Faraja Gasto
Mambo ya
kujifunza katika somo hili;-
1.Mbinu
zitakazosababisha uwepo wako uwe na faida
2.Umuhimu wa
kuwa na uwepo wenye faida.
Lengo la somo: Ni kukupa mbinu zitakazosababisha uwepo wako
uwe na faida katika jamii, katika familia yako, kazini kwako, kanisa, taifa n.k
Utangulizi wa somo
Kila
mwanadamu huwa anazalisha kitu Fulani haijalishi ni chema au kibaya,
ninapozungumzia kuwa na uwepo wenye faida maana yake ni kwamba uwepo wako ulete
mambo ambayo ni mazuri (yanayojenga na kubariki maisha ya watu).
Faida ya
uwepo wako inaonekana kutokana na mchango wako kwa jamii yako, familia yako,
kanisa na taifa, faida ya uwepo wako inatokana na kile kinachozaliwa au kile
kinachotokea ukiwepo.
Katika
kuishi kwetu duniani tuwapo kwenye kazi zetu, makanisani, familia zetu n.k kuna
watu wawepo au wasiwepo kunakuwa hakuna faida yoyote kwa sababu uwepo wao
hautengenezi kitu ambacho ni chema lakini kuna watu wasipokuwepo lazima mtajua
tu fulani hayupo(yaani kunaonekana kuna pengo) na hata akifika tu lazima
itajulikana fulani amefika(pengo litazibika), hiyo yote ni kwa sababu uwepo
wake unasababisha kitu fulani kutokea
Japo kuna
watu wakiwepo lazima ubaya utaonekana au lazima mambo yaharibike, kuna watu
wakiwepo lazima mambo mazuri yataonekana, inategemea na kile ambacho huyo mtu
anatoa/anazalisha.
Nimeona na
kusikia familia mbalimbali wazazi wakilaani uzao wao kwa kuwa hawaoni faida ya
kuzaa kwa kuwa watoto ni watukutu, hawashiki, hawakubali kuelekezwa, pia kuna
familia ambazo watoto wanatamani baba yao afariki au mama yao afariki kwa
sababu hana faida yoyote, yaani awepo au asiwepo hakuna jema linalotengenezwa
na uwepo wake.
Nakumbuka
wakati ilipotangazwa kwamba mtumishi wa Mungu FANUEL SEDEKIA ana hali ambayo
sio nzuri, kuna watu walifunga na kuomba kwa ajili yake, kuna watu walimlilia
Mungu amponye.
Ninachotaka
uone hapo ni kwamba kama uwepo wako hauna faida yoyote hakuna mtu atakuwa na
hamu ya kuwa karibu na wewe, hakuna mtu atajihangaisha kufunga kwa ajili yako,
hakuna mtu ambaye atawaza kuhusu maisha yako, hakuna ambaye atahangaika
kukuombea.
Tunapojifunza
kuwa na uwepo wenye faida maana yake ni kwamba ifike hatua uwepo wako uwe baraka
katika maisha ya watu, uwepo wako usiwe balaa au usiwe hauna faida yoyote
kwenye maisha ya watu wengine haijalishi ni katika jamii unayoishi, katika
kanisa, familia na taifa.
Jitafakari kwa kujiuliza yafuatayo;-
Uwepo wako
una faida gani kwenye jamii unayoishi?
Uwepo wako
una faida gani kwenye kanisa unapoabudu?
Uwepo wako
una faida gani kwenye familia yako?
Uwepo wako
una faida gani kwenye taifa lako?
Ikitokea
umekufa watu watalia kwa sababu gani?
Unapopatwa
na shida Fulani ni watu wangapi wanapata mzigo wa kuona unatoka kwenye shida
hiyo?
MAMBO MATATU (3)YA KUFANYA ILI UWEPO WAKO UWE
NA FAIDA
1.Tekeleza wajibu wako (implement your
responsibilities)
Mungu
alipomuumba mtu alimpa wajibu wa kufanya katika bustani ya Edeni,
tunachojifunza hapo ni kwamba kuwajibika ni suala ambalo haliepukiki maadamu
uko hai lazima ujifunze kuwajibika. Mungu anataka uwajibike kwa ajili yako
mwenyewe na kwa ajili ya wengine.
