UMAKINI (carefulness)



Mwl. Faraja Gasto
Somo hili lina vipengele vitatu
1.Utangulizi
2.Mbinu zitakazokufanya uwe makini au uongeze umakini
3.Kwa nini uwe makini

 ~```Utangulizi```~
Ukisoma kwa haraka Biblia unaweza ukadhani Biblia haijazungumzia suala la umakini lakini ukisoma taratibu utagundua kuwa suala la umakini limezungumzwa ndani Biblia.
Kwa mfano unapoona maneno haya
 (a) ngalieni mtu asi......... (wafanye mateka/asiwadanganye)
(Mathayo 24:4)(Wakolosai 2:8)
Hilo neno "angalieni" lina maanisha "Iweni MAKINI mtu asiwadanganye"
(b) Jihadharini (wafilipi 3:2)(Mathayo 7:15)
Hilo neno "jihadharini" lina maanisha "Iweni MAKINI"
(c)Aangalie asianguke (1 wakorintho 10:12)
Hilo neno "aangalie asianguke" lina maanisha "awe MAKINI asianguke"
---Nimekuonyesha hayo machache ili upate picha kuwa Biblia imezungumza umuhimu wa kuwa MAKINI katika kufanya mambo mbalimbali.
Kila jambo haijalishi ni la kiroho au la kimwili lina hitaji umakini katika kulifanya kwa mfano

