UPI NI MTINDO HALALI WA KUTUMIA KATIKA HUDUMA YA UIMBAJI MAKANISANI



Na Mwl. Faraja Gasto

Hili ndilo swali ambalo linasumbua kanisa la leo na hata imefikia hatua migogoro inatokea kati ya waimbaji na viongozi wa makanisa  kuhusu mitindo ya nyimbo wanayotumia waimbaji na pia imesababisha vipawa vingi vya uimbaji kufa na hata waimbaji wengine wakahamishia vipawa vyao kuimba nyimbo zisizoleta utukufu kwa Mungu(waimbaji kuacha kuimba nyimbo za injili na kuimba nyimbo za kidunia).

Kanisa linapata shida kwa sababu ya mitazamo hasi iliyojengeka ndani ya kanisa kwa muda mrefu juu ya uimbaji kwa mfano makanisa mengi kama si yote yanapotaka kumualika muimbaji huwa yanaangalia mtindo uliotumika kuimba nyimbo hizo kuna makanisa mengine  nyimbo ambazo zimeimbwa kwa mitindo kama vile ya kurap(HipHop),(RnB),(sebene),(Rege) n.k ni dhambi kwao na si ajabu usipewe nafasi ya kuimba hata kama nyimbo hizo zimebeba ujumbe mzuri lakini si kweli kwamba dhambi iko ndani ya mtindo wa wimbo husika bali dhambi ni kita nafasi ndani ya mtu  kama akiiruhusu.

Kama tusomavyo kwenye  neno la Mungu(Biblia) kuwa uimbaji umekuwepo toka mbinguni lakini neno la Mungu halisemi mbinguni ni mtindo gani wa uimbaji unaotumika na hata vizazi vilivyotutangulia tunasoma kwenye Biblia kuwa vilimuimbia Bwana lakini Biblia haisemi waliimba kwa kutumia mtindo gani wa uimbaji lakini kwa wakati huohuo Mungu anatuagiza kuwa tumwimbie kwa hiyo kumbe hata MUNGU haangalii mtindo wa wimbo.
                  
                 Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Na sifa zake tokea mwisho wa dunia;  Ninyi mshukao baharini, na vyote vilivyomo, Na visiwa, nao wakaao humo. (Isaya 42:10)

Ili tujue mtindo ambao ni halali kutumika makanisani kwa ajili ya huduma ya uimbaji hebu turudi kwenye historia kuhusu uimbaji kwa mujibu wa Biblia