Kila
mwanadamu ambaye amejitambua huwa ana aina sita za wajibu ambao anatakiwa
kuutekeleza;-
a).Wajibu
katika familia
Kama ni baba
ana wajibu wa kuongoza na kutunza familia, kama ni mama ana wajibu wa kutii kwa
mume wake na kuhakikisha anamsaidia mumewe ili atomize majukumu na mipango
mbalimbali, kama ni mtoto anawajibika kutii wazazi wake na kufuata kile
anachoelekezwa na wazazi wake.
b).Wajibu unaotokana na masuala ya kiroho au
miongozo ya kiroho
Huu wajibu unategemea
na wito wa mtu au msukumo wa ndani ya mtu husika katika kufanya jambo fulani.
c).Wajibu katika jamii inayomzunguka
Kushiriki
kwenye misiba, sherehe mbalimbali, kushiriki vikao vya mtaa au kijiji n.k
d).Wajibu
unaotokana na kazi ambayo mtu anaifanya
Kama mtu ni
mwalimu wa shule anawajibika kufundisha kile alichopangiwa kufundisha, kama mtu
ni mfanyabiashara anawajibika kuuza na kununua bidhaa n.k
e).Wajibu
unaotokana na taratibu za kisheria
Kutunza mazingira
yanayomzunguka, kupeleka watoto shule, kuheshimu vitu vya watu wengine kama
mipaka ya viwanja n.k
f).Wajibu
unaotokana na taratibu za mtu binafsi (wajibu wa kujipa mwenyewe)
Kwa mfano kusoma
vitabu, kuwatembelea marafiki, ndugu n.k
Kwa hiyo kama
wewe ni baba timiza wajibu wako kama baba, kuna familia zingine yaani baba au
mama akiwepo watoto hawaoni faida ya uwepo wao yaani watoto wanatamani baba afe
au mama afe kwa sababu hawatimizi wajibu unaowahusu, kuna familia ambazo wazazi
hawaoni faida ya kuzaa kwa sababu watoto ni watukutu, hawashikiki wala
hawaambiliki.
Ukitekeleza
wajibu wowote unaokuhusu, lazima uwepo wako utakuwa na faida sana.
Kama wewe ni
mume au baba wa familia hakikisha unatimiza wajibu wako kwa mkeo na kwa watoto
(Waefeso 5:25-29).
Kama wewe ni
mama hakikisha unatimiza wajibu wako kwa mmeo na kwa watoto (Wefeso 5:22-23).
Kama wewe ni
kiongozi hakikisha unatimiza wajibu wako kwa unaowaongoza (1 Timotheo 4:11-12,
2 Timotheo 4:5).
2.Ishi ndoto zako, tembea kwenye maono yako
na pia tembea kwenye wito wako au kwenye kusudi la Mungu juu ya maisha yako (live
your dream, walk on your vision, walk on your calling, fulfill God’s purpose on
your life)
(Mwanzo
41:37-38)
Yusufu
alitembea kwenye kusudi la Mungu kwenye maisha yake ndio maana ilifika hatua
mpaka Mfalme Farao akasema “tupate wapi mtu kama huyu ambaye roho ya Mungu iko
ndani yake” Ukitembea kwenye kusudi la Mungu juu ya maisha yako lazima Mungu
awe pamoja na wewe, kukufundisha na kukuongoza, Yusufu aliweza kutafsiri ndoto
mbalimbali kwa kuwa Mungu alikuwa pamoja naye. Uwepo wa Yusufu kwenye nchi ya
Misri ulikuwa na faida sana kwa sababu alitembea na Mungu.
Nataka
nikupe mifano ya watu wachache ambao uwepo wao umekuwa na faida kubwa sana pale
walipoamua kuishi ndoto zao au kutembea kwenye ndoto zao.
