Na Mwl.Dorcas Simon
Evangelical Holy Pentecostal Church of Tanzania(Mwanza)
UTANGULIZI
Dhahabu
iliyo safi ni ile iliyopitishwa motoni maana yake ni Mkristo anayestahili kuingia Mbinguni ni Yule aliyepitishwa kwenye
majaribu.
Siku
zote mtu hujaribiwa kwa vitu anavyovijua kwa kuwa hakuna kitu kipya duniani.
MGAWANYIKO WA SOMO
Somo hili limegawanyika katika
sehemu kuu tatu
v Majaribu
yanayotolewa na MUNGU.
v Majaribu
yanayotolewa na shetani.
v Majaribu
yanayosababishwa na mtu mwenyewe.
Msitari wa kukumbuka: (Zaburi
34:19)
‘’Mateso ya mwenye haki ni
mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote’’.
Kweli kuu ya somo: (1
Wakoritho 10:13)
‘’Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila
Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja
na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili’’.
MAJARIBU: Ni vipindi tofauti
ambavyo ni vigumu, vinavyoleta shida, dhiki, tabu n.k
Siku zote jaribu huwa
haliangalii tajiri au maskini bali jaribu linaweza likampata mtu yeyote.
Japo majaribu ya aina hizi tatu
yanaweza kufanana lakini matokeo yake huwa ni tofauti.
Mtu yeyote ambaye ameokoka
haijalishi ni tajiri au maskini wakati wake ukifika lazima ajaribiwe tu kwa mfano mtu akiwa na mali jaribu linaweza
likaja kupitia ndugu zake wakamuinukia au mke wake anaweza akamuinukia na hivyo
akawa jaribu kwake. Mtumishi wa MUNGU Yakobo japo alikuwa ni tajiri sana lakini
alikiri kuwa siku zake zote zilikuwa za taabu.
Yusufu akamleta Yakobo babaye ndani akamweka mbele ya Farao Yakobo
akambariki Farao, Farao akamwuliza Yakobo, Je! Siku za miaka ya maisha yako ni
ngapi? Yakobo akamjibu Farao, Siku
za miaka ya kusafiri kwangu ni mia na thelathini; siku za miaka ya maisha yangu zimekuwa chache, tena za taabu, wala
hazikufikilia siku za miaka ya maisha ya baba zangu katika siku za kusafiri
kwao.(Mwanzo 47:7-9)
JAMBO LA KUELEWA: Watu wengi
wanapopitia kwenye jaribu Fulani huwa wanakosa hekima ya kupambanua kipi ni
chanzo cha jaribu wanalolipitia Je ni
jaribu lililoruhusiwa na MUNGU?
Je ni jaribu lililoachiliwa na shetani?
Je ni jaribu lililosababishwa na mtu mwenyewe?
JINSI YA KUPAMBANUA CHANZO CHA
JARIBU
v Jaribu linaloachiliwa na MUNGU huwa
linamvuta mtu achukue hatua za kumtafuta BWANA na huwa halipiti uwezo wa mtu
kulistahimili au kulivumilia.
v Jaribu linaloletwa na shetani huwa
linakuja na msukumo wa kuchukua maamuzi ya haraka sana na mwishowe mtu hujikuta
amemtenda MUNGU dhambi kwa mfano shetani alimtumia mke wa Ayubu ili ampate
Ayubu, mke wa Ayubu alimwambia Ayubu mkufuru MUNGU ufe lakini Ayubu alikataa,
kitu alichokuwa anakitaka shetani ni kumfanya Ayubu atoe maamuzi ya kumkufuru
MUNGU mwishowe afie dhambini.
v Jaribu linalosababishwa na mtu mwenyewe
huwa linasababishwa na tama juu ya kitu Fulani na kutokana na tama hiyo mtu
hujikuta katika shida.
Japo kuna neema kidogo kwa
baadhi ya watu na neema hiyo huwafanya wasipitie jaribu la aina yoyote kwa
mfano mtu amemkiri YESU na baada ya hapo akafariki hivyo basi moja kwa moja
roho ya mtu huyo huenda mbinguni na mtu huyo anakuwa hajapitia jaribu la aina
yoyote.
OMBI LETU SISI: Mungu usitutie
majaribuni (Mathayo 6:9-13) (Luka 11:2-4). YESU alipowafundisha wanafunzi wake
kuwa wamwombe MUNGU asiwatie majaribuni alikuwa anamaanisha kuwa shetani naye
huleta majaribu hivyo wamwombe MUNGU asiruhusu wapiti majaribu yanayoletwa na
adui yetu shetani.
