-----Mwl.Faraja
Gasto----
UTANGULIZI
Kila mwanadamu ameumbwa kwa kusudi Fulani la
Mungu kwa hiyo Mungu humtaka kila mtu kuwa katika eneo sahihi. Kuwa katika eneo
sahihi maana yake ni kwamba ni kuwa katika eneo ambalo Mungu anataka uwepo,
kufanya kazi katika eneo ambalo Mungu anataka ufanye kazi, kusoma shule au chuo
ambacho Mungu anataka usome.
Shida au changamoto zinazowapata watu wakati
mwingine zinasababishwa na watu kutokuwa katika eneo sahihi.
Ni muhimu kila mtu afahamu kuwa kuwa kuna
Baraka hautazipata kama hauko katika eneo ambalo Mungu anataka uwepo.
(Mwanzo 2:15)
Adamu alikuwa anaishi katika bustani ya Edeni
kwa sababu Mungu alimuweka pale kwa kazi ya kulima na kuitunza Bustani, faida
alizopata Adamu alipokuwa katika eneo sahihi;-
a).Mungu alimuumbia mtu wa kumsaidia majukumu
yake.
b).Alipata kila alichotaka(full supply).
c).Alikuwa amefunikwa na utukufu wa Mungu.
d).Alikuwa na kazi ya kufanya.
Ni muhimu ufahamu kuwa kuna faida za kuwa
katika eneo sahihi kwa kuwa unapokuwa kwenye eneo sahihi ni rahisi kupata
msaada wa Mungu katika maeneo mbalimbali, ni rahisi kupata mahitaji yako, ni
rahisi kumsikia Mungu.
Angalia kitu ambacho Mungu alimuuliza Eliya,
Eliya alipokuwa ametishiwa na Malkia Yezebeli kwamba atamuua tunaona Elia
alikimbilia mahali Fulani lakini alipokuwa katika lile eneo Mungu nalimuuliza
“Unafanya nini hapo Eliya” (1 Wafalme 19:9) Swali hilo aliulizwa kwa kuwa
hakuwa katika eneo sahihi ndio maana Mungu anamuuliza Eliya kwa nini yuko hapo.
Cha kujifunza ni kwamba unaweza ukawa katika
eneo Fulani lakini Mungu akawa hajaridhia kukuona ukiwa hapo.
Unaweza ukajiuliza nitajuaje kama niko eneo
sahihi?
ISHARA ZA
KUKUJULISHA HAUKO ENEO SAHIHI (UNAFANYA
KAZI ISIYO SAHIHI, UNASOMA SHULE AU CHUO KISICHO SAHIHI KWAKO)
1.Kufanya
kazi ambayo hauna amani nayo, kazi usiyoifurahia (unafanya kazi lakini moyoni
hauipendi au unajisikia kuichoka).
Soma ushuhuda huu, Mchungaji mmoja alijikuta
anafanya kazi ya Mungu lakini anaona ni mzigo mzito kwake ikabidi aende mbele
za Mungu kumuuliza kwa nini anajisikia kuchoka na hiyo kazi ya uchungaji,
alipokuwa katika kuomba Mungu akamwambia “sikukuita kuwa Mchungaji, nilikuita
ili uwe mwalimu hiyo ndio sababu inayosababisha unajisikia kuchoka na hiyo kazi
kwa kuwa unafanya kazi ambayo sio sahihi kwako kuifanya”
Kama unafanya kazi na hauna amani na hiyo
kazi, unaona hiyo kazi ni kama mzigo mzito ni dhahiri ulidandia kazi ambayo sio
yako, kazi hiyo sio sahihi kwako.
Lakini kama uko mahali na unafanya kazi
sahihi hata kama itafika hatua utaona imekuwa mzigo lazima Mungu atakupa msaada
ili uione kazi ni rahisi.
(Kutoka 181:20)
Mungu alipooona kazi aliyompa Musa imekuwa
mzigo kwa Musa, Mungu alimleta baba mkwe wa Musa ili ampe ushauri wa namna ya
kutenda kazi hiyo, Musa akapata ushauri uliomsaidia kupunguza majukumu hatimaye
Musa akapunguziwa mzigo ili kazi isiwe sababu ya yeye kudhoofika.
2.Kusoma
shule au chuo ambacho unajisikia kuhama hapo au unasoma lakini unajisikia
kuacha kusoma hiyo kozi au hayo masomo.
Ukisoma shule ambayo sio sahihi kwako au
ukisoma kozi ambayo sio sahihi kwako utajikuta unaona safari ya elimu ni mateso
makali sana, utasoma lakni ndani yako unajisikia kuacha shule au chuo, unaona
masomo ni magumu, ukiona hali hiyo tafakari eneo ulipo au kozi au masomo
unayosoma, inawezekana hauko mahali sahihi.
