UTANGULIZI
Si watu wengi wanafahamu kuwa maombi yana
sheria zake yaani ukitaka maombi yako yajibiwe lazima ufuate sheria hizo za
maombi, ikitokea umekosea au usipofuata sheria hizo hauwezi kupata majibu ya
maombi yako hata kama utafunga na kuomba.
BAADHI YA
SHERIA ZA MAOMBI
1. Lazima uamini kwamba Mungu yupo na huwa anajibu maombi.
(Waebrania
12:6b)
“kwa maana mtu
amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale
wamtafutao.”
Kuomba bila imani ni
kupoteza muda wako kwa kuwa maombi ya bila imani hayawezi kusababisha matokeo.
2.
Tunatakiwa kuomba mambo yote kwa jina la Yesu.
(Yohana 15:16)
“Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua
ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili
kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni.”
(Yohana 16:24)
“Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi
mtapata; furaha yenu iwe timilifu.”
Maombi
yote tunayoyaomba lazima tuombe kwa jina la Yesu.
3.
Tunatakiwa kuomba sawasawa na mapenzi ya Mungu.
(Warumi 8:27)
“Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana
hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua
kusikoweza kutamkwa.”
Biblia
imeweka wazi kuwa kuna kuomba sawasawa na mapenzi ya Mungu, tunaweza kuomba
sawasawa na mapenzi ya Mungu endapo tutampa nafasi Roho Mtakatifu atuongoze
katika kuomba kwa kuwa Biblia inasema “hatujui kuomba itupasavyo” yaani hatujui
kuomba katika namna ambayo itamfanya Mungu atujibu ila Roho Mtakatifu ndiye
awezaye kutuongoza kuomba sawasawa na mapenzi ya Mungu.
Ona
kinachotokea endapo tutaomba sawasawa na mapenzi ya Mungu, soma (1 Yohana 5:15)
“Na huu ndio ujasiri
tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu
sawasawa na mapenzi yake, atusikia.”
Nini maana kuomba sawasawa na mapenzi ya Mungu?
Ni
kuomba kulingana na neno la Mungu au ni kuomba sawasawa na neno la Mungu
linavyosema kwa kuwa Mungu huwa analiangalia neno lake ili alitimize.
(Yeremia 1:11-12)
“11. Tena neno la Bwana likanijia, kusema, Yeremia, waona
nini? Nikasema, Naona ufito wa mlozi. 12. Ndipo Bwana akaniambia, Umeona vema, kwa maana ninaliangalia neno langu, ili
nilitimize.”
Kwa
hiyo ni muhimu sana kuweka kwa wingi neno la Mungu ndani yetu kwa kuwa neno la
Mungu likikaa kwa wingi ndani yetu litaboresha mfumo au mifumo yetu ya maombi.
4.
Tunatakiwa kuomba bila kukata tamaa.
(Luka 18:1)
“Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu
sikuzote, wala wasikate tamaa.”
Kuomba
bila kukata tamaa maana yake ni kuomba bila kuacha mpaka utapoona majibu
yamepatikana ndio maana Yesu alitoa mfano wa mwanamke mjane aliyekuwa akidai
haki yake mpaka akaipata ndipo akaacha kuidai.
5.
Mambo mengine hayawezekani ila kwa kuomba na kufunga ndipo yatawezekana.
(Mathayo 17:21)
Yesu
alipolitoa pepo ambalo wanafunzi wake walishindwa kulitoa aliwaambia hawakuweza
kulitoa kwa sababu
a).
Ya upungufu wa imani yao (Mathayo 17:19-20)
b).
Mambo mengine ili kuyatatua yanahitaji kuomba na kufunga (Mathayo 17:21)
HITIMISHO
Nimekuonyesha
baadhi ya sheria za maombi ili zikusaidie kukuwekea msingi mzuri ambao
utakusaidia katika maombi yako, japo ziko sheria nyingi ila nimekuonyesha hizo
chache ili kukuweka hamu ya kuzijua zingine, nakuhamasisha kulisoma neno la
Mungu (Biblia) Roho Mtakatifu atakuwa anakuwezesha kuzifahamu sheria zingine za
maombi.
0 Maoni