Wakati Fulani MUNGU alimtoa
Lutu katika eneo ambalo adhabu ilikuwa imeamriwa (Sodoma na Gomora) kwa sababu
Lutu alikuwa mtu mwenye haki hivyo tunajifunza kuwa mahali Fulani wakiwepo watu
wenye haki watu wa eneo hilo huwa wanapata neema kupitia wenye haki hao.
KWELI
KUU YA SOMO
(1 Wakorintho 10:13-22)
Wakorintho walipojaribiwa
waliona jaribu lile kuwa kubwa kupita uwezo wao wa kustahimili/kuvumilia lakini
Mtume Paulo aliwaandikia waraka kuwa jaribu wanalopitia lilikuwa la kawaida na
ndilo lilikuwa la uwezo wao na wangeweza kulistahimili.
MTAZAMO POTOFU WALIONAO
WAKRISTO JUUYA MAJARIBU
Wakristo wengi wana mtazamo
potofu juu ya majaribu kwani wengi hudhani jaribu ni lile linalochukua muda
mrefu jambo ambalo si kweli kwani jaribu linaweza likachukua sekunde kadhaa,
dakika, masaa, siku ,mwezi/miezi na hata mwaka/miaka.
Yusufu aliingia kwenye jaribu la
kufanya uasherati na mke wa bwana wake (his boss’s wife) kwa dakika kadhaa na
akalishinda jaribu hilo.
SEHEMU
YA KWANZA
MAJARIBU YANAYORUHUSIWA NA
MUNGU
Mungu anaporuhusu jaribu Fulani
huwa lina muda wa kuanza na wa kuisha na ule muda wa kuisha jaribu ndio ambao
huitwa mlango wa kutokea kwenye jaribu.
Wakati wa Mungu kumtoa mtu
kutoka kwenye jaribu ukifika hata kama mtu huyo alikuwa amekata tama Mungu huwa
anaachilia msukumo kwa mtu huyo ili aanze kumtafuta Bwana na baada ya hapo
Mungu humtoa mtu huyo kutoka kwenye jaribu hilo.
Kama Mungu ameruhusu jaribu
limpate mtu kwa muda Fulani ikiwa muda huo haujafika mtu huyo hawezi kutoka
kwenye jaribu hilo hata afannye nini lakini Mungu mwenyewe ndiye ambaye humtoa
mtu huyo kwenye jaribu hilo.
(1 Wakorintho 10:13-22)
Wakorintho walipotafuta njia ya kujitoa kutoka kwenye jaribu walijikuta
wameangukia kwenye ibda ya sanamu.
SWALI
LA KUJIULIZA: Je unapojua jaribu limetoka kwa Bwana huwa unalipokeaje?
‘’Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika
majaribu mbalimbali;(Yakobo 1:2)
Wewe
kama mkristo unapojaribiwa lazima ulipokee jaribu kwa furaha hata kama
linaumiza kwa kuwa ukilipokea jaribu kwa uchungu hata maombi yako yatakuwa ya
uchungu na utamwona Mungu kama amekuonea.
LENGO LA MUNGU KUACHILIA
MAJARIBU
Mungu anaporuhusu majaribu huwa
ana malengo au makusudi matatu makuu.
v Anataka
kuiona imani yetu.
v Anataka
kuona upendo wetu kwake.
v Anataka
kuona uvumilivu wetu.
MUNGU
HUTAKA KUONA IMANI YETU
(1 Petro 1:6-9) (Kutoka 15:1 ) (Kutoka 16:1 )
Wakati wana wa Israeli wanatoka
Misri kwenda Kanaani ilikuwepo njia ya karibu ambayo ingewafanya kufika mpema
Kanaani lakini Mungu aliwapitisha njia ya kwenye jangwa ili aione imani yao juu
ya majaribu aliyoyaruhusu ya wapate lakini mara zote walipokosa nyama, maji n.k
waliishia kumnung’unikia Musa na Mungu, hivyo basi wana wa Israeli walikuwa
watu wa tabia ya mwilinikwani walitanguliza hasira na mitazamo potofu dhidi ya
Musa na Mungu hivyo waliishia kunung’unika na mwishowe wengi waliangamizwa kwa
kuwa walipopitia majaribu walisahau kuwa ni Mungu aliyeigawanya Bahari ya Shamu
wakavuka.
Hivyo nasi twatakiwa kujifunza
kuwa tunapopitia majaribu mbalimbali tusiwe wepesi kumnung’unikia Mungu bali
tunatakiwa tukumbuke mambo ambayo Mungu alikwisha kutufanyia na mwisho tujenge
imani kwa Mungu na tusonge mbele kumwamini Mungu.