Ukisoma kozi sahihi hata kama ni ngumu Mungu
atakusaidia na hautashindwa kwa kuwa uko mahali sahaihi, kama unasoma shule
sahihi ni rahisi kumuona Mungu akijifunua hapo shuleni katika safari yako ya
elimu.
3.Kama
umejenga nyumba katika eneo ambalo una vita kila kona imefika hatua hauoni
furaha kukaa ndani ya hiyo nyumba.
(Isaya 60:21a)
Biblia inasema “utajenga nyumba na kukaa
ndani yake” maana yake ni kwamba ukijenga nyumba ambayo hauna hamu ya kuendelea
kuishi ndani yake maana yake ni kwamba eneo ulilopo sio sahihi kwako,
haukutakiwa kujenga hapo.
4.Kuishiwa/Kupungukiwa
badala ya kuongezeka.
Ikiwa uko katika eneo Fulani na unajikuta
uwepo wa Mungu unaisha ndani yako au unapungua ndani yako badala ya kuongezeka
tafakari eneo ulilopo. Ikiwa unasali katika kanisa ambalo ukiwa hapo unajisikia
kuchoka na safari ya kwenda mbinguni, nguvu za maombi zinapunguka n.k tafakari
eneo ulilopo ila ni vema ufahamu kanisa linaweza likawa zuri kabisa kwa nje
lakini ndani likawa lina shida na pia kania linaweza likawa zuri ni la kiroho
kabisa lakini Mungu hajaridhia wewe uwe hapo kwa hiyo itakuwa ngumu sana kuona
uwepo wa Mungu ukiwa hapo.
Ikiwa uko katika eneo ambalo hata mali zako
zinaisha badala ya kuongezeka, ni muhimu ufahamu hauko mahali sahihi.
Ikiwa uko katika eneo sahihi hata biashara
unayofanya Mungu ataifanya iongozeke, nguvu za kiroho lazima ziongezeke n.k.
(Zaburi 23:16)
Mfalme Daudi anasema Bwana ndiye Mchungaji
wangu, sitapungukiwa na kitu. Kama hawezi kupungukiwa maana yake ni kwamba
katika eneo alilopo lilikuwa eneo sahihi kwa kuwa hiyo nafasi aliyonayo ni
Mungu alimpa kwa hiyo Mungu hawezi kuruhusu apungukiwe kwa kuwa Mungu yupo
kumuongoza ni wapi aende apate mahitaji yake.
(Luka 15:11-13)
Huyu kijana aliondoka kwao na mali lakini
alipofika eneo Fulani akajikuta anatumia zile mali kufanyia anasa na mwishowe
akajikuta hata alichokuwa nacho kimeisha kwa sababu hakuwa katika eneo sahihi.
5.Kutumia
vibaya kile ulichonacho au kutotumia ulichonacho.
Watu wengi hawafahamu kuwa kuna uhusiano kati
ya eneo ambalo mtu yupo na matumizi ya kile alichonacho.
Kitu mojawapo kinachowafanya watu wasiwe na
matumizi mazuri ya vitu walivyonavyo(mali, vipaji, karama n.k) ni kutokuwa
katika eneo sahihi, kama hauko mahali sahihi ni rahisi kujikuta umetumia vibaya
kile ulichonacho au kutotumia kabisa ulichonacho.
Kuna mahali unaweza ukaishi na ukajikuta
akili zako hazifanyi kazi vizuri, unajikuta unashindwa kutumia akili zako
vizuri, unajikuta hautumii vipawa ulivyo navyo n.k maana yake ni kwamba hauko
mahali sahihi.
(Luka 15:11-14)
Huyu kijana alipokuwa kwa baba yake hatuoni
akitumia mali vibaya lakini baada ya kuondoka kwa baba yake akaanza kuishi
maisha ya anasa kwa kutumia mali vibaya. Alienda kuishi eneo ambalo sio sahihi
kuishi akajikuta hata mali alizokuwa nazo anazitumia vibaya.
N.B ni muhimu ufahamu kuwa haina maana kwamba
ukiwa katika eneo sahihi hautakumbana na changamoto, changamoto haziepukiki
hata ukiwa mahali sahihi utakumbana nazo lakini maadamu uko katika eneo sahihi
ni rahisi kuuona msaada wa Mungu katika hizo changamoto.
Angalizo: (1).Usiwe mwepesi wa kufanya maamuzi ya kuacha kazi, kuhama
kanisa, kuhama nyumba au kuhama shule/ chuo au kubadilisha kozi bila kumuuliza
Mungu kwa kuwa shetani akiona uko mahali sahihi huwa anafanya juu chini kuhakikisha
anakutoa mahali hapo anaweza akakuinulia watu wa kufanya vita na wewe ili
uondoke hapo pia anaweza kuchafua hali ili hali hiyo ikuondoe hapo.