----Unahitaji umakini katika kusikiliza
----Unahitaji umakini katika kusoma
----Unahitaji umakini katika kujibu maswali haijalishi ni mtihani au umeulizwa na mtu.
----Unahitaji umakini katika kufanya maamuzi
N. K

 ```Mbinu zitakazokufanya uwe makini au uongeze umakini```
1.Jifunze Kuhakiki Jambo (Proving)
Kuhakiki ni kujiridhisha, kukagua, kulithibitisha jambo,  kulipitia upya jambo fulani, kusoma upya ulichoandika au kilichoandikwa na pia kuhakiki ni kufuatilia jambo ili uone kama ni la kweli au la.
(Matendo ya Mitume 17:10-12)
Watu hao walipohubiriwa neno la Mungu walienda wao wenyewe kusoma upya ili waone kama kweli walichohubiriwa ni sahihi au sio sahihi,  walipojiridhisha kwamba kiko sahihi ndipo wakaamini.
Tabia mojawapo ya watu ambao wako makini ni kulihakiki jambo kabla ya kulitendea kazi.
(Waefeso 5:10)
Biblia inasema ni muhimu kuhakiki jambo ili ujue mapenzi ya Mungu ni yapi,  maana yake ni kwamba Mungu anahitaji watu makini kwa kuwa watu ambao wako makini ni rahisi kuyaelewa mapenzi ya Mungu.
Nataka nikupe mfano kwa kukuuliza hili swali,
Je!  Umewahi kwenda dukani ukanunua bidhaa halafu ukazidishiwa pesa(chenchi)?
Kama uliwahi kuzidishiwa pesa maana yake ni kwamba kilichomfanya huyo muuzaji akuzidishie pesa ni KUKOSA UMAKINI katika kurudisha chechi,  maana yake ni kwamba hakuhakiki kama pesa nayokurudishia ndio unastahili kurudishiwa.

2.Tafakari (Meditation)
Hii ni mbinu ya pili ikiwa unahitaji kuwa makini au kujiongezea umakini katika kufanya mambo mbalimbali,  ni muhimu ujifunze kutafakari.
(Yoshua 1:8)
Mungu alimwambia Yoshua TAFAKARI maneno yote yaliyoandikwa kwenye kitabu cha torati ili UFANIKISHE NJIA YAKO na pia ili USITAWI SANA.
Mungu alikuwa anampa Yoshua mbinu itakayomfanya kuwa mtu mwenye umakini katika kufanya mambo mbalimbali.
Tabia ya kutafakari ni tabia inayopatikana kwa watu  wenye umakini,  ikiwa na wewe unahitaji kuwa miongoni mwao jifunze kujizoeza kutafakari kabla ya kufanya jambo lolote (mithali 16:20a)

3.Jifunze kumuuliza Mungu
Nataka nikupe ushuhuda wangu kuhusu jinsi Mungu alivyokuwa akinifundisha kuhusu umakini.
Ilifika hatua nikawa nasahau sana, hali hiyo ilisababisha nikapoteza fedha nyingi kununua leso, nikawa napoteza vitu vingi kwa kusahau funguo na vitu mbalimbali lakini Mungu alinifundisha KUAGA,  yaani nikitaka kutoka mahali nilipo nilitakiwa kusema "Roho Mtakatifu naondoka hapa" nilipokuwa nikiaga nilikuwa nakumbushwa vitu ambavyo nimevisahau mahali nilipokuwa, hilo lilikuwa darasa la kuniongezea umakini.
(2 Samweli 2:1)
Tabia mojawapo aliyokuwa nayo Daudi ni kuuliza kwa Mungu kuhusu mambo mbalimbali.
Hii ni tabia ambayo unatakiwa kuwa nayo endapo unahitaji kuwa mtu makini,  jifunze kuuliza kwa Mungu kuhusu mambo mbalimbali.

4.Usifanye maamuzi ya haraka,  jifunze kuwa na tahadhari.
(Danieli 2:14-19)
Sifa mojawapo ambayo Danieli na wenzake waliyokuwa nayo ni UMAKINI,  ndio maana utaona hawa jamaa waliwahi kukataa chakula cha Mfalme kwa kuwa walijiridhisha kimeungamanishwa na miungu ya Babeli.
Hilo andiko hapo juu  linatujulisha kuhusu amri aliyotoa Mfalme ya kuwaua wenye hekima wa Babeli baada ya kushindwa kumkumbusha na kumtafsiria Mfalme ndoto aliyoota, lakini Danieli kwa BUSARA NA HADHARI AKAOMBA APEWE MUDA ili aje kumkubusha na kumtafsiria Mfalme ndoto yake.
ninachotaka uone hapo ni kwamba kuna vitu hutakiwi kuvitolea maamuzi au majibu ya haraka,  kuna vitu hutakiwi kuviendea kwa pupa utaumia,  Danieli aliomba apewe muda ili aende mbele za Mungu yeye na wenzake waombe ili Mungu awajulishe ile ndoto na tafsiri yake.
Ukiona mtu mtu anafanya mambo kwa pupa basi ujue UMAKINI HAUMO NDANI YAKE,  na akiendelea hivyo mwishowe ataumia.

5.Usifanye maamuzi kwa kufuata kile ambacho unaona kwa macho ya nje (physical eyes)
Hapa nizungumzie kuhusu vijana hususani linapokuja suala la mahusiano,  vijana wengi wanaingia kwenye mahusiano kwa kumwangalia mtu kwa jinsi alivyo kwa nje mwishowe wanajikuta kumbe walikosea kuchagua na hapo ndipo unatimia ule msemo usemao "ningejua huja mwisho wa safari"
Wengine wamejikuta wakishirikiana na watu ambao wanageuka kuwa kikwazo kwa huduma zao,  biashara zao n.k, kwa sababu ya kufuata kile kinachoonekana kwa nje.

(Mithali 15:25)
Biblia inasema kuna njia ambayo kwa macho ya nje ukiitazama unaona iko sawa lakini kumbe mwishowe hiyo njia inazalisha njia za mauti.
Hiyo ni sawa na kusema kuna jambo unaweza kuliona kwa nje liko sawa lakini kumbe lina madhara ndani yake ndio maana nakuambia usifanye maamuzi kwa kufuata macho yako ya nje.
Kuna wengine kwa kukosa umakini wamejikuta wakiwashirikisha watu fulani siri zao kwa kuwa walipowatazama tu wakaona wanaweza kutunza siri kumbe waliona vibaya, mwishowe wanakuja kushangaa siri zao zimeanikwa nje, wanajikuta wakiwa na hasira, wanawaza mawazo mabaya, wanajuta kuwashirikisha watu siri zao.
Hayo yote yanatokea kwa sababu ya kukosa umakini.

 ```Kwa nini unahitaji umakini```

1.Ili usipoteze vitu mbalimbali
---Nilikupa mfano wa mtu anayemzidishia pesa mteja na nikakwambia mtu huyo anakuwa amekosa umakini kwa hiyo anapomzidishia pesa mteja yeye anapoteza(anapata hasara)

2.Ili usijikute kwenye majuto, mateso n.k
----Nilikuonyesha mfano wa mtu anayeamua kumshirikisha mtu mwingine siri zake bila kujiridhisha kama huyo anayemshirikisha ana uwezo wa kutunza siri, mwishowe anakuja kusikia siri zake zimejulikana anaanza kujuta kwa nini alitoa siri zake.
Hili suala la kutoa siri lilimponza Samsoni mwishowe akang'olewa macho (Waamuzi 16:15-21)
Mungu akubariki kwa kujifunza, huo ni mtaji wa kukuongezea umakini katika kufanya mambo mbalimbali.


Chapisha Maoni

0 Maoni