Mwl.Faraja Gasto
(o767955334)
UTANGULIZI
Nakusalimu katika jina la Bwana Yesu
Katika familia zetu huwa tunashuhudia upendo
wa wazazi ukiangukia kwa baadhi ya watoto au kwa mtoto fulani kutegemeana na
sababu mbalimbali kwa mfano, wazazi wengi huwapenda watoto wao wa kwanza na wa
mwisho na pia wengine huwapenda watoto au mtoto fulani kwa madai kwamba ni mtii
au ana tabia tofauti na wenzake.
Pia tunashuhudia upendo wa wazazi ukiwa
umegawanyika kwa watoto Fulani, kwa mfano utakuta mama anawapenda watoto Fulani
na baba anawapenda watoto Fulani(kuna mtoto au watoto ambao ni kipenzi cha baba
na kuna mtoto au watoto ambao ni kipenzi cha mama)
Katika familia utakuta watoto au mtoto
anayependwa ndiye ambaye anaijua mipango ya wazazi au mzazi(baba au mama),
mtoto anayependwa ndiye ambaye anaruhusiwa kuingia kwenye chumba cha wazazi,
mtoto anayependwa ndiye anayepewa pesa haraka anapoomba n.k
Ukweli
Usiopingika: Upendo hauwezi ukalingana kwa watoto wote, kila mzazi huwa kuna
watoto au mtoto anayempenda kuliko wengine.
Wazazi wengi hawafahamu kuwa kuonyesha upendo
kwa baadhi ya watoto au kwa mtoto fulani ni kumtengenezea vita huyo mtoto au
hao watoto wanaopendwa kuliko wengine, upendo huo wa wazazi huwafanya hao
watoto wachukiwe na wenzao haijalishi mzazi anajua au hajui hilo, chuki hiyo
inaweza kuleta madhara makubwa kuanzia utotoni mwao hata watakapokuwa watu
wazima kama haitashughulikiwa mapema.
(Mwanzo 37:1-4)
Yakobo alikuwa na watoto wengi lakini
alijikuta anampenda Yusufu maana ni mtoto wake wa uzeeni, upendo huo
ulisababisha Yusufu akachukiwa na ndugu zake kutokana na kupendwa na baba yao.
Ninachotaka uone hapo ni kwamba mtoto
anapopendwa sana na mzazi au wazazi wake huwa anajikuta akichukiwa na ndugu
zake, chuki hiyo inaweza kumletea matatizo makubwa kama wazazi au mzazi
hatakuwa makini kuhakikisha mtoto huyo anakuwa salama.
MAMBO AMBAYO
WAZAZI WANATAKIWA KUFANYA IKIWA KUNA MTOTO AU WATOTO WANAOWAPENDA KULIKO
WENGINE
1.Waombee
hao watoto ili Mungu awalinde na ikiwa ni mmoja muombee ili Mungu amlinde
(Mwanzo 37:20)
Unapoona unampenda mtoto au watoto Fulani
zaidi ya ndugu zao hakikisha unawaombea ili Mungu awalinde dhidi ya chuki ya
ndugu zao.
2.Wasihi hao
watoto wasipende kuwaambia ndugu zao
mipango yao au ndoto zao
(Mwanzo 37:5)
Yusufu alipowaambia ndugu zake ndoto alizoota
tunaona ndugu zake wakazidi kumchukia maana yake ni kwamba chuki iliongezeka
maradufu waliposikia ndoto ya Yusufu.
Kwa hiyo wewe kama mzazi hakikisha unawasihi
watoto unaowapenda kuliko wengine au mtoto unayempenda kuliko wengine asipende
kuelezea mipango yake au ndoto zake akiwa na ndugu zake ni heri akuambie wewe
mzazi kuliko kuwaambia ndugu zake.
3.Jitahidi Kuuficha
upendo
Nimeanza kwa kusema JITAHIDI kwa sababu
upendo una nguvu ya ajabu, mtu akipenda kitu lazima itajulikana tu kwamba
amependa ila unaweza kujitahidi kuuficha upendo wako ili isijulikane kirahisi
ni mtoto yupi unampenda kuliko wengine.
(Mwanzo 37:3-4)
Yakobo alimpenda Yusufu ikafika hatua
ikajulikana kuwa anampenda Yusufu kuliko ndugu zake, ndugu zake walijua hilo
kwa sababu Yakobo aliufunua upendo wake kwa Yusufu kwa kumshonea kanzu ndefu,
hiyo kanzu aliyoshonewa Yusufu ilidhihirisha jinsi anavyopendwa na baba yao.
Sasa unaweza ukajiuliza unafichaje upendo
wako?
(a).Epuka kumpa zawadi mtoto unayempenda kuliko
wengine, usimpe zawadi mbele ya macho ya ndugu zake lakini haina maana kwamba
hautakiwi kumpa zawadi, endapo utajisikia kumletea zawadi ni vema umpe akiwa
peke yake na pia usizoee kumpa zawadi yeye peke yake, jifunze kuwapa watoto
wako wote zawadi bila kubagua, unapowapa zawadi watoto wote ni vema zawadi zao
zifanane ili kusiwepo na alama ya kuuliza kwa nini fulani kapewa zawadi tofauti
na wenzake.
(b).Epuka kumsifia huyo mtoto unayempenda
kuliko wengine, usimsifu mbele ya ndugu zake.
(c).Unapohitaji kuzungumza na mtoto
unayempenda kuliko ndugu zake, usimuite chumbani kwako wakati ndugu zake wapo,
ni vema usubri wakati ndugu zake wakiwa hawapo ndipo uzungumze naye unayotaka
kumwambia.