(2).Usifanye kazi maadamu ni kazi, usijenge
nyumba maadamu una uwezo wa kujenga, usisome masomo yoyote maadamu alama(marks)
zako zinaruhusu kusoma hiyo kozi, ni muhimu kuhitaji maelekezo ya Mungu kwanza
ili usije ukajikuta hauko mahali sahihi halafu mwisho wa siku ukajikuta hauoni
msaada wa Mungu katika unachofanya.
MAMBO
YANAYOWAFANYA WATU WASIWE KATIKA ENEO SAHIHI
1.Kuangalia
mazingira au hali Fulani.
Kwa mfano vijana wengi hususani wanaosoma
ukiwauliza kwa nini wanasoma masomo wanayosoma utasikia wakisema ni kwa sababu
watu waliosoma hayo masomo wanaajiriwa sana.
Kwa hiyo wanasoma kwa kuangalia upepo
unaendaje, ikitokea upepo umebadilika ghafla ndio maana wengi wanajikuta hawana
ajira, wamesoma lakini ni kama hawakusoma, hiyo yote ni kwa sababu hawakuwa
katika eneo sahihi.
Tabia ya kuangalia upepo unavyoenda au
kuangalia mazingira imewafanya watu kuwa katika maeneo ambayo sio sahihi, kwa
kufanya kazi katika maeneo yasiyo sahihi, kusoma kozi ambazo sio sahihi kwao.
(Mwanzo 13:10-13, 19:1-29)
Lutu aliangalia mazingira, akaenda akakaa
kwenye eneo ambalo mwishowe liliangamizwa hatimaye akaondoka akiwa hana mali,
hana mke.
2.Kutomsikiliza
Mungu
(Mathayo 17:24-27)
Laiti kama Petro asingekuwa mahali sahihi
asingepata fedha ya kulipia kodi, Petro alipata fedha ya kulipia kodi kwa kuwa
alifuata maelekezo ya Yesu.
(Mathayo 2:13-14)
Herode alipopanga kumuangamiza Yesu, Mungu
alimtuma malaika kumwambia Yusufu aondoke katika lile eneo. Laiti kama Yusufu
asingefuata maelekezo aliyopewa na Mungu, yamkini Herode angeweza kumuua Yesu.
JE! MUNGU
HUWA ANATOA MAELEKEZO KUHUSU ENEO SAHIHI LA WEWE KUWEPO?
Ndio Mungu huwa anatoa maelekezo ya kuhusu mahali
sahihi kwa wewe kuwepo, Mungu huwa anaweza kutoa maelekezo shule ipi au chuo
kipi usome, Mungu anaweza akatoa maelekezo ujenge nyumba wapi, Mungu anaweza
kutoa maelekezo wapi ufanye kazi (biashara au ajira au huduma)
Soma mifano ifuatayo:-
(Mwanzo 12:1)
Mungu alimwambia Ibrahimu atoke katika hilo
eneo alilopo aende katika eneo ambalo atamuonyesha kwa kuwa akikaa hapo hawezi
kupata Baraka ambazo Mungu anakusudia kumpa.
Ibrahimu alipochukua hatua ya kuondoka hapo
akaenda mahali ambapo Mungu alimuelekeza, Ibrahimu alipokea Baraka za Mungu kwa
kiwango kikubwa sana.
(Matendo ya mitume 1:4)
Yesu aliwaambia wanafunzi wake wasitoke
Yerusalemu mpaka watakapopokea uwezo utokao juu, wasitoke Yerusalemu bila
kujazwa Roho Mtakatifu, kwa kuwa endapo wataondoka hapo bila huo uwezo
watajikuta hawafanyi kitu chenye matokeo katika huduma aliyokusudia waifanye.
(Waamuzi 6:24-26)
Mungu alimwambia Gideoni mahali sahihi ambapo
anatakiwa kujenga madhabahu. Tunachojifunza hapa ni kwamba unaweza ukajenga
madhabahu katika eno ambalo Mungu hajakuagiza kujenga, tunaona Gideoni
alipotokewa na malaika wa Mungu Gideoni alijenga madhabahu(Waamuzi 6:24) lakini
Mungu alikuja kumpa maelekezo ya kujenga madhabahu katika eneo ambalo Mungu
ameliridhia.
Tunapotazama nyakati za leo watumishi wengi
wamekuwa na viwango vya chini vya kumsikiliza Mungu, wengi wanapojenga
makanisa, wanajenga ili mradi wawe na mahali pa kuabudia badala ya kufuata
maelekezo ya Mungu ili wajenge kwenye eneo sahihi.
HITIMISHO
Kwa hayo machache naamini kuna kitu Mungu
amekipanda ndani yako, ni ombi langu Mungu akupe hatua ya kutendea kazi
fundisho hili ili uwe katika eneo sahihi hatimaye iwe rahisi kupata msaada wa
Mungu n.k
0 Maoni