KUOMBA NA KUFUATILIA MATOKEO

 


UTANGULIZI

Sheria mojawapo ya maombi inasema hivi “imetupasa kumwomba Mungu sikuzote bila kukata tama” (Luka 18:1)

Maana ya kuomba bila kukata tama ni kuomba mpaka uone matokeo ya maombi yako au kuomba mpaka uone mpenyo, kuomba mpaka uone mlango au kuomba mpaka upate jibu la unachokiomba.

Tunapomuomba Mungu lazima tujenge tabia ya kufuatilia matokeo ya maombi, vivyo hivyo tunapowaombea watu ni vema tujenge tabia ya kufuatilia matokeo ya maombi yetu ili tuone kama maombi yameleta matokeo au la kwa kuwa kuomba ni kitu kingine na kupokea majibu ni kitu kingine.

BAADHI YA WATU WALIOOMBA NA KUFUATILIA MATOKEO YA MAOMBI YAO

1.      Bwana Yesu

(Marko 8:22)

22. Wakafika Bethsaida, wakamletea kipofu, wakamsihi amguse. 23. Akamshika mkono yule kipofu, akamchukua nje ya kijiji, akamtemea mate ya macho, akamwekea mikono yake, akamwuliza, Waona kitu? 24. Akatazama juu, akasema, Naona watu kama miti, inakwenda. 25. Ndipo akaweka tena mikono yake juu ya macho yake, naye akatazama sana; akawa mzima, akaona vyote waziwazi.”

 

Yesu alimtemea mate huyu kipofu kisha akamwekea mikono kisha akamuuliza unaona nini? Yule kipofu akajibu akasema anaona watu kama miti inakwenda, Biblia inasema Yesu akaweka tena mikono juu ya macho ya kipofu ghafla akapokea uponyaji akaanza kuona.

 

Ninachotaka uone hapo ni kwamba Yesu aliweka mikono huku anafuatilia kama kuna matokeo, yaani ni sawa na kusema Yesu alikuwa anamuombea kipofu huku anafuatilia kama yale maombi yamesababisha matokeo, Yesu alipoona matokeo yametokea ndipo akaacha kuomba.

 

2.      Nabii Eliya

(1 wafalme 18:41-45)

“41. Naye Eliya akamwambia Ahabu, Haya! Inuka, ule, unywe; kwani pana sauti ya mvua tele. 42. Basi Ahabu akainuka ili ale na kunywa. Naye Eliya akapanda juu mpaka kilele cha Karmeli; akasujudu kifudifudi, akainama uso mpaka magotini. 43. Akamwambia mtumishi wake, Kwea sasa, utazame upande wa bahari. Akakwea, akatazama, na kusema, Hakuna kitu. Naye akanena, Enenda tena mara saba. 44. Ikawa mara ya saba akasema, Tazama, wingu linatoka katika bahari, nalo ni dogo kama mkono wa mtu. Akanena, Enenda, umwambie Ahabu, Tandika, ushuke, mvua isikuzuie. 45. Ikawa, muda si muda, mbingu zikawa nyeusi kwa mawingu na upepo, ikanyesha mvua nyingi. Ahabu akapanda garini, akaenda zake Yezreeli.”

 

Nabii Eliya alikuwa anaomba mvua inyeshe kisha anamtuma mtumishi wake akaangalie kama maombi yake yamesababisha matokeo, Yule mtumishi akawa akimletea ripoti kuwa hakuna dalili ya mvua, Eliya aliomba mara saba, mara ya saba ndipo dalili ya mvua ikaonekana ndipo Eliya akaacha kuomba.

 

Nilichotaka uone hapo ni kwamba Nabii Eliya alikuwa anaomba huku anafuatilia kama maombi yake yamejibiwa.

 

(1 Wafalme 17:17-21)

“17. Ikawa, baada ya hayo, mwana wake yule mwanamke, bibi wa nyumba ile, akaugua; ugonjwa wake ukazidi hata akawa hana pumzi tena.18. Akamwambia Eliya, Nina nini nawe, Ee mtu wa Mungu? Je! Umenijia ili dhambi yangu ikumbukwe, ukamwue mwanangu? 19. Akamwambia, Nipe mwanao. Akamtoa katika kifua chake, akamchukua juu chumbani mle alimokaa mwenyewe, akamlaza kitandani pake. 20. Akamwomba Bwana, akanena, Ee Bwana, Mungu wangu, je! Umemtenda mabaya mjane huyu ninayekaa kwake hata kumfisha mwanawe. 21. Akajinyosha juu ya mtoto mara tatu, akamwomba Bwana, akanena, Ee Bwana, Mungu wangu, nakusihi, roho ya mtoto huyu imrudie ndani yake tena. 22. Bwana akaisikia sauti ya Eliya; na roho ya mtoto ikamrudia, akafufuka.”

 

Nabii Eliya alipokuwa anamuombea mtoto wa mjane afufuke, aliomba mara tatu Biblia inasema mara ya tatu Mungu akayajibu yale maombi, maombi yakaleta matokeo mtoto akafufuka. Nabii Eliya alikuwa anomba huku anafuatilia matokeo kama maombi yake yamejibiwa.

 

3.      Mtume Paulo

(Waefeso 1:15-23)

“15. Kwa sababu hiyo mimi nami, tangu nilipopata habari za imani yenu katika Bwana Yesu, na pendo lenu kwa watakatifu wote, 16. siachi kutoa shukrani kwa ajili yenu; nikiwakumbuka katika sala zangu, 17. Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; 18. macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; 19. na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; 20. aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; 21. juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; 22. akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo 23. ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.”

 

Mtume Paulo alikuwa anawaombea waefeso na anafuatilia maendeleo yao ndio maana alisema “tangu nilipopata habari za imani yenu katika Bwana Yesu na pendo lenu kwa watakatifu wote” maneno hayo yanaashiria kuwa alikuwa anaomba huku anafuatilia maendeleo ya watu anaowaombea ndio maana alipokuwa akipata habari zao kwamba jambo Fulani halijakaa sawa alikuwa anawaombea na kuwafundisha neno la Mungu.

 

HITIMISHO

Unapoomba uwe na utaratibu wa kufuatilia matokeo ya mombi yako ili uone kama maombi yameleta matokeo, hata kama bado haujaona matokeo ya maombi yao, endelea kuomba mpaka uone matokeo.


Chapisha Maoni

0 Maoni