Nikianza na
mtu anaitwa Mark Zuckerberg mwanzilishi na mmiliki wa mtandao wa facebook,
alivumbua mtandao huu akiwa na miaka 20 tu. Leo hii Facebook ni mtandao maarufu
duniani unaokuwezesha kuwasiliana na mtu ambaye yupo katika nchi yoyote duniani
maadamu awe na akaunti kwenye mtandao huu, kupitia mtandao huu kuna watu
wamefikiwa na injili, kupitia mtandao huu kuna watu imani zao zimekua, kupitia
mtandao huu kuna watu wamepata wake na waume n.k hayo ni baadhi ya mambo chanya
yaliyotokana na mtandao huu.
Mfano wa
pili nahitaji nimzungumzie mtu anaitwa Alexander Graham Bell huyu anatajwa kuwa
ndiye mgunduzi wa simu mnamo mwaka 1876.
Nimekuonyesha
hao watu wachache ili kukuonyesha namna uwepo wako utakuwa na faida endapo
utaamua kutembea kwenye ndoto zako au maono yako.
(Kutoka 5:1)
Uwepo wa
Musa katika nchi ya Misri ulikuwa na maana sana pale alipokubali kutembea
kwenye kusudi la Mungu, kupitia Musa wana wa Israeli walifanikiwa kutoka Misri
kwenye nchi ya utumwa na mateso.
Ninachotaka uone
hapo ni kwamba ukitembea katika kusudi la Mungu utaufanya uwepo wako uwe na
faida pale utakapotembea katika kusudi la Mungu, unapokubali kufanya kile
ambacho Mungu anakuelekeza kufanya lazima uwepo wako uonekane una faida.
3.Fanyika Baraka kwenye maisha ya watu
wengine au Sababisha mambo mema kutokea (become a source of good things)
Sababisha
mambo mema kutokea kwenye maisha ya watu wengine
a).Fanyika
sababu ya watu wengine kupata furaha
b).Fanyika sababu
ya watu kutojutia kuzaliwa
c).Fanyika sababu ya watu wengine kumuona Mungu
d).Fanyika
furaha ya watu wengine
e).Kama
umeajiriwa, sababisha kampuni ipate faida n.k
(Matendo ya
mitume 9:36-41, ukisoma habari hiyo utaona kuna mwanamke mmoja aitwaye Dorcas,
huyo mama alikuwa akiwashonea wajane nguo, alifanyika Baraka sana kwa hao
wajane hata ilipofika hatua amefariki walipata huzuni kubwa sana kwa kuwa
waliona hakuna mtu wa kuziba hilo pengo.
Mzalie Mungu
matunda kwa kufanya kazi njema.
(Yohana 15:1-2)
Ili uwepo
wako uwe na faida, jifunze kufanya kazi ambazo zinamzalia Mungu matunda, kazi
ambazo zitawafanya watu wampe Mungu sifa kwa sababu ya uwepo wako.
Naamini
umewahi kusikia watu wakimwambia mtu Fulani “ukiwepo wewe hakuna
kinachoharibika” yaani kila kitu kinakwenda vizuri.
Hivyo ndivyo
Mungu anavyotaka kutuona tukimzalia Matunda kwa kila kazi njema.
UMUHIMU WA KUWA NA UWEPO WENYE FAIDA
1.Utapata watu wa kukuombea hata kama wewe
haujajiombea(you’ll get people who will pray for your sake)
Dorkasi
alikuwa mwanamke aliyekuwa na uwepo wenye faida ndio maana alipokufa kuna watu
hawakukubali ikabidi wamuite Petro aje aombe na alipoomba Mungu akamrudisha
tena Dorkasi.
(Matendo ya
mitume 9:36-41) Unadhani kama uwepo wake ungekuwa hauna faida wangehangaika
namna hiyo? Ni wazi wangemzika kama walivyokuwa wanazika watu wengine.
(Matendo ya
mitume 12:5-17)
Uwepo wa
mtume Petro ulikuwa na faida kwa kanisa ndio maana alipopatwa na tatizo, watu
walijitoa kumuombea mpaka akatolewa gerezani.