Tunaposoma Biblia tunaona mtu wa kwanza kuelezewa kwenye Biblia kuwa wa kwanza kwenye masuala ya upigaji wa muziki alikuwa anaitwa YUBALI mtoto wa Lameki na huyo Lameki alikuwa akitoka kwenye ukoo wa KAINI kwa hiyo mpiga vyombo wa kwanza alitoka kwenye ukoo wa KAINI mtoto wa Adamu ila hatuambiwi alikuwa akipiga muziki wa aina gani.
                    Lameki akajitwalia wake wawili, jina la wa kwanza ni Ada, na jina la wa pili ni Sila. Ada akamzaa Yabali; huyo ndiye baba yao wakaao katika hema na kufuga wanyama.21  Na jina la nduguye aliitwa Yubali; huyo ndiye baba yao wapigao kinubi na filimbi. 22 Sila naye akamzaa Tubal-kaini, mfua kila chombo cha kukatia, cha shaba na cha chuma; na umbu lake Tubal-kaini alikuwa Naama.  (Mwanzo 4:19-22)
Na pia tunaposoma neno la Mungu tunaona kuwa baada ya Mungu kuwatoa wana wa Israeli utumwani kutoka katika nchi ya Misri tunaona wana wa Israeli wakimtukuza Mungu kwa jinsi alivyowavusha katika Bahari ya Shamu lakini hatujui ni mtindo gani walioutumia kumsifu Mungu.
                 Ndipo Musa na wana wa Israeli wakamwimbia Bwana wimbo huu wakanena, na kusema, Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana; Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini. (Kutoka 15:1)
              Na Miriamu, nabii mke, ndugu yake Haruni, akatwaa tari mkononi mwake; wanawake wakatoka wote wakaenda nyuma yake, wenye matari na kucheza.  (Kutoka 15:20)
Wana wa Israeli walitoka utumwani Misri walikokaa kwa muda wa miaka 450 hivyo hata mtindo waliotumia kumsifu Mungu ulikuwa wa kiMisri kwa kuwa wote waliotolewa utumwani walizaliwa pale Misri kwa hiyo hata kuimba kwao walimsifu Bwana kwa mtindo waliouzoeaa kutoka katika nchi ya Misri kwa kuwa ni muda mrefu sana waliokaa na hakuna mahali ambapo Mungu aliwazuia kumwimbia kwa mtindo huo wa liouzoea kutoka MISRI na pia uimbaji wa wana wa Israeli ulikuwa ukubadilika kutokana mabadiliko ya kizazi kimoja mpaka kingine kwa kuwa walikuwa wakichukuliwa utumwani kwenda sehemu mbalimbali walikokuwa wakizoea hata uimbaji wa aina tofauti tofauti kwa hiyo hata uimbaji wao ulienda ukibadlika ndio maana ukienda leo au ukisikiliza nyimbo za wayahudi wa sasa ni tofauti kabisa na zile za zamani.
Uimbaji katika agano la kale ulitegemea na taifa husika kwani kila taifa lilikuwa na mtindo wake wa uimbaji ndio maana wana wa Israeli walipochukuliwa mateka katika nchi ya Babeli tunasoma katika Biblia kuwa watu wa Babeli walishangaa sana mtindo walioutumia wana wa Israeli kumwimbia Bwana hivyo wakawalazimisha wawaimbie nyimbo zao lengo lilikuwa si kusikia jinsi wanavyomsifu MUNGU wao bali lengo lilikuwa kusikia ule mtindo waliokuwa wakiutumia katika uimbaji wao.
                 Kando ya mito ya Babeli ndiko tulikoketi, Tukalia tulipoikumbuka Sayuni. 2 Katika miti iliyo katikati yake Tulivitundika vinubi vyetu.3Maana huko waliotuchukua mateka Walitaka tuwaimbie; Na waliotuonea walitaka furaha; Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni.  (Zaburi 137:1-3)
Mtindo wa uimbaji unategemea sana ni chombo kipi kinachotumika kwa kuwa kila chombo huwa kinauwezo wa kuzalisha aina Fulani ya mtindo wa muziki. Hapo zamani kulikuwa na vyombo tofauti na tunavyotumia leo kwa hiyo mtindo wa uimbaji ulitegemea sana chombo kiliweza kuzalisha aina gani ya muziki, kwa hiyo watakatifu wa MUNGU waliimba kutokana na mtindo uliozalishwa na vyombo walivyvitumia katika kuimba.
BAADHI YA MITINDO YA UIMBAJI AMBAYO NI MAARUFU ILIYOTOKEA KARNE YA KUMI NA TISA(19) NA AMBAYO INATUMIKA KATIKA HUDUMA YA UIMBAJI
Tunapoiangalia karne ya kumi na tisa ndio karne ambayo imechangia kuleta mitazamo tofautitofauti kwenye tasnia ya uimbaji kwa kuwa katika karne hiyo mitindo mingi ya uimbaji ilitambulishwa duniani kama vile RnB(Rhythm and Blues) , Rock, HipHop(muziki wa kufoka au kurap),Reggae(Rege), Quito(kwaito),Blues(muziki wa taratibu), muziki wan chi(Country music) n.k hii ni baadhi ya mitindo ambayo inatumiwa na waimbaji wa nyimbo za injili bila kujali makanisa waliyopo.

Muziki wa HipHop (muziki wa kurap/kufoka)
Ni aina ya muziki ulioanza kunako miaka ya 1970, ukiwa umeanzishwa na Wamarekani weusi katika miji mikubwa ya Marekani. Hip hop mara nyingi inatumia staili moja ya kuimba iitwayo kurap au kufokafoka.Kurap ni staili ya uimbaji ambayo mwimbaji anatoa au anaimba maneno-mashairi yaambatanayo na vina. Mashairi mengi yaliyoimbwa katika muziki wa hip hop yalikuwa yakizungumzia maisha halisi ya watu weusi wa nchini Marekani, sanasana katika miji mikubwa.
Julai 23 mwaka 2007, Jiji la New York, lilitangaza rasmi kuitambua 1520 sedgwick Ave iliyoko Bronx kuwa sehemu ambayo hip hop ilizaliwa. “1520 sedgwick  Avenue ni sehemu ambayo Recreation Room, chumba alichokitumia muasisi wa hip hop, Dj Cool Herc.  August 11, 1973, ndiyo tarehe ambayo hip hop ilizaliwa kwa mujibu wa Cindy Campbell ambaye ni dada yake na Dj Kool Herc. Onesho la kwanza la hip hop lilifanyika siku hiyo. Onesho hilo liliandaliwa na
Dj Kool Herc kwa lengo la kuchangisha pesa ili dada yake (Cindy Campbell) aweze kurudi shule (back to school party). Herc alikodisha recreation room kwa dola ishirini na tano za kimarekani na kiingilio ilikuwa ni thumni (cent) 25 kwa wanawake na thumni 50 kwa wanaume. Herc alikuwa kwenye mashine na msema chochote (mc) wa siku hiyo alikuwa ni dada yake (cindy), tukio hili ndilo linalomfanya cindy Campbell kuwa mwanamke wa kwanza katika hip hop (first lady of hip hop).


