UTANGULIZI
Hapa duniani kuna aina nyingi sana za vifaa vya uokozi (vinavyotumiwa katika kuokoa) baadhi ya vifaa hivyo ni mtungi wa kuzimia moto (fire extinguisher), boya (buoy), mitungi ya gesi ya oksijeni (gas cylinders), jaketi la maisha (life jacket) na kamba (string).
Pia katika ulimwengu wa roho kuna aina mbalimbali za vifaa vinavyotambuliwa kama vifaa vya uokozi, kifaa kimojawapo ni UNYENYEKEVU (KUJISHUSHA)
Unyenyekevu unaweza kuokoa watu, vitu nakadhalika.
MIFANO YA KIBIBLIA INAYOTUPA KUFAHAMU UNYENYEKEVU KAMA KIFAA CHA UOKOZI
MFANO WA 1: UNYENYEKEVU UNAVYOWEZA KUMUOKOA MTU NA MITEGO NAKADHALIKA.
(Mithali 6:1-5)
Biblia inaeleza habari ya mtu ambaye alikubali kuwa mdhamini wa rafiki yake (yaani ni sawa na mtu ambaye amekubali kumdhamini rafiki yake ili achukue mkopo Benki au amemdhamini rafiki yake ili Polisi wamuachie lakini imefika hatua mdhamini amejikuta hatiani kutegemeana na masharti ya dhamana na haujui cha kufanya)
Sasa huyu mtu anapewa ushauri kwamba ili ajiokoe na matokeo ya hatia ile INAMPASA KUNYENYEKEA.
Soma mfano huu ili unielewe vizuri, kwa mfano unamdai mtu lakini badala ya kukujibu vizuri kuhusu deni anakujibu vibaya "silipi deni" au "fanya utakalo" lazima utajisikia vibaya na unaweza kufanya maamuzi ya kumfikisha mtu huyo kwenye vyombo vya sheria, sheria inaweza kuamuru uchukue vitu vyake ili kufidia deni au kuuza vitu vyake ili alipe deni.
Kitakachokuwa kimemponza mtu huyo sio deni bali ni kukosa unyenyekevu, kwa kuwa alikosa unyenyekevu ndio maana aliaibika.
Ndivyo ilivyo kuhusu unyenyekevu, unyenyekevu unaweza kumuokoa mtu dhidi ya aibu nakadhalika.
MFANO WA 2: UNYENYEKEVU WA ABIGAILI ULIVYOMUOKOA MUMEWE ASIUAWE, ULIVYOWAOKOA WATU WAKE WASIUAWE NA ULIVYOOKOA MALI ZAO ZISIANGAMIZWE.
(1 Samweli 25:1-33)
Daudi alimtendea mema Nabali pasipo Nabali kujua, ulifika wakati Daudi akahitaji kutendewa mema na Nabali lakini Nabali hakutenda Wema, Daudi aliamua kumuangamiza Nabali na familia yake, vitu vyake vyote na watu watumishi wake wote.
Lakini Abigaili alipopata taarifa za ujio wa Daudi na nia ya Daudi ya kufanya maangamizo, Abigaili alikwenda kumlaki Daudi kwa unyenyekevu.
Daudi alipouona unyenyekevu wa Abigaili alighairi mpango wa kuangamiza, unyenyekevu wa Abigaili ndio ulimuokoa Nabali, watumishi wake na Mali zao.
MFANO WA 3: UNYENYEKEVU ULIVYOWAOKOA MAASKARI WA MFALME AHAZIA WASIUAWE
(2 Wafalme 1:9-15)
Baada ya Mfalme Ahazia kuambiwa atakufa, alituma maaskari 51 kwa Nabii Eliya, walikwenda kwa Nabii Eliya kwa kiburi cha uaskari wao moto ukashuka kutoka mbinguni ukawateketeza.
Mfalme akatuma maaskari wengine 51 nao wakafa kwa moto kwa kuwa walikwenda kwa mtumishi wa Mungu bila unyenyekevu.
Lakini Mfalme alipotuma maaskari wengine walipofika kwa mtumishi wa Mungu, yule kiongozi wa maaskari hao alijinyenyekeza ndipo Mungu alimwambia Nabii Eliya aende pamoja naye.
NB: Kilichowaponza wale maaskari wa kundi la kwanza na la pili ni kukosa unyenyekevu lakini kilichowaokoa wale maaskari wa kundi la tatu ni unyenyekevu wa kiongozi wao.
HITIMISHO
Tumeona namna unyenyekevu unavyoweza kuokoa watu na kuwaepusha na mambo mbalimbali hivyo basi Kila mmoja anapaswa kujifunga unyenyekevu kwa kuwa unyenyekevu unaweza kukuokoa na mambo mbalimbali, unyenyekevu wako unaweza kuokoa wengine, unyenyekevu unaweza kuokoa mali zako kama jinsi unyenyekevu wa Abigaili ulivyookoa mali zao.
0 Maoni