inavyomsaidia kuweka akiba ya chakula wakati kinapopatikana ili wakati ambao chakula kitakuwa hakipatikani awe na chakula kwa kuwa aliweka akiba.


Hekima hiyo ndio hekima inayomuokoa chungu ili asije kuathirika na njaa wakati ambao chakula hakipatikani.


HITIMISHO

Hiyo ni baadhi ya mifano ya namna hekima inaweza kuokoa, hekima inaweza kuokoa mtu dhidi ya hatari nakadhalika, hekima inaweza kuokoa nchi, hekima inaweza kuokoa taasisi nakadhalika.

Chapisha Maoni

0 Maoni