Muziki wa Rege
Ni aina ya muziki kutoka nchini Jamaika. Ulianzishwa tangu 1968 na ulitambulishwa duniani kwa mara ya kwanza na Robert Nesta "Bob" Marley (6 Februari 1945 - 11 Mei 1981) alikuwa mwimbaji na mwanamuziki kutoka nchini Jamaika. Alivuma hasa kunako miaka ya 1970 na 1980. Ameweza kuifanya staili ya muziki wa reggae kuwa maarufu sana duniani. Muziki wake mwingi ulikuwa unazungumzia hadithi za nyumbani kwake na dini ya Rastafari ambayo yeye alikuwa anaifuata. Kuna baadhi ya nyimbo zake zinahusu masuala ya dini na zingine siasa.

Muziki wa kwaito (muziki wa kafrika kusini)
Ni aina ya muziki uliotambulishwa duniani na Miriam Makeba ambaye alizaliwa tarehe 4 Machi 1932 katika jiji la Johannesburg, Afrika Kusini. Miriam alikuwa ni mwanamuziki pekee wakati huo aliyeweza kufanikiwa kuzieneza nyimbo zenye asili ya Kiafrika. Pia alikuwa ni miongoni mwa wanamuziki waasisi wa kuchanganya mitindo tofauti ya muziki na kutengeneza muziki wa kuvutia kama Kwaito.

Muziki wa dansi (Bendi)
Muziki ulianzishwa kunako miaka ya 1920-1930, zikiwa na mandhari ya muziki wa "soukous" kutoka Kongo-Kinshasa,

Muziki wa Taarab
Ni aina ya muziki ya Afrika ya Mashariki yenye asili yake katika utamaduni wa Waswahili. Neno lenyewe limetokana na Kiarabu "tarab" (طرب) linalomaanisha "uimbaji/ wimbo". Muziki huu uliingia pwani ya Afrika Mashariki ukitokea nchini Misri.

Muziki wa RnB(Rhythm na blues )
Ni aina ya muziki uliomaarufu, ambao umejumlisha muziki wa jazz. Kwa mara ya kwanza, muziki huu ulikuwa ukiimbwa na wasanii Waamerika Weusi. Lakini baadaye ulipendwa na watu wengi na kufikia hata kutumika na makundi na tamaduni za watu mbalimbali duniani.

Muziki wa Taratibu (blues)
Ni aina ya muziki ambao ulianzia nchi Marekani mwanzoni kabisa mwa karne ya 20 na ulitambulishwa duniani na mwanamama Bessie Smith. Uliazishwa na watumwa wa zamani wa Kiafrika waliokuwa wakiimba nyimbo za kiroho.

Muzikiwa Bongo Fleva
Ni mtindo wa muziki unaopendwa sana miongoni mwa vijana wa Tanzania. Mtindo wake unahusiana na mtindo wa kufoka/kurap na ule wa taratibu(American hip hop na R&B). Mtindo huu ulibuniwa miaka ya 1990, kama mchanganyiko wa American hip hop na nyongeza ya athari kutoka kwenye rege, R&B, afrobeat, dancehall na mitindo ya kiasili ya Kitanzania kama vile taarab na ngoma za asili.

MTINDO AMBAO NI HALALI WA KUTMIA KATIKA HUDUMA YA UIMBAJI

Mtindo wowote ule ni halali kutumika kwenye huduma ya uimbaji maadamu tu katika kuimba kwa mtindo huo shetani hapewi utukufu kwa namna yoyote bali MUNGU pekee.
Kama ambavyo tumeona kuwa kila taifa huwa lina mtindo wake wa uimbaji na kupitia mitindo hiyo watu katika taifa husika hutumia kumsifu, kumwabudu, kuhubiri na pia kumshukuru MUNGU wa mbingu na nchi na MUNGU huzipokea sifa hizo kwa hiyo haipendezi kwa kanisa la MUNGU kuwaweka waimbaji kwenye kifungo cha kutotumia baadhi ya mitindo ya uimbaji kwa kigezo kuwa mitindo hiyo ni ya kihuni jambo ambalo si kweli kwani MUNGU ni MUNGU wa mataifa yote.
         Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, 10  ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi
(Ufunuo 5:9-10)

Chapisha Maoni

0 Maoni