MUNGU
HUTAKA KUONA UPENDO WETU KWAKE
Ikawa baada ya mambo hayo
Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi
hapa.Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende
zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima
mmojawapo nitakaokuambia.Ibrahimu akaondoka alfajiri, akatandika punda wake,
akachukua vijana wawili pamoja naye, na Isaka mwanawe, akachanja kuni kwa ajili
ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka, akaenda mpaka mahali alipoambiwa na
Mungu.(Mwanzo 22:1-3)
Mungu alikuwa hamhitaji Isaka
bali Mungu alikuwa anataka kuona upendo wa Ibrahimu dhidi yake.
SWALI
LA KUIJULIZA: Je pale ambapo Mungu anatujaribu kwa kumtaka Isaka wetu au Mungu
anapotujaribu juu ya yale mambo tunayoyathamini je huwa tunaonyesha kumpenda
Mungu tu au?
MUNGU
HUTAKA KUONA UVUMILIVU WETU
Tunajifunza kwa mtu wa Mungu
Ayubu pale alipojaribiwa alionyesha kuwa yeye ni mvumilivu na mwishowe Mungu
alimbariki maradufu.
Hata katika maombi yetu
tunatakiwa kuwa wavumilivu sana kwa sababu wakati mwingine Mungu huwa anaacha
kujibu kwa makusudi ili aone uvumilivu wetu.
Akawaambia mfano, ya
kwamba imewapasa kumwomba Mungu
sikuzote, wala wasikate tamaa. Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji
fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. Na katika mji huo palikuwa
na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui
wangu. Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake,
Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu
ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima. Bwana
akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu. Na Mungu, je! Hatawapatia
haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu
kwao? Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa
Adamu, je! Ataiona imani duniani? (Luka 18:1-8)
AMBACHO HUTOKEA PALE WATU
WANAPOINGIA MAJARIBUNI
Watu wengi wanpokuwa katika
vipindi vya majaribu huwa wanamtenda Mungu dhambi kama vile wana wa Israeli
walivyokuwa wakimtenda Mungu dhambi kutokana na majaribu ndivyo ilivyo hata leo
kwani watu wengi humtenda Mungu dhambi pale wanapoingia kwenye majaribu kwa
mfano utakuta mtu ameingia katika jaribu la kukwama kiuchumi na inafika hatua
mpaka watoto wake wanashindia uji tu utakuta mtu huyo anakwenda kuomba msaada
kwa jirani yake ili apewe unga kwa kusudi la kuwapikia watoto wake na akifika
kwa jirani utakuta anamwambia kuwa watoto wake walilala njaa lakini kumbe
walilala wamekunywa uji hivyo mtu huyo anakuwa tayari ametenda dhambi ya uongo
akiwa kwenye jaribu.
Kwa mfano mtu anakwenda dukani
na inatokea muuzaji anamzidishia pesa yaani unakuta mtu anakwenda dukani akiwa
na shilingi 500/= na ananunua kitu cha shilingi 300/= na muuzaji kwa kujisahau
anamrudishia shilingi 2000/= kwa kudhani kuwa alipewa shilingi 5000/= na
utakuta watu wengi wanachukua pesa isiyo yao kwa kudai kuwa ni Mungu
aliwanyooshea mkono wapate Baraka hiyo hivyo wanakuwa wametenda dhambi ya wizi.
Tunatakiwa kujifunza kwa YESU
kwa kuwa yeye alijaribiwa katika mambo yote lakini hakutenda dhambi.
‘’Kwa kuwa hamna kuhani
mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye
alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi’’. (Waebrania
4:15)
MAJARIBU
KATIKA HUDUMA
Mungu anaweza kuliachilia au
kuruhusu jaribu limpate mtu akiwa
anajiandaa kuingia kwenye huduma au uongozi au akiwa kwenye huduma au nafasi ya
uongozi.
USHUHUDA: Mchungaji mmoja aliyekuwa
anamtumikia Mungu chini ya dhehebu Fulani ,Mungu alimpa kazi ya kwenda kuchunga
kanisa Fulani lililokuwa chini ya huduma hiyohiyo aliyokuwepo Mchungaji huyo na
alipokwenda katika kanisa hilo waumini waliokuwa kwenye kanisa hilo walimkataa
kuwa hastahili kuwachunga na ikatokea alipokuwa akiingia madhabahuni kuhudumu
watu wanamvuta atoke madhabahuni na kwa unyenyekevu aliokuwa nao Mchungaji Yule
alikaa nay eye kama muumini wa kawaida hku akizidi kumwomba Mungu na kutokana
na uvumilivu wake siku moja waumini hao walipatwa na maradhi mabaya sana na
walipoingia kuomba mbele za Bwana, Bwana aliwaambia waende kwa Mchungaji Yule
waliyemkataa asiwe Mchungaji wao ili awaombee wapone na walipokwenda kuombewa
na Mchungaji huyo Mungu aliwaponya na ndipo walipojua hakika Mungu amempa kazi
ya kuwachunga na tokea wakati huo Mchungaji huyo aliendelea kuwachunga.
