✍ Faraja Gasto
Chanzo kikuu cha matatizo yote hapa duniani ni DHAMBI.
Chanzo cha matatizo sio wachawi, sio pepo, sio kukosa elimu, sio kukosa pesa, sio kukosa Kazi, sio kukosa mtaji nakadhalika, chanzo ni DHAMBI.
Mahali pa kuanzia kutatua matatizo au hatua ya awali ya kutatua matatizo ni TOBA AU KUTUBU.
KUTUBU NI NINI?
1. Kutubu ni kubadili misimamo (Mathayo 21:28-30)
2. Kutubu ni kuachana na chochote ambacho ni kibaya (Isaya 55:7)
- Kuachana na njia mbaya, mawazo mabaya, maisha mabaya au maisha ya uovu, kuachana na mume wa mtu, mke wa mtu, kuachana na dhuluma, kuachana na kulipa kisasi nakadhalika.
3. Kutubu ni kubadili mwenendo (Luka 15:17-20)
- Kuachana na mwenendo ulio kinyume na neno la Mungu.
4. Kutubu ni kurejea kwa Mungu kimahusiano. (Matendo ya mitume 3:19)
FAIDA CHACHE ZA TOBA
1. Kutubu kunasababisha dhambi zifutwe (Matendo ya mitume 3:19)
- Kumbuka nimekuambia dhambi ndio chanzo cha matatizo, dhambi ikifutwa mlango uliopitisha tatizo hilo unafungwa katika ulimwengu wa roho halafu Mungu anaingilia kati kufanya matengenezo, kujenga yaliyobomolewa na dhambi nakadhalika.
2. Kutubu ni mlango wa furaha au kutubu kunasababisha furaha kurudi tena.
(Matendo ya mitume 3:19)
Biblia inasema "TUBUNI basi mrejee ili dhambi zenu zifutwe ZIPATE KUJA NYAKATI ZA KUBURUDISHWA kwa kuwako kwake Bwana"
Dhambi ni mlango wa matatizo mbalimbali ikiwemo kukosa furaha au kupoteza furaha ila toba ni mlango wa furaha.
(Zaburi 51:12)
Mfalme Daudi alipotenda dhambi alikuja kugundua kuwa alipoteza furaha ya Mungu ndani yake ndio maana alipotubu aliomba hivi "UNIRUDISHIE FURAHA YA WOKOVU WAKO"
(Luka 15:11-16)
Huyu kijana alipojiingiza kwenye maisha ya uasherati alijikuta amepoteza vitu vingi ikiwemo furaha (hakuwa na furaha).
Lakini alipotubu akarejea kwa babaye alijikuta furaha imerejea tena katika maisha yake (Luka 15:22-24)
Je! umepoteza furaha? Nakufundisha siri hizi kuhusu toba ikusaidie kuondokana na tatizo la kukosa furaha.
3. Kutubu kunarejesha mahusiano kati ya mtu na mtu au kati ya mtu na Mungu.
(Luka 15:21-24)
Toba ilirejesha mahusiano kati ya baba na mtoto wake.
(Isaya 55:7)
Toba inarejesha mahusiano kati ya mtu na Mungu.
Barikiwa.
0 Maoni