Namna ya kuweka vipaumbele




a).Lazima uangalie umuhimu wa hicho unachotaka kukifanya.
(Mwanzo 1:1) “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi”. Mungu alipoanza kuumba alianza kuumba vitu vyenye umuhimu kuliko vingine vyote ndio maana akaanza na mbingu na ardhi ndivyo vilivyokuwa na umuhimu kuliko vyote alivyotaka kuviumba ndio maana akaanza na hivyo.
Jaribu kufikiri mtu anahitaji kujenga nyumba halafu akaanza kwa kununua matofari kabla ya kununua kiwanja ambacho atakitumia kujenga nyumba, ni kweli matofari ni ya muhimu katika ujenzi lakini kiwanja ni cha muhimu kuliko matofari kwa kuwa matofari ukiyaacha kwa muda mrefu yanaweza kuharibika lakini kiwanja hakiwezi kuharibika kwa kuwa kiwanja ni mali isiyohamishika(fixed asset) lakini matofari) ni mali inayohamishika, mtu anayepanga kujenga akianza kununua matofari kabla ya kiwanja atakuwa hajajua namna ya kuweka vipaumbele.

b)Lazima uzingatie uwezo wako
(Waamuzi 6:14) Bwana akamtazama, akasema enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli na mkono wa Midiani . Je! si mimi ninayekutuma?
Ukisoma hiyo habari utaona wana wa Israeli walipomlilia Mungu kwa sababu ya mateso waliyokuwa nayo kutokana na walivyoteswa na wamidiani, Mungu alimwambia Gideoni aende kuwaokoa wana wa Israeli kwa UWEZO ule aliokuwa nao, lengo lilikuwa kujinasua kutoka kwenye mkono wa wamidiani, Mungu alipomtazama Gideoni akaona ana uwezo ambao anaweza kuutumia kufanyia mambo mbalimbali ndio maana alimwambia aende kwa uwezo huu maana yake ni kwamba ule uwezo aliokuwa nao umsaidie kuweka vipaumbele katika kazi iliyokuwa mbele yake ya kupambana na wamidiani na ndio maana kabla ya kupigana na wamidaini Gideoni aliambiwa avunje madhabahu ya mungu Baali iliyokuwa inasimamiwa na baba yake mzazi na baada ya hapo amjengee Bwana madhabahu kwa taratibu zake(Waamuzi 6:25-26) kwa sababu Mungu alijua hayo ni mambo ambayo yapo kwenye UWEZO wake ndio maana ya Mungu kumwambia aende kwa uwezo huu. Kumbuka lengo lilikuwa kujinasua kutoka kwenye utumwa wa wamidiani lakini vipaumbele vilikuwa ni; kuvunja madhabahu ya mungu Baali na kujenga madhabahu ya Bwana, baada ya hapo alitakiwa kuandaa jeshi ambalo litatumika kupigana na wamidiani na baada ya hapo walitakiwa kufuata maelekezo ya Mungu juu ya vita iliyokuwa mbele yao.
Unapoweka vipaumbele lazima uangalie uwezo wako, ni kipi unaweza kukifanya, Mungu alipomuambia Gideoni aende kwa uwezo aliokuwa nao, Mungu alijua kuwa kile alichomuambia Gideoni kimo ndania ya uwezo wake yaani anaweza akakifanya.
Kosa ambalo watu wengi hulifanya ni kutaka kufanya mambo zaidi ya uwezo wao na hatimaye malengo ya wengi yameishia kutotimia.


c).Lazima ujifunze kutumia akili ipasavyo
(1 wakorintho 15:34a) “Tumieni akili ipasavyo”. Kosa ambalo watu wengi wanalifanya ni kutotumia akili zao kama inavyowapasa, kazi mojawapo ya akili ni kukufanya ufikiri juu ya ubora au viwango unavyovitaka juu ya kile ambacho unataka kufanya, watu wengi wamejikuta wanafanya mambo chini ya kiwango kwa kuwa hawatumii akili vizuri bali wanatumia hisia katika kufikiri badala ya kutumia akili katika kufikiri.
(Mithali 3:19b) “Kwa akili zake akazifanya mbingu imara” biblia inatupa kufahamu kuwa wakati Mungu anaumba alitumia akili na kutokana na matumizi ya akili akaumba mbingu IMARA, biblia inapozungumza kwa habari ya uimara wa mbingu biblia inazungumzia UBORA wa mbingu, wote tunafahamu na tunaona jinsi mbingu zilivyowekwa bila nguzo ni kwa sababu Mungu alitumia akili sana katika kuumba ndi maana akaumba kitu imara au kitu bora.
Ni vema kila mtu afahamu kuwa jambo mojawapo linaloamua ubora wa kitu au kitu kifanyike kwa viwango gani ni akili ya mtu na ndio maana hata mashuleni au vyuoni wanafunzi wanofaulu vizuri(the best) ni wanafunzi wanaoutumia akili zao vizuri, kumbuka huwezi kutumia akili zako vema halafu ukakosa vipaumbele, wanaotumia akili ndio watu wanofanya mambo kwa ubora au katika viwango vikubwa lakini kwa watu wasiotumia akili huwa wanafanya mambo bila kufikiri na huwa wanafanya mambo chini ya kiwango.

Chapisha Maoni

0 Maoni