MADHARA
YANAYOTOKANA NA MGAWANYIKO WA UPENDO BAINA YA WAZAZI WAWILI(BABA NA MAMA)
Kama ambavyo nimetangulia kusema ni kwamba
kila familia huwa ina mtoto au watoto ambao ni kipenzi cha mama na kuna mtoto
au watoto ambao ni kipenzi cha baba bila kujali jinsia kwa sababu mama anaweza
kujikuta upendo wake umeangukia kwa mtoto au watoto wa kiume, baba anaweza
kujikuta upendo wake umeangukia kwa mtoto au watoto wa kike itategemeana na watoto
waliopo wana mchanganyiko wa jinsia au wana jinsia moja. Pia wazazi wanaweza
kujikuta upendo wao umeangukia kwa watoto wa kiume kuliko watoto wa kike na pia
upendo unaweza ukaangukia kwa watoto wa kike kuliko wa kiume kutegemeana na
sababu mbalimbali.
(Mwanzo 25:27-28)
Isaka alikuwa na watoto wawili ambao ni Esau
na Yakobo, kila mtoto alikuwa na sifa yake, Esau alikuwa mwindaji, Yakobo
alikuwa mtu mtulivu aliyependa kukaa nyumbani huku akiwa anapika chakula,
tunaona Isaka alimpenda sana Esau kwa sababu alikula mawindo yake, Rebeka
alimpenda sana Yakobo kwa sababu alikuwa mtulivu na alipenda kukaa nyumbani na
mama yake.
Wakati Isaka amezeeka alitaka kumbariki Esau
kwa kuwa ndiye mzaliwa wake wa kwanza na pia kwa sababu alimpenda ndio maana
alipotaka kumbariki alimwambia akalete mawindo ili aandae chakula anachokipenda
yaani Isaka alitaka apate kwanza kitu kinachomfanya ampende Esau ndipo ambariki
lakini hatuoni Isaka akiwa na mpango wa kumbariki Yakobo kwa sababu upendo wake
haupo kwa Yakobo japo ni mtoto wake.
Tunaona Rebeka aliposikia Isaka anataka
kumbariki Esau, Rebeka alimuita Yakobo akampa mbinu kuhusu namna ya kuzipokea
zile Baraka zilizokusudiwa kwenda kwa Esau mwishowe Yakobo alizipata zile Baraka
(Mwanzo 27:27-29)
Esau alimchukia sana Yakobo kwa sababu
ametwaa Baraka ambazo hazikutakiwa kwenda kwake, Esau akasema anasubiri msiba
ukiisha basi atamuua Yakobo, Rebeka alipopata taarifa kuwa Esau anakusudia
kumuua ndugu yake tunaona Rebeka anamshauri Yakobo akimbie akakae mbali na
ndugu yake mpaka ghadhabu ya ndugu yake itakapotulia (Mwanzo 27:42-45)
Madhara yaliyotokea: Esau alikuwa na chuki
dhidi ya ndugu yake, Yakobo ilibidi akimbie akae mbali na kwao.
Madhara Ya
Upendo Kugawanyika
1.Katika familia huwa kunakuwa na
matabaka(classes)
Kama baba akiwa uwezo wa kiuchumi kuliko mama
basi watoto wanaopendwa na baba watakidhiwa mahitaji yao kwa haraka kuliko wale
wanaopendwa na mama. Pia ni rahisi kukuta wakisaidiana watoto wanaopendwa na
baba tu, na wale wanaopendwa na mama watajikuta wakisaidiana wao kwa wao.
2.Watoto wasiopendwa na baba hujikuta
wakimuona baba yao kama adui vivyo hivyo watoto wasiopendwa na mama hujikuta
wanamuona mama yao kama adui yao.
3.Ubinafsi huwa unapandikizwa ndani ya watoto
Vitu walivyo navyo watoto wanaopendwa na baba
vitatumiwa na wao tu yaani utadhani wao wana familia yao, pia vitu walivyonavyo
watoto wanaopendwa na mama watajikuta wanapenda kupeana vitu wao kwa wao.
4.Migogoro itatokea baina ya watoto na watoto
pia baina ya wazazi na watoto
Nimewahi kusikia mama akimchukia binti yake kwa
madai kwamba yamkini anatembea na baba yake kwa sababu imefika hatua baba anampenda
mtoto wake wa kike kuliko mkewe, hii ni hatari sana ikitokea katika familia.
5.Kutatokea hali ya kushushana thamani
Kama baba atampenda mtoto Fulani kuliko
wengine, hao watoto watamshusha thamani baba yao na pia hawatamtii kwa sababu
wanajua hana upendo wa dhati kwao. Vivyo hivyo kama mama atampenda mtoto Fulani
kuliko wengine basi hao wengine watamshusha thamani mama na pia hawatamtii kwa
sababu wanajua hana upendo dhidi yao.
KWA NINI UPENDO WA WAZAZI UNAGAWANYIKA
Zipo sababu nyingi ambazo zinasababisha
upendo wa wazazi kugawanyika, sababu zote hizo ziko kwenye makundi mawili;-
1.Sababu za kiroho
Kwa mfano kama mtoto alizaliwa au amezaliwa
kutokana na ahadi ya Mungu yaani Mungu ametimiza ahadi yake ya kukupa mtoto
lazima utajikuta unampenda huyo mtoto kuliko wenzake ambao hawakuzaliwa kwa
ahadi ya Mungu. Ndio maana upendo aliopendwa Ishmaeli haukulingana na upendo
aliopendwa Isaka kwa sababu kuzaliwa kwao kulikuwa kwa jinsi mbili tofauti.
Hiyo ni sababu mojawapo.
2.Sababu za kimwili
Kwa mfano kama mtoto ni mtii lazima utajikuta
unampenda kuliko wengne ambao hawatii.
0 Maoni