Utangulizi
UFUNUO NI NINI?
Baadhi ya maana za ufunuo
1.Ufunuo ni mambo ya siri yaliyowekwa wazi na Mungu.
2.Ufunuo ni ufahamu unaoletwa na Mungu kuhusu wa mambo ya siri au mambo yaliyofichwa.
Mungu huwafunulia watu mambo mbalimbali ya kiroho, ya kiuchumi nakadhalika, Mungu huwafunulia watu mbinu, ujuzi, nyimbo, siri nakadhalika, soma baadhi ya mifano ifuatayo:-
Mungu hawezi kufanya neno lolote bila kuwafunulia watumishi wake (Amosi 3:7)
Mtume Paulo alifunuliwa mambo mbalimbali (Wagalatia 2:1-2)(2 Wakorintho 12:7)
Mtume Petro alifunuliwa (Mathayo 16:17)
Mtume Yohana alifunuliwa (Ufunuo wa Yohana 1:1)
Nabii Danieli alifunuliwa (Danieli 2:19)
BAADHI YA MADHARA YA KUKOSA UFUNUO
1.Mambo mengi hayaendi vizuri kwa kuwa watu wamekosa ufunuo.
2.Huduma nyingi au makanisa mengi yameshindwa kupiga hatua au kuendelea kwa sababu ya kukosa ufunuo.
3.Biashara nyingi zimekufa kwa sababu ya kukosekana kwa ufunuo.
4.Familia nyingi zimejikuta kwenye mnyonyororo wa matatizo kwa sababu ya kukosekana kwa ufunuo.
5.Miradi mingi imekufa kwa sababu ya kukosekana kwa ufunuo.
6.Shetani amefanikiwa kuwashinda watu mbalimbali kwa sababu ya kukosekana kwa ufunuo.
7.Watu wengi wamejikuta kwenye hatari mbalimbali kwa sababu ya kukosa ufunuo.
UMUHIMU WA KUPATA UFUNUO KUTOKA KWA MUNGU
1.Ufunuo unatuwezesha kumshinda shetani.
(Matendo ya mitume 13:6-12)
Mtume Paulo alifunuliwa kinachosababisha liwali Sergio Paulo asimwamini Yesu ni mchawi, Mtume Paulo akamshughulikia yule mchawi hatimaye Sergio Paulo akamwamini Yesu akiyastaajiabia mafundisho ya Bwana Yesu.
Ufunuo ulimsaidia Mtume Paulo kushinda hila za Ibilisi kupitia Elima mchawi.
2. Ufunuo unatuwezesha kupanua mipaka ya kihuduma.
(Matendo ya mitume 10:9-16)
Mtume Petro alikuwa hana mpango wa kwenda kuhubiri injili Kwa watu wa mataifa (wasio wa Israeli) lakini alipopata ufunuo kuhusu mataifa alichukua hatua kwenda kuhubiri kwa wasio wayahudi hatimaye watu wakamwamini Yesu.
Mipaka ya huduma ya Mtume Paulo ilipanuka baada ya kupata ufunuo.
3. Ufunuo unaleta upatanisho (mapatano)
(Mwanzo 32:13)
Baada ya Yakobo kuwasilisha maombi yake kwa Mungu, usiku huohuo Yakobo alipata ufunuo wa kupeleka zawadi kwa Esau, zile zawadi zilitengeneza mtazamo mpya ndani ya Esau hatimaye Esau alilainika akawa tayari kupatana na ndugu yake (Yakobo).
Ufunuo alioupata Yakobo ulileta mapatano kati yake na ndugu yake (Esau).
4.Ufunuo unaleta majibu ya maswali mbalimbali.
(Mathayo 16:17)
Yesu aliuliza watu husema yeye ni nani? wanafunzi wake walianza kumpa majibu mbalimbali Kisha Yesu aliwauliza na wao wanasema yeye ni nani? Petro ndiye aliyepata jibu sahihi alikuwa, ufunuo alioupata ndio ulileta jibu sahihi (Mathayo 16:15-17) ndio maana Yesu alisema "mwili na damu havikukufunulia bali BABA WA MBINGUNI NDIYE AMEKUFUNULIA"
Wapo watu wana maswali mbalimbali wengine wanajiuliza watafanikiwa lini, wataolewa lini, watapata kitu fulani lini nakadhalika.
Ufunuo unaleta majibu ya maswali mbalimbali.
5. Ufunuo unatupa kufahamu mambo ya siri kuhusu watu, mazingira nakadhalika.
Ukisoma kitabu cha Ufunuo wa Yohana utaona Yohana alipofunuliwa alifahamu mambo ya siri kuhusu makanisa Saba yaliyokuwa Asia nakadhalika.
Ukisoma kitabu cha Yohana 4:16-18 Yesu alifahamu maisha ya mwanamke msamaria kupitia ufunuo.
6. Ufunuo unatuepusha na hatari mbalimbali.
(2 Wafalme 6:8-10)
Mfalme wa Shamu alikuwa akipanga mipango mibaya dhidi ya Mfalme wa Israeli lakini ufunuo aliokuwa akiupata Nabii Elisha ulimsaidia Mfalme wa Israeli kuepuka hatari mbalimbali.
Duniani Kuna aina nyingi za hatari zinazomkabili mwanadamu, Mtume Paulo alikumbana na aina mbalimbali za hatari (2 Wakorintho 11:26), Kila mtu anakabiliwa na aina mbalimbali za hatari TUKIPATA UFUNUO KUTOKA KWA MUNGU TUTAEPUKA HATARI HIZO.
NB: Mungu huwafunulia watu kwa njia mbalimbali kama vile ndoto, mawazo, maono, kusoma na kutafakari neno la Mungu, mahubiri, unabii nakadhalika. Mtu anaweza kupata ufunuo kutoka kwa Mungu anapoomba, anaposoma na kutafakari neno la Mungu, anaposikiliza neno la Mungu kupitia mahubiri, anapomsifu na kumuabudu Mungu nakadhalika.
0 Maoni