UHUSIANO WA TOBA NA KUONEWA HURUMA

 

                 ✍️  Faraja Gasto


(Luka 15:16b)

"wala hapana mtu aliyempa kitu"


Chanzo kikuu cha matatizo yote ni dhambi, kutokuoneana huruma ni tatizo mojawapo lililoletwa na dhambi.


Biblia inaposema "wala hapana mtu aliyempa kitu" maana yake ni sawa na kusema "wala hapana mtu aliyemwonea huruma Katika tatizo lililompata"


Iko hivi, jambo mojawapo linalosababisha mtu amsaidie mtu mwingine ni HURUMA, huruma isipokuwepo basi kutatokea tatizo la kutosaidiana, kumbuka Mungu ni Mungu mwenye huruma (Luka 6:36) Mungu hutusaidia kupitia watu kutokana na huruma anayoweka ndani yao, huruma hiyo ndio huwasukuma watu kuwasaidia wengine.


(Luka 15:16b)

Huyu kijana alijikuta hakuna mtu aliyempa kitu kwa kuwa hakuna aliyemwonea huruma.


Jaribu kufikiri uko kwenye wakati mgumu halafu hakuna wa kukuonea huruma, unajaribu kuwaeleza watu matatizo yanayokusibu halafu unashangaa hakuna wa kukuonea huruma, USIWALAUMU WATU, wewe kumbuka toba ili upate msaada kutoka kwa Mungu.


Usidhani huyo kijana alikuwa hawaambii watu matatizo yake, alikuwa anawaambia watu lakini hakuna aliyemwonea huruma.


ONA KILICHOTOKEA ALIPOTUBU

(Luka 15:17-20)

Biblia inasema alipotubu, baba yake ALIMWONEA HURUMA.


Kutokana na huruma ya baba yake, baba aliamuru liletwe vazi lililo bora wamvike, wakamvika pete, wakamvika viatu kisha ikafanyika sherehe kubwa.


Jaribu kufikiri kama angeufanya moyo wake kuwa mgumu, jaribu kufikiri kama angebaki kuwanung'unikia ambao hawamsaidii katika tatizo lililokuwa limempata, ukweli ni kwamba yamkini angefia kule kwenye nchi ya mbali pia asingezikwa Kwa heshima.


NIKUULIZE HIVI

Je! unapitia wakati mgumu matatizo yamekuzunguka na hakuna anayekuonea huruma?


Kama jibu ni ndiyo basi fanya kama alivyofanya yule kijana, TUBU ili upate msaada wa Mungu, kutubu kutamfanya Mungu aingilie kati matatizo yaliyokupata.


Barikiwa.

Chapisha Maoni

0 Maoni