(1 Samweli 18:6-16)
Daudi alipitia majaribu
mbalimbali na jaribu lake la kwanza lilianza baada ya yeye kumuua Goliathi.
Majaribu
aliyopitia Daudi
v Jaribu
la kuwindwa na Mfalme Sauli ili auawe.
v Jaribu
la kutaka kupinduliwa kwenye ufalme wake, jaribu lililopitia kwa mtoto wake
Daudi ambaye ni Absalomu.
v Jaribu
la kunenewa mabaya.
(a) Jaribu la kutaka kuuawa.
Baada ya Daudi kumuua Goliathi
na wanawake wakamshangilia ilijenga chuki ndani ya Mfalme Sauli na akaanza
kutafuta nafasi ya kumuua Daudi kwa kuwa Mfalme Sauli aliona kuwa Daudi ndiye ambaye
atakuja kupewa ufalme hivyo akaamua kumtafuta Daudi ili auawe.
Lakini Daudi alipomkimbia
Mfalme Sauli ilifikia hatua Daudi akiwa na kundi lake walifanikiwa siku moja
kukuta Sauli na jeshi lake wakiwa wamelala mahali usiku na Daudi alikataa
kumuua Mfalme Sauli kwa kuwa Daudi alisema Sauli ni mpakwa mafuta wa Bwana hivyo
aliacha kumuua.
JAMBO
LA KUJIFUNZA: Je Mungu anapokuwekea adui yako mbele yako au atakapokuwekea adui
yako mbele yako utamfanya nini huyo adui yako?
Tunatakiwa kuwa na moyo kama wa
Daudi kwani Mungu alipomuweka adui mikononi mwake Daudi alijua ule haukuwa
wakati sahihi wa kumuua adui yake bali Dauidi alimwachia Bwana mwenyewe ili
ampiganie.
(b) Jaribu la kutaka
kupinduliwa kwenye ufalme wake.
(2 Samweli 15:1-18) Ilifikia
hatua mtoto wa Daudi ambaye aliitwa Absalomu alimwinukia baba yake na akataka
kumpindua kwenye ufalme ili amiliki yeye, japokuwa Daudi alikuwa na jeshi
ambalo lingweza kumdhibiti mwanaye lakini Daudi aliamua kumkimbia mwanaye na
mwanaye alipokufa Daudi alilia sanasana mpaka wanajeshi wake walimshangaa sana.
(c) Jaribu la kunenewa mabaya.
(2 Samweli 16:5-8) Mfalme Daudi
alipitia jaribu hili la kunenewa mabaya(kutukanwa) japokuwa Mfalme Daudi
alikuwa na jeshi ambalo lingeweza kumuangamiza mtu Yule aliyekuwa akimtukana
lakini Mfalme Daudi alinyamaza kimya tu.
Unaweza ukwa kwenye huduma au
ukawa uko kwenye nafasi ya uongozi na watu wanakunenea mabaya hata kama watu
hao una uwezo wa kuwadhibirti hebu mwachie Mungu akutetetee kinyume na watu hao
hautakiwi kuacha huduma.
Majaribu
aliyopitia Nabii Yeremia
(Yeremia 38:1-13) Nabii Yeremia
alipitia majaribu mbalimbali kama vile
(a) Kutosikilizwa.
(b) Kutupwa kwenye shimo la
matope.
Majaribu
aliyopitia Yusufu
v Jaribu
la kutupwa kwenye shimo (Mwanzo 37:20).
v Jaribu
la kuuzwa Misri (Mwanzo 39:1).
v Jaribu
la kulazimishwa kufanya uasherati na mke wa bwana wake(boss) (Mwanzo 39:6-9)
v Jaribu
la kufungwa Gerezani kwa kosa lisilo la kwake (Mwanzo 39:20)
MAJARIBU YANAYOLETWA NA SHETANI
Mtu
yeyote ambaye ana mbegu ya wokovu ndani yake lazima apitie majaribu mbalimbali
kwa sababu shetani hulenga kuondoa mbegu ya wokovu ndani yetu na kupanda mbegu
ya uasi ndani yetu.
Shetani
naye anaporuhusu majaribu huwa ana malengo makuum matatu.
v Analenga kututoa kwenye Imani.
v Analenga huduma au tusimtumikie Mungu.
v Analenga kumfanya mtu atende dhambi.
0 Maoni