Unaweza
ukajiuliza kwani kuna umuhimu gani wa kuwa na watu wa
kukuombea?..............................Ni muhimu uwe na watu wa kukuombea kwa
kuwa kuna wakati huwa inafika hatua muda wa kuomba unapungua, kiu ya kuomba
inapungua, mazingira hayakuruhusu kuomba n.k kwa hiyo kuna umuhimu wa kupata
watu wa kuomba kwa ajili yako, njia mojawapo ya kupata watu wa kukuombea ni
kufanyika Baraka katika maisha ya watu wengine.
2.Utakuwa mtu wa kutamkiwa Baraka badala ya
laana (you’ll be blessed instead of being cursed).
Huduma
ambayo Yesu aliifanya wakati akiwa hapa duniani iligusa maisha ya watu wengi
sana hata ilifika hatua mwanamke mmoja akamwambia Yesu “libarikiwe tumbo
lililokuzaa na matiti uliyonyonya (Luka 11:27).
3.Utaheshimiwa (you’ll be hanoured)
Kuna watu
wanadharauliwa kwa sababu uwepo wao hauna faida yoyote, jaribu kutazama familia
zingine utakuta baba wa familia hana heshima kwa kuwa hawajibiki kama baba wa
familia.
Ninachotaka
uone hapo ni kwamba kitu mojawapo kinachotengeneza heshima ni faida wanayoipata
watu ukiwepo, kama uwepo wako hauna faida yoyote basi kudharauliwa litakuwa ni
fungu lako.
Unaweza
ukawa na elimu kubwa kuliko watu wote katika jamii, kanisa na familia yako
lakini kama uwepo wako hauna faida basi tarajia kudharauliwa.
Hivi
umeshawahi kujiuliza kwa nini watu wenye fedha hususani wanaotoa fedha zao kwa
ajili ya mambo fulani wanaheshimika hata kama wana umri mdogo, ni kwa sababu
uwepo wao una faida katika maisha ya watu.
(Wafilipi
2:5-11)
Yesu
alifanyika Baraka kwetu kwa kuwa alikubali kufa kwa ajili yetu, uwepo wake
katika dunia ulikuwa wa baraka sana alipokamilisha kazi aliyokuja kuifanya alikirimiwa
JINA lipitalo majina yote ni sawa na kusema alipewa heshima kubwa sana.
Ninachotaka
uone hapo ni kwamba uwepo wako unapokuwa na faida heshima itakuwa fungu lako.
4.Thamani yako inaongezeka (your value will
increase)
Mbinu
mojawapo ya kuongeza thamani yako ni kuhakikisha uwepo wako unakuwa na faida,
uwepo wako ukiwa na faida utajikuta thamani yako inaongezeka, watu watatamani
usiondoke, watu watatamani wakusikie, watu hawapata amani pale itakapotokea
umepatwa na shida Fulani n.k.
(Mwanzo
39:1-6)
Tunaona
Yusufu alipoingia kwenye nyumba ya potifa, nyumba ya Potifa ilianza kubarikiwa
hata shamba la Potifa likabarikiwa kwa sababu ya Yusufu.
Uwepo wa
Yusufu katika nyumba ya Potifa ulikuwa wa Baraka sana kwenye nyumba ile,
thamani ya Yusufu iliongezeka sana ikafika hatua Potifa akamkabidhi Yusufu kila
kitu akisimamie isipokuwa mke wake (mke wa Potifa).
Hapa nataka
nikuulize wewe ambaye umeajiriwa, je! Uwepo wako una faida gani kwenye hiyo
ofisi, kampuni au taasisi?
Je! Toka
umeajiriwa umeshafanya mambo gani mazuri kwenye hiyo ofisi?
Kama uwepo
wako hauna faida uwe na uhakika siku ikitokea kampuni hiyo au taasisi hiyo
ikataka kupunguza wafanyakazi na wewe unaweza kujikuta umeondolewa kazini kwa
kuwa uwepo wako hauna faida yoyote yaani hata usipokuwepo kampuni au taasisi
haiwezi kupata hasara au tatizo lolote. Kama uwepo wako una faida hata wakitaka
kukuaachisha kazi lazima utapata watetezi watakaosababisha usiondolewe kazini.
0 Maoni